Dar es Salaam. Waziri Mkuu, Dk Mwigulu Nchemba amezielekeza halmashauri zote kuweka wazi kuhusu fedha za miradi inayotekelezwa kwenye halmashauri husika kwa kile alichoeleza usiri unasababisha uchepushaji wa fedha za miradi.
Dk Mwigulu ametoa maelekezo hayo leo Mchi 8,2026 wakati akizungumza na wananchi wa Laela mkoani Rukwa ambapo aliagiza kuanzia sasa taarifa za fedha za miradi ya maendeleo zitolewe kwa viongozi mbalimbali ili kuongeza uwazi na uwajibikaji.
Hatua hiyo imekuja kufuatia kutoridhishwa na utekelezaji wa miradi kadhaa inayotekelezwa mkoani humo ikiwemo ya ujenzi wa shule, madarasa na bwalo ambapo licha ya kutolewa fedha kazi hizo hazijakamilika.
Akizungumza katika mkutano huo wa hadhara ametolea mfano miradi ya ujenzi wa shule ya sekondari na ya msingi ya Mzindakaya pamoja na ujenzi wa shule ya wasichana ya Mkoa wa Rukwa ambayo imeripotiwa kuchelewa licha ya kupokea fedha.
Waziri Mkuu, Dk Mwigulu Nchemba akizungumza alipokuwa katika ukaguzi wa maendeleo ya ukarabati na uboreshaji wa Uwanja wa Ndege wa Sumbawanga uliopo mkoani Rukwa.
Pamoja na majibu ya utetezi yaliyotolewa na baadhi ya viongozi, Waziri Mkuu hakuridhishwa na maelezo hayo na kuagiza uchunguzi wa kina ufanyike kubaini matumizi ya fedha hizo.
Kufuatia hilo amemtaka Kamanda wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) kufanya uchunguzi wa kina wa kila senti iliyotumika na kuwabaini wote waliohusika na ucheleweshaji huo. “Kamanda wa Takukuru nifanyie uchunguzi wa kina kila senti ilivyotumika na kila muhusika aliyehusika nipate taarifa yake. Hata kama ameshahama tutamfuata hukohuko.
“Kuanzia sasa fedha za maendeleo zikifika nakala iende kwa mkuu wa mkoa. Zikishatumwa halmashauri nakala apewe mkuu wa wilaya na mbunge. Fedha zikifika kwenye mradi nakala apewe diwani wa eneo husika haya mambo ya usiri yanasababisha uchepushaji wa fedha na wizi,” amesema. Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu pia ametangaza kupiga marufuku mfumo wa ununuzi wa mazao kwa kutumia kipimo cha lumbesa.
“Kufikia tarehe 20 mwezi huu ni marufuku kuuziana mazao kwa lumbesa kwa kuwa huo ni utaratibu wa kinyonyaji, wizi na ukandamizaji,” amesema.
Amesema Serikali inataka mauzo na manunuzi ya mazao yafanyike kwa vipimo sahihi ili kuwalinda wakulima dhidi ya unyonyaji. Pia amemwelekeza waziri wa kilimo kukutana na wanunuzi wa mazao na kuwaeleza kuwa hairuhusiwi tena kuwakopesha wakulima wakati wa kununua mazao yao. “Wajiandae kulipa fedha taslimu. Kama wanaona utaratibu wa kukopa ndiyo mzuri, basi nendeni mkakope benki ili mkifika kwa wakulima muwe na fedha,” amesema.
Katika hatua nyingine Dk Mwigulu ameweka msimamo mkali kwa viongozi wa mikoa na halmashauri akitaka ndani ya miezi sita baada ya kuanza kwa bajeti mpya kusiwe na shule, kituo cha afya wala zahanati isiyokuwa na maji au yenye upungufu wa vyoo, akionya kuwa uzembe katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo hautavumiliwa.
Waziri Mkuu, Dk Mwigulu Nchemba alipokuwa katika ukaguzi wa maendeleo ya ukarabati na uboreshaji wa Uwanja wa Ndege wa Sumbawanga uliopo mkoani Rukwa.
Dk Mwigulu ameagiza kila mkoa kutumia mitambo ya uchimbaji visima na huduma za maji iliyotolewa na Serikali kumaliza changamoto ya maji katika taasisi za huduma za jamii. “Naelekeza kila mkoa utumie mitambo iliyotolewa kwa ajili ya kumaliza changamoto ya maji. Tumieni hiyo mitambo. Miezi sita baada ya kuanza bajeti sitaki kuona shule, kituo cha afya wala zahanati isiyokuwa na maji,” amesema.
Amesisitiza kuwa kila mkoa tayari una mitambo hiyo, hivyo hakuna sababu ya shule kukosa huduma hiyo muhimu. “Wekeni kwenye vipaumbele vyenu vifaa vingine vitakavyohitajika kuhakikisha maji yanapatikana. Tunataka tuwe na mitambo inayofanya kazi, sio inayokaa tu,” ameongeza.
Mbali na suala la maji, Waziri Mkuu pia amegusia changamoto ya miundombinu ya vyoo mashuleni akitaka tatizo la upungufu wa matundu ya vyoo kumalizika ndani ya kipindi hicho hicho cha miezi sita. “Tunakuwaje nchi ambayo inaweza kutekeleza miradi mikubwa ya kielelezo halafu tuwe na shule ambazo hazina vyoo.”
Waziri Mkuu, Dk Mwigulu Nchemba akipewa maelezo alipokuwa katika ukaguzi wa maendeleo ya ukarabati na uboreshaji wa Uwanja wa Ndege wa Sumbawanga uliopo mkoani Rukwa.
Amewataka makatibu tawala wa mikoa kuwasimamia watendaji wa halmashauri kufanya tathmini ya mahitaji na kuyajumuisha kwenye bajeti ili kuondoa changamoto hiyo. “Fanyeni tathmini, wekeni kwenye bajeti. Sitaki kusikia tena habari ya upungufu wa matundu ya vyoo. Mambo mengine ni kupuuza tu, sio kwamba yanashindikana,” amesema.