Safari ya mjamzito aliyebebwa kwa machela kwenda kujifungua aeleza maumivu, ushujaa na furaha

Kilolo. Nadhani tunakumbuka picha ya mama mjamzito kutoka Kiwalamo, wilayani Kilolo, aliyebebwa kwa machela na wanakijiji akiwa katika uchungu wa kujifungua kutokana na barabara mbovu hadi Hospitali ya Dabaga kwenda kujifungua.

Hii ni simulizi ya kishujaa ya Zaineth Kipingi, mama wa Moreen, aliyejifungua kwa mara ya kwanza Juni mwaka huu akibebwa kwenye machela kutoka Kiwalamo Kilolo hadi Hospitali ya Dabaga, baada ya barabara ya kijiji hicho kuwa katika hali mbaya kiasi kwamba hakukuwa na uwezekano wa gari, pikipiki wala bajaji kupita kumpeleka hospitalini, licha ya kuwa alikuwa tayari ameanza kupata uchungu wa kujifungua.

Simulizi hii inaonyesha uchungu, mshikamano wa kijamii na furaha ya kukumbatia maisha mapya licha ya changamoto kubwa, ikionesha pia thamani ya kusaidiana katika jamii wakati wa dhiki.

“Nilipokuwa kwenye machela, nilihisi mchanganyiko wa hofu na matumaini na binafsi nilijisemea kimya, ‘Moreen, mama yako yupo hapa, tutaenda pamoja,’” anasema Zaineth.

Mama Moreen anasema alibebwa kwa machela kutokana na barabara ya Kiwalamo Kilolo kuwa mbovu sana, yenye mashimo, matope na utelezi, hali iliyofanya hata pikipiki au bajaji kushindwa kupita, huku gari likiwa haliwezi kabisa kufika eneo hilo.

“Nilihisi hofu ikinipamba huku nikiumia kwa uchungu wa kujifungua, lakini majirani walikuja bila kusita na waliunganisha nguvu zao wakitengeneza machela ya kienyeji kwa kutumia miti, turubai na kamba,” anasema Zaineth huku akiongeza kuwa:

“Wanaume walinisogeza mbele taratibu wakiwa wamenibeba kwenye machela, huku wanawake wakitoa maneno ya faraja wakisikika wakisema, ‘Usiogope Zaineth, tutakusaidia kufika salama,’ na mimi nilihisi maneno yao yakinyanyua uchungu wangu na kunipa matumaini katika kila pumzi niliyovuta.”

Zaineth anasema hatimaye walifika Hospitali ya Dabaga wilayani Kilolo mkoani Iringa, ambapo wahudumu wa afya walishangazwa na mshikamano wa wanakijiji walioungana kumsaidia kufika hospitalini salama.

Mama yake, Yunis Kikula, alijawa na machozi ya furaha huku akisema:

“Shukurani kwa kila mmoja aliyejitolea kwani bila msaada wenu, uwezekano huu ungekuwa mgumu sana.”

Zaineth sasa anasema kila anapomuangalia mtoto wake akicheza anakumbuka kuwa,

“hakuna kitu katika maisha kinachoweza kushinda moyo uliojaa matumaini na upendo,” kwani safari ya Moreen ni ushuhuda wa mshikamano wa kijamii, ujasiri na thamani ya kusaidiana.

Zaineth anasema upendo na mshikamano aliouona siku hiyo ulimfundisha somo kubwa kuwa kutoa msaada kwa wengine ni njia ya kuleta maisha, tumaini na furaha isiyo na kikomo.

“Safari yetu imebaki moyoni mwangu daima kama kumbukumbu ya ujasiri na mshikamano. Nilijua chochote kilichotokea kilikuwa ni sehemu ya maisha iliyotufundisha thamani ya kusaidiana,” anasema Zaineth.

Atoa ushauri kwa wanawake wajawazito

Zaineth Kipingi anasema uzoefu alioupitia ulimfundisha kuwa mwanamke ana nguvu kubwa ya kuvumilia changamoto za uzazi hata katika mazingira magumu.

Anaeleza kuwa wanawake wanapaswa kujiamini na kuamini kuwa licha ya mazingira magumu wakati wa kujifungua watoto, bado wanaweza kuvuka salama iwapo watajitunza na kupata ushauri wa kitaalamu.

“Niseme tu jambo la kwanza ni wanawake kujitunza na kufuatilia afya zao wakati wa ujauzito, pamoja na kuhakikisha wanapata ushauri wa wataalamu wa afya kadri inavyowezekana,” anasema Zaineth huku akiongeza kuwa:

“Hata kama mazingira ni magumu, maandalizi na uelewa wa hali ya ujauzito vinaweza kusaidia kupunguza hatari wakati wa kujifungua.”

Zaineth anaendelea kuwahimiza wanawake kuwa na moyo wa uvumilivu na kutokata tamaa wanapokutana na changamoto wakati wa kujifungua.

Anasema wakati mwingine safari ya uzazi inaweza kuwa ngumu kuliko ilivyotarajiwa, lakini nguvu ya mama pamoja na msaada wa jamii vinaweza kufanya mambo yawezekane.


“Wanawake wenzangu wasikate tamaa wanapokutana na mazingira magumu, kwa sababu nguvu ya mama ni kubwa kuliko changamoto,” anasema Zaineth.

Pia anasisitiza umuhimu wa mshikamano wa familia na jamii katika kusaidia wanawake wajawazito, hasa vijijini ambako huduma za afya na miundombinu mara nyingi huwa changamoto.

Zaineth anasema kwake Siku ya Wanawake Duniani, iliyoadhimishwa jana Machi 8, ni kama dhahabu inayong’aa katika maisha ya wanawake kwa sababu inakumbusha thamani, nguvu na mchango mkubwa wa mwanamke katika jamii.

“Tukumbuke kuwa wanawake tunapitia changamoto nyingi katika maisha yao kuanzia malezi ya familia, kazi za kila siku hadi jukumu la kuzaa na kulea watoto, hivyo siku hiyo ni ishara ya kutambua na kuheshimu juhudi zetu,” anasema Zaineth.

Vilevile anaeleza kuwa mwanamke ni kama shina na mzizi wa maisha ya binadamu, kwani kupitia mwanamke ndipo kizazi kipya kinazaliwa na jamii inaendelea kuwepo.

Kwa mtazamo wake, bila mwanamke dunia isingekuwa na mwendelezo wa maisha, jambo linaloifanya nafasi ya mwanamke kuwa ya kipekee na yenye thamani kubwa katika jamii.

“Bila mwanamke watu wasingeweza kuzaliana wala dunia kuendelea, hivyo kuwa mwanamke ni bahati na tunapaswa kujivunia nafasi yetu katika jamii,” anasema Zaineth.