Global Publishers
March 8, 2026
0 Comments
WAZIRI MKUU, Dkt. Mwigulu Nchemba amesema kuwa Serikali itachukua hatua kali ikiwemo kufilisiwa kwa yeyote anatakayebainika kuhujumu wakulima kwa kuwauzia pembejeo zisizokuwa na ubora zikiwemo mbegu.
Ameyasema hayo leo Jumapili, Machi 08, 2026 alipozungumza na wananchi katika mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye Uwanja wa Shule ya Msingi Laela A wilayani Sumbawanga, Rukwa. Amesisitiza kuwa watu hawatovumiliwa kwa kuwa wana lengo la kuliingiza Taifa katika njaa.
Waziri Mkuu ametoa kauli hiyo baada ya Mbunge wa Viti Maalumu, Sylvia Sigula kuishukuru Serikali kwa kuwapatia ruzuku ya pembejeo ila ameiomba Serikali kuwatatulia changamoto ya kuuziwa mbegu zisizokuwa na ubora jambo linalosababisha wakulima kupata hasara kwani kilimo ndio uchumi wa Rukwa.

Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Kilimo, David Silinde amesema wizara amekuwa ikifanya uchunguzi na kuchukua hatua pale inapobaini kuwepo kwa pembejeo zisizokuwa na ubora na tayari kuna mtu mmoja amekamatwa mkoani humo.
Vilevile, Naibu Waziri huyo ametumia fursa hiyo kuwaelimisha wananchi kuwa mbegu na mbolea za ruzuku zinazotolewa na Serikali zinakuwa na namba za utambuzi ambazo ukiingiza kwenye namba *148*52# itaeleza kama ni halali, hivyo amewasisitiza wakulima kuendelea kuwa makini.

Awali, Waziri Mkuu alitumia fursa hiyo kuwasisitiza Watanzania kwamba mambo yote yaliyomo kwenye Ilani ya Uchaguzi yatatekelezwa kwa vitendo kwa kuwa Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ni mtu wa matokeo na akisema jambo anatekeleza.
“Watu wa Rukwa ni mashahidi kutokana na utekelezwaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo katika maeneo yenu ikiwemo ujenzi wa hospitali za wilaya, vituo vya afya na shule za msingi, sekondari na za amali, hili ni jambo kubwa linaloleta heshima kwa nchi.” 