Mwenyekiti wa Umoja wa Wanazuoni wa Kiislamu, Sheikh Abdallah Swallehe Ndauga, amewahimiza Waislamu kutekeleza ipasavyo ibada ya Zaka ili kusaidia kupunguza umasikini katika jamii.
Alisema kwa mujibu wa mafundisho ya dini ya Kiislamu, Zaka imewekwa mahsusi ili kuwainua watu wasiojiweza pamoja na kuimarisha mshikamano wa kijamii miongoni mwa waumini wa dini hiyo.
Sheikh Ndauga alieleza kuwa Waislamu wakitekeleza ibada hiyo kwa uaminifu na kwa kuzingatia maelekezo ya dini, inaweza kuwa nyenzo muhimu ya kupunguza umasikini na kuboresha maisha ya watu wengi.
Alisema baadhi ya watu wamekuwa wakidai kuwa Zaka inapaswa kutolewa kwa yatima pekee bila kuzingatia mafundisho sahihi ya Kiislamu kuhusu makundi yanayostahili kupewa Zaka.
Sheikh Zuberi alifafanua kuwa katika mafundisho ya Kiislamu, yatima hawakutajwa moja kwa moja miongoni mwa makundi ya wanaostahili kupewa Zaka isipokuwa pale wanapokuwa katika hali ya umasikini.
Wanazuoni hao walisisitiza umuhimu kwa Waislamu kujifunza na kuelewa kwa usahihi mafundisho ya dini kuhusu utoaji wa Zaka ili kuhakikisha ibada hiyo inatekelezwa kwa mujibu wa utaratibu uliowekwa.
