Safari ya Monica kutoka kwenye soka hadi fundi simu Kariakoo

Dar es Salaam. Kwa nje, unaweza kumuona kama fundi simu wa kawaida anayefanya kazi zake Kariakoo lakini nyuma ya meza yake ya kazi, kuna historia ya kipekee ya maisha ya soka, mapambano ya majeraha na uamuzi wa kuanza upya.

Hii ni safari ya Monica Conrad, mchezaji wa zamani wa mpira wa miguu wa wanawake aliyewahi kuwa sehemu ya waanzilishi wa Yanga Princess.

Monica anaanza simulizi yake kwa kukumbuka alikotoka kwa kusema mpira haukuwa jambo la ghafla maishani mwake, bali ni kitu alichokulia nacho tangu utotoni.

“Mpira nilianza nikiwa na miaka mitano kwa mujibu wa kaka yangu nilikuwa nacheza na watoto wenzangu. Lakini rasmi nilianza nikiwa na miaka 15 nikiwa najitambua,” anasema.

Anakiri wakati huo hakujiona akifanya vizuri katika masomo, jambo lililomfanya aweke nguvu zaidi kwenye kipaji chake. Hata hivyo, familia yake haikuridhishwa na uamuzi huo mwanzoni.

“Familia yangu hawakutaka nicheze mpira wao waliamini kwenye masomo lakini baadaye walinielewa na wakaniunga mkono,” anasema.

Miongoni mwa waanzilishi wa Yanga Princess

Monica anasema mpira ulikuwa sehemu ya maisha yake, si burudani tu bali ndoto aliyoiishi kila siku.

Hatua muhimu katika safari yake ilikuja alipojiunga na Yanga Princess, kipindi ambacho timu ya wanawake ilikuwa bado inaandaliwa.

Anasema yeye na wenzake walikuwa miongoni mwa waanzilishi wa Yanga Princess kabla haijaingia rasmi kwenye ligi. Walifanya kazi kubwa kuijenga timu, kuandaa kikosi na kuweka msingi wa ushindani.

“Kabla timu hii haijaingia kwenye ligi, sisi ndio waanzilishi nilichukuliwa nikiwa Mash Queens baada ya kuonekana kuwa nina kipaji ambacho kitakuwa msaada katika ujenzi wa wa timu ili ipande na isimame vizuri,” anasema.

Monica anasema licha ya jitihada zote hizo lakini alidumu Yanga kwa misimu miwili, kwani kulikuwa na mabadiliko ya makocha hivyo kila mmoja na harakati zake katika kuwezesha timu inafanya vizuri na kufikia malengo.

Hata hivyo, anasema Kipindi hicho hakukuwa na malipo makubwa kama ilivyo sasa katika baadhi ya timu, lakini walicheza kwa mapenzi na ari ya kutengeneza historia.

“Malipo hayakuwa makubwa, lakini tulikuwa tunacheza kwa kujituma. Hata kidogo unachopata, unakishukuru,” anasema.

Anasema baadaye alirejea Mash Queen ya Mwanza, ambako alipapata mapenzi ya kipekee na jiji hilo. Ndani ya timu hiyo, alichaguliwa miongoni mwa wachezaji nane waliokwenda kusaidia Baobab Queens kupanda daraja.

“Katika timu yetu tulitoka wachezaji nane kwenda kusaidia Baobab, na tulifanikiwa kufika hatua za juu ambazo ziliwavutia Fountane Gate na kuingia nao mkataba mwaka 2019,”anasema

Anasema huko alicheza kwa miaka miwili kabla ya kupatwa na jeraha la kifundo cha mguu (Ankle) lililobadilisha kabisa mwelekeo wa maisha yake.

“Jeraha lilikuwa kubwa kiasi cha kunilazimu kukaa nyumbani kwa muda mrefu na hatimaye kuachana na soka la ushindani kwani kila nikitibiwa ilikuwa ngumu kupona hata hospitali waliniwekea hogo mara saba lakini ilishindikana,”anasema.

Anakiri kuwa ulikuwa wakati mgumu kwake kwa sababu mpira ulikuwa sehemu kubwa ya maisha yake lakini hakuwa na namna zaidi ya kukubali hali halisi.

Katika kipindi chake cha uchezaji, Monica anasema amepitia mikono ya makocha mbalimbali, lakini anamtaja Maalim Salehe kama kocha aliyemuelewa zaidi.

“Kocha Maalim Salehe alinielewa sana, nilikuwa napenda kukaa na mpira, lakini alinifundisha kucheza kwa akili na kujenga tabia ya toa moja, achia moja, ili nisiumie na timu icheze vizuri,” anasema.

Anasema mafunzo hayo yalimsaidia kubadilika na kuwa mchezaji anayefikiria zaidi kwa manufaa ya timu.

Monica Conrad, (kushoto) akizungumza na mwandishi wa Mwananchi, Devotha Kihwelo.



Baada ya kukaa nyumbani kwa muda kutokana na jeraha, kaka yake alimshauri aende Kariakoo kujifunza ufundi. Hapo ndipo ukurasa mpya wa maisha yake ulipoanza.

“Kaka yangu aliniambia niende naye Kariakoo nijifunze ufundi kwa sababu sikuwa na kazi nyingine baada ya kuachana na mpira rasmi hivyo nilianza kwa kuangalia, taratibu nikajifunza,” anasema.

Monica anasema hana elimu rasmi ya ufundi, lakini alijifunza kwa vitendo na anaamini kipaji hicho ni neema kutoka kwa Mungu.

“Mungu ndiye fundi wangu si kila kitu lazima usome darasani, kuna vingine unajifunza kwa kuangalia na kujituma mengine yanafuata ndicho nilichokifanya mimi tangu mwaka 2024,” anasema.

Hata hivyo, anasema mwanzo haukuwa rahisi akiwa mwanamke katika kazi inayotawaliwa na wanaume, alikumbana na changamoto ya kutokuaminiwa na wateja.

“Kwa kweli mwanzoni ilikuwa ngumu watu walikuwa wananiona mtoto wa kike siezi kufanya kazi ya wanaume husasni ufundi simu hivyo hawakuniamini haraka,” anasema.

Anasema kwa uadilifu, kutokata tamaa na kazi nzuri, amejenga jina lake na sasa ana wateja wanaompigia simu moja kwa moja na kumuamini kwa kumuachia simu pamoja na kuomba msaada wa kutafutiwa simu kutokana na uzoefu wake.

“Sasa wananipigia simu, wananiamini mtu anaweza kuniambia niletee simu fulani, najua utanisaidia pia wakati mwingine wanatuma watu wao kuniletea simu zilizoharibika,” anasema.

Pia, anasema changamoto kubwa iliyopo ni ushindani mkubwa katikati ya wanaume pamoja na mamlaka za jiji kutowaruhusu kufanya shughuli zao pembezoni mwa barabara.

“Changamoto iliyopo, mafundi tuko wengi na zamani kulikuwa na mikwaruzano baina yetu na mamlaka za jiji, lakini sasa hali imetulia. Tunashukuru Mungu kwa riziki ya kila siku ambayo sikosi Sh 30,000,” anasema.

Monica anasema sasa anaangalia mbele ndani ya miaka miwili ijayo, anatarajia kupanua biashara yake endapo atafanikiwa kupata mtaji hata kwa njia ya mkopo kwani biashara zake anazofikiria kiwango cha juu ni Sh1 milioni.

“Nina mpango wa kuwekeza zaidi na kufungua biashara zangu mwenyewe, angalau vitengo viwili au vitatu kwa sasa kinachonikwamisha ni mtaji kwani nimechoka kukimbizana na mamlaka,” anasema Monica.

Anasema hataki kubaki barabarani kusubiri wateja wa kupita, bali anataka kuwa na duka rasmi na biashara imara itakayompa uhakika wa kipato.