Tumsifu Yesu Kristo. Nakusalimu kwa jina la Bwana wetu Yesu Kristo aliye hai. Ni matumaini yangu kuwa, kwa neema ya Mungu, unaendelea vizuri. Ninamshukuru Mungu kwa kunipa kibali cha kusema na wewe siku ya leo, ikiwa ni Siku ya Wanawake Duniani.
Maadhimisho ya mwaka jana, kupitia ukurasa huu, nilipata pia kibali cha kukukumbusha juu ya umuhimu wa kuwaandaa watoto wa kiume kuwa bora. Sijajua ni kwa kiasi gani tangu mwaka jana umetia juhudi katika kuhakikisha unamlea mwanao wa kiume katika misingi inayompendeza Mungu.
Mithali 19:13a inasema: “Mwana mpumbavu ni msiba kwa babaye,” na Mithali 17:20: “Mwana mpumbavu ni huzuni kwa babaye na uchungu kwa mamaye aliyemzaa.” Kumbe jukumu la malezi ni kwa wazazi wote wawili, na kwa hakika halipaswi kuwa jukumu la mama peke yake.
Leo, ikiwa ni siku ya maadhimisho ya Wanawake Duniani, napenda kuwashukuru na kuwapongeza kina baba kwa namna wanavyoendelea kuwa mstari wa mbele katika kutuunga mkono kwa jitihada zote tunazoonesha ili kujikwamua. Mungu awabariki sana.
Tafakari ya ujumbe wa leo inasema: Simama katika zamu yako. Kama mama na mke katika familia, kuna wajibu ambao Mungu ametupatia. Wajibu huo, iwapo kila mama atautekeleza, basi tutakuwa na familia bora, kanisa imara na taifa lenye nguvu.
Hebu tuone sasa baadhi ya majukumu ya mwanamke katika familia, jamii, kanisa na taifa kwa ujumla.
Suala la maombi si jukumu la mama fulani, kila mwanamke anawajibika kuomba kwa ajili ya familia yake, jamii, kanisa na taifa lake. Unapokumbana na changamoto mbalimbali, ni vizuri kama mama kutambua kuwa mahali sahihi pa kupeleka matatizo yako ni kwa Mungu peke yake.
1 Petro 5:6-7 inasema: “Huku mkimtwika yeye fadhaa zenu zote, kwa maana yeye hujishughulisha sana na mambo yetu.” Mungu anajishughulisha na kila changamoto uliyonayo, hivyo mahali sahihi pa kupeleka shida zako ni kwa Mungu. 1 Samweli 1:10 inasema: “Naye huyo mwanamke alikuwa na uchungu rohoni mwake, akamwomba Bwana, akalia sana.” Uchungu wa Hana ulitokana na yeye kukosa mtoto, jambo lililopelekea kusimangwa na mke mwenzake.
Hana alitambua mahali sahihi pa kupeleka shida zake. Alijisogeza mbele za Mungu, akaomba kwa machozi mengi, huku akimsihi Mungu aone taabu lake na aweze kumpatia mtoto. Mungu alisikia maombi ya Hana, baada ya mateso ya muda mrefu na kuomba sana, Mungu alimpatia mtoto Samweli. Haijalishi unapitia nini, wewe mweleze tu Mungu, naye atakusaidia.
b. Mwanamke ni mtetezi na mlinzi wa familia yake
Tunajifunza kutoka kwa Abigaili (1 Samweli 25). Mama huyu, baada ya kugundua mumewe amefanya kosa kwa kushindwa kuwatendea mema watumishi wa Mfalme Daudi, Daudi alikusudia kuwaua wote wa nyumbani mwake.
Mama huyu alipata taarifa za kile mumewe amefanya na kile Daudi amekusudia juu ya familia yake. Mstari wa 17 unasema: “Basi sasa ujue na kufikiri utakayotenda, kwa sababu yamekusudiwa mabaya juu ya bwana wetu na juu ya nyumba yake yote.”
Alipopata tu taarifa hii, aliingilia kati. Mstari wa 18 unasema: “Ndipo Abigaili akafanya haraka, akatwaa mikate mia mbili, na viriba viwili vya divai, na kondoo watano waliofanyizwa tayari, na vipimo vitano vya bisi, na vishada mia vya zabibu, na mikate ya tini mia mbili; akavipakia vitu hivi juu ya punda.”
Akawambia vijana wake: “Haya tangulieni.” Mama huyu aliwahi kwa Daudi kuomba msamaha kwa ajili ya bwana wake ili uovu uliokusudiwa katika familia yake usiwapate. Mstari wa 24 unasema: “Akamwangukia miguuni pake, akasema, Bwana wangu, juu yangu mimi na uwe uovu, tafadhali mjakazi wako na anene masikioni mwako, nawe uyasikilize maneno ya mjakazi wako.”
Ili familia yake iwe salama, mama huyu anaamua kubeba uovu wa mumewe. Ni wanawake wangapi watasimama katika zamu zao kama Abigaili? Ni wangapi wanaokumbuka kuomba toba na rehema kwa ajili ya waume zao? Wangapi wanaweza kulipia maovu ya waume zao?
Mama huyu alianguka miguuni pa Daudi, akainama mpaka nchi na kusema: “Usimwangalie huyu mtu asiyefaa, yaani Nabali; kwa maana kama lilivyo jina lake, ndivyo alivyo yeye. Jina lake ndilo Nabali, na upumbavu anao.”
Wewe mama unamjua mumeo vizuri, udhaifu wake unaujua. Ni nini unafanya anapokosea? Kumtangaza kwa shoga zako kana kwamba watakusaidia? Hilo ni jukumu lako. Aibu ya mumeo ni aibu yako, tatizo lake ni lako pia.
Unammudu mumeo, ndiyo maana ukapewa huyo. Pale alipo dhaifu, upo kumkamilisha na si vinginevyo.
Punguza kulalamika juu ya familia ambayo Mungu amekuamini na kukupatia. Ni jukumu lako kuilinda.
Yeremia 31:22 inasema: “Kwa maana Mungu ameumba jambo jipya duniani; mwanamke atamlinda mwanamume.” Ulinzi wetu ni kupitia maombi na si kukagua simu zao na kutafuta ugomvi.
Hakuna mkate mgumu kwenye chai. Mama, ukikaa vizuri, ukatimiza majukumu yako na kutambua nafasi yako, hakuna siku utajuta. Nyumba yako itakuwa baraka, na kupitia wewe wengi watabarikiwa.
Mhubiri Peace Marino anatoka Kanisa la KKKT Nyashimo, Busega mkoani Simiyu. Kwa maombi na ushauri 0783 999 044.