Itilima. Mwananchi wa Kijiji cha Lagangabilili wilayani Itilima, mkoani Simiyu, Mzee Majija Madata amewasilisha malalamiko kwa Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Kenani Kihongosi, akidai kudhulumiwa shamba lake na mmoja wa viongozi wa CCM katika ngazi ya wilaya mkoani Shinyanga.
Kihongosi yupo mkoani Simiyu tangu Machi 7, 2026 kwa ziara ya kikazi inayolenga kukagua utekelezaji wa miradi ya maendeleo iliyopatiwa fedha na Serikali, kusikiliza changamoto za wananchi pamoja na kufuatilia uhai wa chama hicho.
Akizungumza katika mkutano wa hadhara uliofanyika juzi jioni katika Kijiji cha Lagangabilili, Madata aliomba nafasi ya kuzungumza na alipopewa nafasi hiyo alimueleza Kihongosi kuwa eneo lake lililopo Mwakitolyo limechukuliwa na kiongozi mmoja wa chama katika ngazi ya wilaya.
Alidai kuwa tayari alishinda kesi mahakamani kuhusu umiliki wa eneo hilo, lakini licha ya uamuzi huo bado anaendelea kudhulumiwa na kiongozi huyo.
Akijibu malalamiko hayo, Kihongosi alisema hakuna kiongozi wa chama aliye juu ya sheria na kusisitiza kuwa CCM haitasita kuchukua hatua dhidi ya viongozi watakaobainika kuwaonea au kuwadhulumu wananchi.
Alimuagiza Mkuu wa Wilaya ya Itilima, Anna Gidarya, kufuatilia kwa karibu suala hilo ili kuhakikisha mwananchi huyo anasikilizwa na uchunguzi unafanyika.
“Mkuu wa wilaya msikilize mwananchi huyu na uwasiliane na Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga kumtafuta kiongozi anayelalamikiwa ili haki itendeke. Endapo tuhuma hizo zitathibitika, hatua za kisheria zichukuliwe mara moja ili mwananchi apate haki yake,” alisema Kihongosi.
Wananchi wa kijiji cha Lagangabilili wakiwa kwenye mkutano wa hadhara wa Chama cha Mapinduzi (CCM), katika ziara ya Katibu wa NEC Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa CCM, Kenan Kihongosi wilayani Itilima mkoani Simiyu.
Alisisitiza kuwa kama itabainika kiongozi huyo alihusika na vitendo vya kumdhulumu mwananchi, hatua kali za kisheria zitachukuliwa bila kujali nafasi au cheo chake ndani ya chama.
Kihongosi alisema viongozi wanapaswa kutumia madaraka waliyopewa kuwatumikia wananchi kwa haki na uadilifu badala ya kuwanyanyasa au kuwadhulumu.
“Ndani ya chama hakuna aliye juu ya sheria. Atakayeharibu anashughulikiwa hapo hapo,” alisema.
Aliongeza kuwa CCM ina mifumo imara ya kusimamia nidhamu na kuwawajibisha viongozi wake ili kulinda haki na usawa kwa wananchi.
Katika ziara hiyo mkoani Simiyu, Kihongosi alianza wilayani Maswa kabla ya kuendelea Itilima na baadaye alifanya mkutano wa hadhara wilayani Bariadi.
Katika mikutano hiyo, Kihongosi aliwahimiza wananchi kuendelea kuiunga mkono Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan pamoja na CCM, akisisitiza kuwa chama hicho kinaendelea kusimamia utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika sekta mbalimbali.