Bahati itawabeba waamuzi wetu AFCON 2027      

Mechi ya Watani wa Jadi (Derby) katika soka, kikawaida huwa ndio mchezo unaovutia na kuteka hisia za kundi kubwa la watu katika soka kwenye nchi husika.

Ni mechi kati ya timu mbili ambazo zina ushindani mkubwa, mara nyingi kwa sababu zinatoka eneo moja (mji au kanda moja) au zina historia ndefu ya ushindani.

Klabu mbili zenye utani wa jadi zinapokutana, hapana shaka unakuwa ni mchezo unaobeba alama na utambulisho wq soka la ngazi ya klabu kwa nchi husika na kwa vile hufuatiliwa na idadi kubwa ya watu, unaweza kuwa chanzo cha fursa nyingi kwa wachezaji, maofisa wa timu na maofisa wa mchezo.

Kwa hapa Tanzania, mechi kubwa ya Watani wa Jadi ni ile inayozikutanisha timu za Simba na Yanga ambazo zote zilianzishwa katika maeneo yanayokaribiana, zimetwaa idadi kubwa ya matawi lakini pia ndio zenye namba kubwa ya mashabiki.

Ni mchezo unaosimamisha nchi kwa muda pindi unapochezwa lakini pia hushirikisha namba kubwa ya mashabiki na wasimamizi wa mchezo kulinganisha na mingine ya ligi.

Kwa mwaka huu, timu hizo zilikutana Jumapili, Machi Mosi katika Uwanja wa New Amaan Complex ukiwa ni mchezo wa Ligi ambao ulimalizika kwa sare tasa ya bila kufungana.

Kama ambavyo imeainishwa awali kuwa mchezo huo unaweza kuwa fursa au ukageuka shubiri kwa wachezaji na maofisa wa mechi na miongoni mwao ni marefa wa mchezo.

Kwa mazingira yaliyotokea kabla, wakati na baada ya mechi, kuna uwezekano mchezo huo ukawaweka katika wakati mgumu sana marefa wetu wa Tanzania kueleka Fainali za Mataifa ya Afrika (AFCON) 2027 ambazo zitafanyika hapa kwa kushirikiana na Kenya na Uganda.

Kabla ya mchezo, tuliamua refa wa kati asiye na beji ya uamuzi ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Duniani (FIFA) ashike filimbi kuchezesha mechi huku wale wenye beji tukiamua kutowatimua.

Tanzania ina marefa saba wa kati wenye beji ya FIFA. Mechi kama hizo ndio jukwaa zuri kwao kuonyesha utayari wao katika maandalizi yao miezi michache kabla ya kufanyika kwa fainali za AFCON 2027.

Kutompa nafasi angalau mmoja kati yao, kunaweza kufanya tutafsirike ama tumepoteza imani na waamuzi wetu au wenyewe hawana uwezo na viwango vya kusimama kati kwenye mechi hiyo.

Fursa nzuri ya kulishawishi Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) ilikuwa ni mchezo huo kuchezeshwa na refa wa kati mwenye beji ya FIFA. Kutotoa fursa hiyo kunawapa uhalali CAF kutowatumia kwenye fainali zijazo za AFCON.

Kama sisi hatukuwaamini katika mechi yetu kubwa basi hatutokuwa na haki ya kuwahoji CAF ikiwa haitowatumia katika mashindano yake makubwa.

Wakati wa mchezo, marefa wetu wawili wasaidizi wenye beji ya FIFA wakafanya makosa mawili ya kushindwa kutafsiri vyema sheria ya kuotea ambapo kila mmoja alifanya kosa moja.

Na baada ya hapo, mmoja akafungiwa kuchezesha kwa muda wa miezi mitatu na mwingine hatochezesha kwa kipindi cha miezi sita.

Adhabu hizi zinaweza kuipa uhalali kamati ya marefa ya CAF kutotupa nafasi katika fainali za AFCON 2027 na kisha fursa hiyo kuielekeza kwa marefa wa mataifa mengine.

Kipindi hiki ambacho tumebakiza muda mfupi kabla ya kufanyika kwa Fainali za AFCON hapa nchini, tulipaswa kuhakikisha tunatengeneza taswira nzuri kwa marefa wetu wa kati na wale wasaidizi.

Njia mojawapo ni kuwapa fursa ya kuchezesha mechi kubwa kama ya watani wa jadi lakini wao wenyewe marefa pia walipaswa kujilinda kwa kuhakikisha wanachezesha vyema na kuepuka mazingira ambayo yatatia doa uamuzi wao.

Hata hivyo, imekuwa kinyume ambapo marefa wetu saba wa kati wenye beji ya FIFA hawakupata fursa hadhimu ya kuishawishi CAF kupitia Dabi ya Kariakoo na wasaidizi wao ambao walipata nafasi hiyo wakajiangusha kwa kufanya kosa jepesi ambalo mwishoni limesababisha wafungiwe.

Ikitokea CAF hawajachagua refa kutoka Tanzania kwenye AFCON 2027, hatutokuwa na wa kumlaumu zaidi ya sisi wenyewe na kama akichaguliwa au wakichaguliwa, itakuwa wameamua kutufanyia hisani tu.