Fei Toto awaibua wakongwe Ligi Kuu Bara

WAKATI Ligi Kuu Bara ikiwa imesimama kupisha Kombe la Shirikisho la CRDB (FA),  Feisal Salum ‘Fei Toto’ ndiye kinara anayehusika kwenye mabao hadi sasa akikaribiwa na mshambuliaji wa Yanga, Prince Dube, huku wachezaji wa zamani wakimpa maua yake.

Kwenye chati ya ufungaji Fabrice Ngoy wa Namungo ndiye anaongoza kwa kufunga mengi akiwa nayo nane mbele ya Dube mwenye sita huku Fei akiwa nafasi ya tatu na mabao matano.

Hata hivyo, takwimu za jumla zinamfanya Fei kuwafunika mastaa hao wageni, kutokana na kuwa kinara wa pasi zilizazaa mabao akiwa nazo nne, hivyo kumfanya awe amehusika kwenye mabao tisa hadi sasa, akifuatiwa na Ngoy ambaye amefunga nane bila pasi ya bao, huku Dube akifunga sita na pasi moja ya bao hivyo amehusika kwenye mabao saba.

Ukiachana na data za msimu huu, misimu miwili nyuma Fei Toto 2024/25 alifunga mabao 4 na asisti 13, 2023/24 mabao 19, alimaliza na asisti 7, wakati Dube 2024/25  alifunga mabao 13 na asisti nane.

Msimu wa 2023/24 alikuwa na mabao 7 asisti 2, 2024/25 akiwa Geita kabla ya kwenda nje Mwalimu alikuwa na mabao sita na msimu wa 2023/24 hakuwa na bao wala asisti.

Kitendo cha Fei Toto kuhusika kwa mabao mengi akiwa ni mzawa pekee hadi sasa, kimemuibua kiungo mshambuliaji wa zamani wa Simba, Yanga na Taifa Stars, Haruna Moshi ‘Boban’ aliyesema:


“Ni kitu kizuri kuona uwiano wa ushindani wa wachezaji wazawa na wageni, kikubwa Fei Toto ni kati ya vipaji vikubwa anapaswa kukaza buti, ili akimaliza msimu data zake ziwe juu.”

Mchezaji mwingine wa zamani aliyelizungumzia hilo ni Nurdin Bakari aliyesema: ”Ligi kwa ujumla ina ushindani, napenda anachokifanya Fei Toto msimu wa 2023/24 alitengeneza bato na aliyekuwa mshambuliaji wa Yanga, Aziz Ki aliyemaliza na mabao 21 yeye akamaliza na 19.

“Ukiachana na Fei Toto pia George Mpole akiwa Geita Gold alimaliza na mabao 17, alitengeneza bato kali na aliyekuwa mshambuliaji wa Yanga, Fiston Mayele ambaye alimaliza na 16 nyakati hizo, hilo linaleta heshima kubwa kwa wazawa kuthamini vipaji vyao.”

Mshambuliaji wa Tanzania Prisons, Jeremiah Juma ambaye ana bao moja kwenye ligi alisema:

”Napenda kuuona ushindani wa wazawa mbele ya wageni, asiwe Fei Toto peke yake na hilo linachangia ligi kuwa nzuri na bora kwa upande wa Mwalimu ni mchezaji mzuri akiamini kupewa nafasi ya mara kwa mara naamini idadi ya mabao itaongezeka.”