SIMBA inahesabu kubwa sana za kusuka zaidi kikosi na sasa kuna msako unafanyika wakipambana kunasa mashine moja ya mabao pale walipotoka mastaa wengi akiwemo Anicet Oura.
Simba ilifanya usajili mkubwa kwenye dirisha dogo la usajili na sasa imerejea kwenye makali yake baada ya kuanza msimu kwa kusuasua, lakini kiwango ambacho wameonyesha kwenye michezo ya hivi karibuni ukiwemo ule wa Derby ya Kariakoo imeonekana kuwarudisha kwenye makali yao.
Iko hivi, mwisho wa msimu huu mshambuliaji Seleman Mwalimu kwa mujibu wa mkataba wake wa mkopo atatakiwa kurudishwa klabu yake ya Wydad Athletic ya Morocco ambao ndio wataamua tena kumuachia au kusalia huko kwa kuwa mkataba wake ulikuwa wa mkopo wa msimu mmoja na hauna kipengele cha Simba kumnunua moja kwa moja.
Achana na Mwalimu kuna Jonathan Sowah huyu naye sio uhakika kama ataweza hata kumaliza msimu huu, kutokana na sintofahamu kati yake na uongozi wa timu hiyo juu ya madai ya utovu wa nidhamu na inaelezwa kuwa mwishoni mwa msimu huu ataachana na timu hiyo ya Msimbazi.
Hesabu hizo zimewarudisha Simba sokoni mapema wakiona kuna umuhimu wa kutafuta mashine sahihi ya kufunga mabao na unavyosoma taarifa hii kuna mazungumzo yanaendelea kati ya wekundu hao na Souleymane Fofana ambaye anacheza eneo la ushambuliaji.
Hii ina maana kuwa Simba kwenye eneo hilo itakuwa na mastaa wanne wenye moto mkali ambao ni Fofona, Libasse Gueye, Anicet Oura pamoja na Inno Loemba, itakuwa safu hatari sana.
Fofana ni tishio jipya kwenye kikosi cha Asec Mimosas ya Ivory Coast akiwa na kasi ya kufunga mabao ya kiufundi, timu ambayo ilimpika staa wa Simba kwa sasa winga Oura kabla ya kuuzwa Ulaya na sasa akadondoshwa kwa wekundu hao, lakini pia wamewahi kucheza hapo mastaa mbalimbali wakiwemo Stephen Aziz KI, Anthony Tra Bi Tra, Kouassi Yao, Pacome Zouzoua, Aubin Kramo na Josaphat Arthur Bada
Simba inamtaka Fofanba ili kuongeza ubora kwenye safu yao ya ushambuliaji huku uongozi unaomsimamia mshambuliaji huyo ukiwa hauna shida na kufanikisha dili hilo.
Hata hivyo chanzo chetu kimetueleza kuwa uhakika kwa Simba kumpata Fofana upo kwenye uongozi wa Asec kutokana na mshambuliaji huyo kubakiza mkataba wa mwaka mmoja na nusu na klabu hiyo bingwa wa kutengeneza vipaji.
Msimu huu namba za Fofana zipo juu akiwa ameshafunga jumla ya mabao 11 kwenye mechi 21 alizocheza akiwa ndio mfungaji kinara ndani ya timu hiyo.
Achana na kufunga Fofana pia ni mjuzi wa kutengeneza mabao akiwa na jumla ya asisti tano na kumfanya kuhusika kwenye jumla ya mabao 16 kwenye timu yake.
Mshambuliaji huyo mwenye nguvu na mwili mkubwa unaompa urahisi kupambana na mabeki, silaha yake nyingine ni kwamba anaweza kufunga kwa miguu yote kwa ubora mkubwa.
“Tunaendelea na mazungumzo unajua kazi ya kusuka kikosi haiwezi kufanyika kwa dirisha moja, tulianza dirisha hili lakini tunataka kuongeza wengine bora dirisha lijalo kama tukifikia makubaliano na wasimamizi wake na uongozi wa Asec,”alisema bosi mmoja wa juu wa Simba.
“Fofana ni mchezaji mzuri mwenye uwezo mkubwa, tukimpata utakuwa usajili mzuri, bado mdogo miaka 19 ni mchezaji ambaye tunaweza kuja kukaa naye kwa muda mrefu.”
Mbali na kuweza kucheza kama mshambuliaji wa kati lakini Fofana anaweza kutumika kama kiungo mshambuliaji na kuonyesha ubora mkubwa, hivyo Simba inaonekana itakuwa na makali zaidi kwenye eneo la ushambuliaji ambapo itakuwa pia ikimtumia Oura, Libasse Gueye ambaye amekuwa na makali tangu ametua kwenye timu hiyo pamoja na kiungo Inno Loemba.