Msuva alitoa zawadi bao lake kwa Iran, awatoa hofu Watanzania

WINGA wa Tanzania, Simon Msuva anayekipiga Al Talaba ameendelea kuonyesha kiwango bora katika Ligi Kuu ya Iraq baada ya kufunga bao muhimu na kisha kulitoa zawadi kwa taifa la Iran huku akiomba hali ya amani irejee katika eneo hilo.

Msuva alifunga bao hilo katika ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Al Qassim kwenye mechi ya ligi iliyopigwa katika mazingira yaliyoelezwa kuwa na presha kutokana na hali ya usalama inayoendelea kuripotiwa kwenye ukanda huo.

Bao  hilo liliwashangaza mabeki wa Al Qassim kutokana na alivyopiga mpira wa kichwa uliotokana na krosi na kumshinda kipa aliyebaki akiutazama ukijaa nyavuni.

Akizungumza na Mwanaspoti, Msuva alisema ameamua kulitoa bao hilo kwa wananchi wa Iran huku akiomba hali itulie haraka kwa sababu ikiendelea hivyo inaweza kuathiri hata mwenendo wa ligi.

“Nimelitoa goli hili kwa Iran, tunaomba mambo yawe sawa haraka kwa sababu hali ikiendelea hivi inaweza kuleta changamoto kubwa hata kwa ligi kuendelea.”

Aliongeza katika kipindi hiki cha machafuko amekuwa akipokea simu nyingi kutoka kwa watu mbalimbali wakitaka kujua hali yake ya usalama, akisisitiza kwa sasa yuko salama na anaendelea na majukumu yake ya soka.

“Watu wengi wamekuwa wakinipigia simu kuniuliza hali yangu ya usalama, lakini namshukuru Mungu niko vizuri na naendelea na kazi yangu,” alisema Msuva.

Ushindi huo umeifanya Talaba isogee hadi nafasi ya tatu kwenye msimamo wa ligi ikiwa na pointi 40 katika mechi 21 ilizocheza.

Bao hilo linakuwa la tatu kwa Msuva msimu huu ishara kuwa winga huyo bado anaendelea kuwa na mchango mkubwa ndani ya kikosi hicho licha ya ushindani mkubwa uliopo katika ligi hiyo.