Wabunge Chato, madiwani wanne wafikishwa kortini tuhuma za rushwa

Chato. Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Mkoa wa Geita imewafikisha mahakamani wabunge wawili wa Chato, Pascal Lutandula (Chato Kusini), Cornel Magembe wa (Chato Kaskazini) na madiwani wanne akiwemo aliyekuwa Mwenyekiti wa Halmashauri ya Chato, Bathoromeo Manunga wakituhumiwa kwa rushwa wakati wa mchakato wa kumpata mwenyekiti wa halmashauri hiyo.

Mbali nao, wengine ni madiwani Frank Francis wa Mganza, Njile Mboligo wa Muungano na Josephat Manyenye wa Bwera ambao wote kwa pamoja ni wanachama wa Chama cha Mapinduzi (CCM) ambao wamepandishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Geita leo Jumatatu, Machi 9, 2026.

Akizungumza na waandishi wa habari, Mkuu wa Takukuru Mkoa wa Geita, James Ruge amesema kesi hizo zimesajiliwa kwa namba CC Na 5100/2026 pamoja na CC Na. 5099/2026.

Amesema Novemba 28 na 30, walipokea taarifa za uwepo wa vitendo vilivyoshukiwa ni vya rushwa vilivyofanywa na Magembe kwa kushirikiana na Francis.

Ruge amesema uchunguzi ulithibitisha viongozi hao waliwakusanya madiwani wateule 20 wa Halmashauri ya Wilaya ya Chato katika Hoteli ya Lakezone iliyopo jijini Mwanza na baadaye Serengeti Palace Hotel iliyopo mji mdogo wa Katoro mkoani Geita kwa lengo la kuwashawishi kwa hongo ya fedha, chakula na malazi kwa madiwani hao.

Amesema lengo ni kupiga kura za upendeleo kwa mgombea waliyemtaka katika nafasi ya mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Chato.

Ruge amesema inadaiwa Lutandula kwa kushirikiana na Manunga na Manyenye walihusika na vitendo vya rushwa katika kuwania nafasi ya Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Chato.

Katika tukio hilo, amedai wanatuhumiwa walijenga ushawishi kwa kumpa rushwa Mboligo ili kujiondoa katika kinyang’anyiro cha uchaguzi wa nafasi ya Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya Chato.

Kufuatia matukio hayo, Takukuru ilianzisha uchunguzi na kubaini uwepo wa vitendo vya rushwa katika mchakato wa uchaguzi huo ndani ya CCM.

Amesema walilazimika kuchukua hatua za kisheria dhidi ya waliobainika kwa mujibu wa sheria ya Takukuru sura ya 329 marejeo ya mwaka 2023, iliyofanyiwa marekesbisho na sheria Na 11 ya mwaka 2024.

Machi 6, 2026, Halmashauri ya CCM Mkoa wa Geita ilitangaza kumfukuza uanachama Manunga akituhumiwa kwa makosa mbalimbali ya utovu wa nidhamu ikiwemo vitendo vya rushwa wakati wa mchakato wa kushinda wadhifa huo.

Hata hivyo, Manunga ambaye amekuwa diwani kwa miaka 15, aliahidi kuanza mchakato wa kukata rufaa kwa kuwa katiba ya chama inampa nafasi ya rufaa ndani ya siku 90.