Siku moja baada ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kuufungia Uwanja wa Sokoine kwa kukosa sifa ya kuchezewa mechi za mashindano yaliyo chini ya shirikisho hilo, Tanzania Prisons imehamishia mechi yake dhidi ya Yanga mkoani Tabora kwenye Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi.
Sokoine umefungiwa jana Machi 8, 2026 ikiwa ni muda mfupi baada ya mechi ya Kombe la Shirikisho la CRDB baina ya Mbeya City dhidi ya Bandari Tanzania iliyomalizika kwa wenyeji kushinda 3-0 na kufuzu 16 bora.
Ikumbukwe uwanja huo unaomilikiwa na Chama Cha Mapinduzi (CCM) unatumika kwa timu za Mbeya City na Tanzania Prisons zinazoshiriki Ligi Kuu na hazijawa na matokeo mazuri msimu huu.
Wakati uwanja huo ukifungiwa, Tanzania Prisons ilikuwa ikijiandaa kuikaribisha Yanga kwenye mwendelezo wa Ligi Kuu, mechi itakayochezwa Machi 12, 2026, huku Mbeya City ikijinoa kuipokea Singida Black Stars, Machi 15, 2026.
Akizungumza na Mwanaspoti leo Machi 9, 2026, Mtendaji Mkuu wa Tanzania Prisons, Ajabu Kifukwe, amewaomba radhi mashabiki na wadau wa soka jijini Mbeya kwa kuhamisha mechi hiyo akieleza kuwa ni jambo lililo nje ya uwezo wao.
Amesema uongozi unaomba radhi pia kwa matokeo yasiyoridhisha akieleza kuwa kwa sasa wachezaji wana ari na nguvu mpya tangu walipomaliza mechi dhidi ya Azam FC iliyoisha kwa suluhu ya bila kufungana akieleza kuwa matarajio yao ni kufanya vizuri.
“Mchezo wetu dhidi ya Yanga utachezwa Tabora katika Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi, tumejipanga kushinda baada ya kutokuwa na mwanzo mzuri, ari ya wachezaji iko juu na tunaomba radhi kwa mabadiliko haya yaliyonje ya uwezo wetu.
“Kuhusu hamasa nje ya uwanja, hii ni timu ya taasisi na imekuwa na utaratibu wake pale inaposhinda Mkuu wa Jeshi la Magereza huwa anatoa ofa, hii ni mwendelezo, tunaenda kwa kujiamini kutafuta pointi tatu,” amesema Kifukwe.
Ameongeza kuwa, benchi la ufundi chini ya kocha Shadrack Nsajigwa limekuwa na program nzuri na wachezaji wakijiandaa na mechi hiyo akiahidi kuwa Tanzania Prisons inahitaji ushindi ili kujiweka pazuri katika msimamo wa Ligi Kuu.
Tanzania Prisons imecheza mechi 15 za Ligi Kuu Bara msimu huu na kuvuna pointi 13 ikishika nafasi ya 15, huku Yanga ikiongoza msimamo kwa pointi 32 ikishuka dimbani mara 12.
Hata hivyo, wakati timu hizo zikienda kukutana, Yanga imeonekana kuwa na rekodi bora dhidi ya Maafande hao, kwani mara ya mwisho Tanzania Prisons kushinda mbele ya bingwa huyo mtetezi ilikuwa Mei 10, 2018 ilipoilaza mabao 2-0.