Dar es Salaam. Katika kuadhimisha Siku ya Wanawake Duniani 2026 yenye kauli mbiu ya “Give to Gain”, Diamond Trust Bank Tanzania (DTB) imetoa zawadi maalum kwa wafanyakazi wake wanawake kama ishara ya kutambua mchango wao muhimu katika mafanikio ya taasisi hiyo ya kifedha.
Hatua hiyo inalenga kuhamasisha usawa wa kijinsia na kuendelea kujenga mazingira jumuishi ya kazi yanayowathamini na kuwawezesha wanawake.
Diamond Trust Bank Tanzania imeeleza kuwa inaamini uwekezaji kwa wanawake katika nafasi za kazi na uongozi ni muhimu kwa maendeleo ya taasisi na jamii kwa ujumla.
Makabidhiano ya zawadi hizo yaliongozwa na Ofisa Mtendaji Mkuu wa benki hiyo, Ravneet Chowdhury, kwa kushirikiana na viongozi wengine waandamizi wa benki katika hafla maalum iliyofanyika ndani ya taasisi hiyo ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya siku hiyo muhimu duniani.
Akizungumza katika hafla hiyo Machi 8, 2026, Chowdhury amewapongeza wanawake wa DTB kwa bidii, weledi na mchango wao mkubwa katika kuimarisha huduma za benki pamoja na kusaidia ukuaji wa taasisi hiyo.
“Benki yetu itaendelea kujenga mazingira shirikishi yanayowapa wanawake nafasi sawa ya kukua kitaaluma, kushika nafasi za uongozi na kutoa mchango chanya ndani ya taasisi na katika jamii,” amesema.
Aidha, alisisitiza kuwa uwezeshaji wa wanawake katika sekta ya fedha ni hatua muhimu katika kuchochea maendeleo ya uchumi.
Alibainisha kuwa taasisi za kifedha zina wajibu wa kuunga mkono juhudi za kuongeza ushiriki wa wanawake katika maamuzi ya kiuchumi, huku akihimiza wanawake kuendelea kutumia fursa zilizopo kujijengea uwezo na kuchangia maendeleo ya taifa.