Serikali kuendeleza mageuzi ya kidemokrasia, wasomi watahadharisha

Dar es Salaam. Wachambuzi wa siasa na diplomasia wameeleza kwamba, dhamira ya Serikali kuendeleza mageuzi ya kidemokrasia inaweza kuwa na mchango katika kuimarisha umoja wa kitaifa ikiwa itazingatia misingi ya uwazi, ushirikishwaji na kuheshimu utawala wa sheria.

Wachambuzi wameeleza hayo leo Machi 9, 2026 baada ya Tanzania kuthibitisha dhamira yake ya kuendeleza mageuzi ya kidemokrasia na kuzingatia maadili ya Jumuiya ya Madola wakati iliposhiriki katika Mkutano wa 72 wa Kikosi Kazi cha Mawaziri wa Nchi Wanachama.

Mkutano huo wa Jumuiya ya Madola (CMAG) ulifanyika London, Uingereza Machi 7, 2026, chini ya uenyekiti wa Dk Ian Borg, Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Mambo ya Nje na Utalii wa Malta.

Ujumbe wa Tanzania uliongozwa na Profesa Palamagamba Kabudi, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Kazi Maalum), ambaye aliwafahamisha nchi wanachama kuhusu hatua zilizochukuliwa na Serikali kufuatia matukio ya Oktoba 29, 2025 pamoja na mageuzi yanayoendelea kutekelezwa.

Katika mkutano huo, Tanzania iliwasilisha maendeleo yaliyopatikana chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan, yakiongozwa na mfumo wa kitaifa wa Kurekebisha, Kujenga Upya na Kurejesha unaolenga kuimarisha taasisi za kidemokrasia, kukuza maridhiano ya kitaifa na kuimarisha imani ya wananchi katika mfumo wa utawala.

Kwa mujibu wa taarifa ya Wizara ya mambo ya Nje, Profesa Kabudi aliufahamisha mkutano kuhusu kazi inayofanywa na Tume Huru ya Uchunguzi inayoongozwa na Jaji Mkuu mstaafu Chande Othman, pamoja na maandalizi yanayoendelea ya kuanzisha Tume ya Kitaifa ya Maridhiano, itakayosaidia kuendeleza mazungumzo ya kitaifa na kuimarisha mshikamano.

Akizungumzia hatua hiyo ya Serikali, mhadhiri wa Chuo cha Diplomasia cha Dk Salim Ahmed Salim, Innocent Shoo amesema mageuzi hayo yanaweza kuwa na mchango mkubwa katika kuimarisha umoja wa kitaifa ikiwa yatazingatia misingi ya uwazi, ushirikishwaji wa wananchi na kuheshimu utawala wa sheria.

Amesema mageuzi ya kidemokrasia yanaweza kuongeza imani ya wananchi kwa taasisi za dola. Pia, amesema pale uchaguzi unapokuwa huru na haki, na vyombo vya dola vinatenda kwa uwajibikaji, wananchi kutoka makundi mbalimbali ya kijamii na kisiasa hujiona kuwa sehemu ya mfumo wa kitaifa.

“Mageuzi yanaweza kuimarisha ushiriki wa wananchi katika uamuzi ya kisiasa. Demokrasia inapowapa wananchi nafasi ya kutoa maoni yao kupitia vyama vya siasa, asasi za kiraia na vyombo vya habari huru, hujenga utamaduni wa majadiliano badala ya migongano,” amesema.

Hata hivyo, amesema mageuzi ya kidemokrasia pekee hayatoshi kuimarisha umoja wa kitaifa. Umoja wa kweli unahitaji pia maendeleo ya kiuchumi yenye usawa, haki za kijamii na kupunguza tofauti za kipato na fursa kati ya makundi mbalimbali ya wananchi.

“Kwa hiyo, ingawa mageuzi ya kidemokrasia ni hatua muhimu katika kujenga Taifa lenye umoja na utulivu, yanapaswa kuambatana na sera za maendeleo jumuishi na uimarishaji wa taasisi za kitaifa ili kufikia umoja wa kudumu,” amesema.

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom), Dk Paul Loisulie amesema mageuzi hayo yakifanyika kwa dhamira njema, yatasaidia kuondoa mizozo ya kila msimu wa uchaguzi, jambo ambalo husababisha athari kwa Taifa.

“Kama Serikali itatekeleza mageuzi hayo kwa dhamira njema ya kutaka kujenga demokrasia, litakuwa ni jambo jema, lakini sharti mageuzi hayo yalete usawa kwenye ulingo wa kisiasa ili kumaliza malalamiko yaliyopo,” amesema Dk Loisulie.