Kihongosi awapigania wafanyabiashara Bariadi | Mwananchi

Bariadi. Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Kenani Kihongosi ametaka wafanyabiashara walioondolewa katika eneo ambalo ujenzi wa soko kuu la Wilaya ya Bariadi unaendelea kupewa kipaumbele ujenzi utakapokamilika.

Pia, ametoa maagizo mawili kwa mkandarasi anayejenga soko hilo, akitaka ujenzi ukamilike ndani ya muda wa mkataba, Februari 3, 2027 na pia kuongeza kasi ya ujenzi huo wa soko hilo.

Hadi sasa ujenzi umefikia asilimia 25, ukihusisha pia barabara za lami zenye urefu wa kilomita 8.6 na ofisi vitakavyogharimu zaidi ya Sh26.5bilioni.

Kihongosi ambaye leo Jumatatu, Machi 9, 2026 anahitimisha ziara yake mkoani Simiyu, akikagua miradi ya maendeleo ambayo Serikali imepeleka fedha, kusikiliza changamoto za wananchi na kufuatilia uhai wa chama, alianzia wilayani Maswa Machi 7, kisha Itilima na leo anahitimisha katika wilaya ya Bariadi.

Mafundi wakiendelea na kazi kwenye ujenzi wa Soko kuu la Wilaya ya Bariadi.



Akiwa Bariadi, Kihongosi ametembelea shina namba tano la Mahaha, sanjari na kukagua mradi wa shamba la pamba na ujenzi wa soko kuu la wilaya linalojengwa eneo Sima, wilayani humo.

Katika mradi wa soko ambao ukikamilika utakuwa na maduka 251, vizimba 592, vizimba vya samaki 64 na maeneo mengine ikiwamo maegesho ya magari na maeneo maalumu ya mama lishe na baba lishe, Kihongosi amesisitiza wafanyabiashara waliokuwa wakifanya biashara awali katika eneo hilo kupewa kipaumbele.

Wenyeji wanaeleza kabla ya ujenzi huo wa kisasa, soko hilo lilikuwa la kawaida, dogo na halikuwa na huduma nyingi muhimu, kabla ya Serikali kuwahamishia wafanyabiashara kwenye soko walilolitaja kama soko la jioni ili kupisha ujenzi wa kisasa.

Akizungumzia ugawaji wa maduka na vizimba, Kihongosi amesisitiza uwe wa haki na wale waliokuwa wakifanya biashara awali katika eneo hilo kupewa kipaumbele

“Katika hili, ugawaji wa vibanda uwe wa haki wale (wafanyabiashara) waliokuwepo mwanzo wapewe kipaumbele, maduka yakibaki ndiyo wapewe wapya.

Eneo la mradi wa ujenzi wa Soko kuu la Wilaya ya Bariadi.



“Isitokee kiongozi mmoja ana maduka matatu, wanaostahili wapewe kwa utaratibu mzuri,” amesema Kihongosi akiagiza viongozi wa wilaya kulisimamia hilo na kusisitiza Serikali inasimamia haki na CCM imejengwa kwa misingi inayojali na kusimamia utu,” amesema Kihongosi huku akishangiliwa na wananchi.

Kihongosi pia amemuagiza mkandarasi kuhakikisha ujenzi huo unakamilika katika muda uliopo kwenye mkataba wa Februari 3, 2027.

Akielezea maendeleo ya ujenzi wa soko hilo, Hessein Katakweba aliyezungumza kwa niaba ya mkurugenzi wa Bariadi, Iddi Ndabhona hadi sasa ujenzi umefikia asilimia 25 akidai changamoto ya hali ya hewa ya mvua imesababisha kazi kusimama.

Katakweba amesema soko hilo litakapokamilika litakuwa na maduka ya kisasa, vizimba na mabucha ya kisasa na eneo la kukusanyia taka ngumu sanjari na miundombinu mingine rafiki kwa makundi yote na wananchi wa Bariadi wataweza kufanya shughuli za kiuchumi mchana na usiku.

Wakielezea fursa ambazo wanazitarajia ujenzi wa soko hilo ukikamilika, baadhi ya wananchi wamesema mbali na kuboresha wilaya yao, usalama wa mali zao utakuwa wa uhakika.

“Soko la awali lilikuwa dogo, si salama na mazingira yake hayakuwa rafiki, ili jipya linakwenda kwanza kuiboresha wilaya yetu, pia kutuhakikishia usalama wa biashara sisi wananchi,” amesema Martha Mabula.

Mwananchi mwingine, Priscar Aseno amesema ujenzi wa soko hilo ni fursa kwao ya kiuchumi akiishukuru Serikali kwa maendeleo ambayo inawaletea.