Mjumbe Maalum wa UN Aipongeza Tanzania kwa Juhudi za Kurejesha Amani na Kuimarisha Taasisi za Kidemokrasia

Mwakilishi Maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa katika Umoja wa Afrika na Mkuu wa Ofisi ya Umoja wa Mataifa katika Umoja wa Afrika (UNOAU), Bw. Parfait Onanga-Anyanga amewasili nchini kwa ziara akiwa kama Mjumbe Maalum wa Mhe. Antonio Guterres, Katibu Mkuu UN kwenye ziara ya kikazi lengo likiwa ni kukutana na kufanya mazungumzo na Mamlaka pamoja na wadau mbalimbali kuhusu matukio yaliyotokea kabla na baada ya Uchaguzi Mkuu wa Tanzania, 2025 na kuangalia hali ya maisha ya Tanzania kwa sasa.

Bw. Onanga-Anyanga ametoa pongezi hizo alipofanya mazungumzo na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Mahmoud Thabit Kombo (Mb.), jijini Dar es Salaam, ikiwa ni hatua ya mwanzo ya mazungumzo yake na Serikali pamoja na wadau mbalimbali wa kitaifa.

Mjumbe huyo yupo nchini kwa ziara ya kikazi kwa lengo la kufanya mashauriano na Serikali na wadau wengine wa kitaifa kuhusu hali ya kisiasa nchini, pamoja na kujadili namna Umoja wa Mataifa unavyoweza kuunga mkono juhudi za Serikali katika kuimarisha taasisi za kidemokrasia, kusimamia mageuzi na kuendeleza umoja na mshikamano wa kitaifa kupitia maridhiano jumuishi.

Aidha, amempongeza Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuonesha utulivu na uongozi makini katika kipindi hicho kigumu kwa taifa. Amekaribisha pia uamuzi wa Serikali wa kuunda Tume ya Kuchunguza Matukio Wakati na Baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025

Bw. Onanga-Anyanga aliipongeza Tume hiyo inayoongozwa na Mhe. Mohamed Chande Othman, Jaji Mkuu Mstaafu kwa kazi yake nzuri yenye kubeba uzito na ubobezi na viwango vya hali ya juu na ya kuigwa kimataifa. Ameeleza pia kuwa muundo wa Tume hiyo unaojumuisha wajumbe kutoka kada mbalimbali umeongeza ubora na uhuru wa kazi yake.

Aidha, ameipongeza Serikali kwa juhudi zake za kurejesha imani ya wananchi na kudumisha utulivu baada ya matukio hayo, pamoja na hekima na utulivu uliotumika katika kushughulikia changamoto zilizojitokeza wakati wa kipindi cha uchaguzi.

Katika muktadha huo, Mwakilishi huyo Maalum alikaribisha mpango mpana wa kitaifa uliotangazwa na mamlaka mwezi Januari 2026 chini ya kaulimbiu ya “Repair – Rebuild – Renew,” akibainisha kuwa mpango huo unaweka msingi muhimu wa kuimarisha utawala wa kidemokrasia, kusimamia mageuzi ya taasisi pamoja na kuendeleza maridhiano ya kitaifa.

Vilevile, amempongeza Mhe. Mahmoud Kombo, kwa juhudi zake za kuielezea jumuiya ya kimataifa hatua na michakato ya ndani ya nchi inayochukuliwa kushughulikia matukio hayo na kuimarisha mshikamano wa kitaifa.

Katika ratiba ya ziara yake nchini, Bw. Onanga-Anyanga anatarajiwa kukutana na viongozi wa vyama vya siasa ikiwemo Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), ACT Wazalendo, Chama cha Ukombozi wa Umma (CHAUMA) na Chama Cha Mapinduzi (CCM) ili kubadilishana mawazo kuhusu masuala ya utawala bora, demokrasia na mshikamano wa kitaifa.

Aidha, atafanya mazungumzo na Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jaji Mkuu pamoja na Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambani ni wawakilishi wa mihimili yote mitatu ya dola.

Kwa upande wake, Mhe. Balozi Mahmoud Thabit Kombo (Mb.) ameishukuru Umoja wa Mataifa kwa ushirikiano wake na kueleza kuwa Tanzania inathamini sana ushirikiano huo. Ameeleza kuwa Serikali itaendelea kushirikiana na UN na haitasita kuomba msaada wake pale inapohitajika katika kuimarisha taasisi za taifa na kulinda amani, utulivu na mshikamano wa wananchi.