Profesa Mahalu afariki dunia, aacha historia

Dar es Salaam. Profesa wa sheria na mwanadiplomasia nguli, Profesa Costa Mahalu (77) amefariki dunia.

Taarifa kutoka kwa familia yake imethibitisha Profesa Mahalu amefariki dunia leo katika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) alikokuwa akipatiwa matibabu.

Hadi anafariki dunia, Profesa Mahalu alikuwa Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu St Augustine akiendelea kutoa elimu ya sheria.

Profesa Mahalu alifungua ukurasa mpya wa maisha yake ya umma mwaka 1996 aliposhawishiwa na Rais Benjamin Mkapa kuingia kwenye masuala ya kidiplomasia.

Aliteuliwa kuwa ofisa balozi katika ubalozi wa Tanzania nchini Ujerumani, nafasi ambayo alihudumu kwa miaka mitatu na baadaye aliteuliwa kuwa Balozi wa Tanzania nchini Italia, ambapo pia alihudumu kama mwakilishi wa nchi kwenye Shirika la Chakula na Kilimo (FAO), Mpango wa Chakula Duniani (WFP), na Mfuko wa Kimataifa wa Maendeleo ya Kilimo (IFAD).

Kwa kuzingatia utendaji wake wa juu kama balozi, Jamhuri ya Italia ilimpa Profesa Mahalu heshima ya Tuzo ya “Order of Star of Italian Solidarity” kwa jitihada zake za kuimarisha uhusiano wa kidiplomasia na Tanzania.

Profesa Mahalu alikuwa Mwafrika wa sita kupata tuzo hiyo, ikionyesha umahiri wake na mchango wake mkubwa katika uwakilishi wa Tanzania kimataifa.

Profesa Mahalu aliwahi kunukuliwa akisema kwamba Jaji Joseph Warioba ndiye aliyemvutia kusomea sheria jambo lililobadilisha maisha yake kutoka ndoto ya utotoni ya kuwa mwigizaji wa filamu maarufu, hadi kuwa profesa mashuhuri wa sheria na balozi wa kimataifa.

Alinukuliwa akisema shauku yake ya kuingia kwenye fani ya sheria ilianza wakati akiwa mwanafunzi wa sekondari Kibaha, ambapo kaka yake, Profesa William Mahalu (marehemu), alikuwa rafiki wa karibu wa Warioba na alimuomba amsimamie kwenye masomo ya sheria.

Kwenye mahojiano hayo Profesa Mahalu alikumbuka namna alivyokuwa akitumia likizo zake kushiriki na familia ya Warioba, ambapo alipata mwongozo wa kidiplomasia na kitaalamu kuhusu taaluma ya sheria.

Mjumbe wa Bunge la Katiba

Pia, Profesa Mahalu wakati wa mchakato wa mabadiliko ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mwaka 2014 alichaguliwa kuwa mjumbe wa Bunge la Katiba akiwakilisha Baraza la Maaskofu wa Kanisa Katoliki Tanzania (TEC).

Katika Bunge hilo, aliteuliwa kuwa Mwenyekiti wa kamati ya kupanga masharti, kanuni na taratibu zilizotumika katika kuandaa rasimu ya katiba hiyo.

Alifanya kazi pamoja na viongozi wakiwemo Naibu Mwenyekiti, sasa Rais, Samia Suluhu Hassan, na Mwenyekiti wa Bunge, aliyekuwa Spika, Samuel Sitta (marehemu).

Profesa Mahalu na mke wake Vulfrida Grace Mahalu, wamebarikiwa kupata watoto wawili, Costa Ricky Emanuel na Deogratius Isack, ambao wote ni mawakili, kama vile mke wake.

Moja ya tukio la kukumbukwa kwa Profesa Mahalu ni pale Rais wa awamu ya pili hayati Benjamin Mkapa alipokwenda mahakamani kutoa ushahidi katika kesi iliyomkabili Profesa Mahalu na mwenzake, Grace Martin, kuhusu madai ya wizi wa zaidi ya Euro 2 milioni (Sh5.69 bilioni) katika ununuzi wa jengo la ubalozi wa Tanzania nchini Italia.

Kesi hiyo iliyokuwa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Mkapa alikuwa shahidi wa Profesa Mahalu na aliieleza mahakama kuwa alikuwa na taarifa za mikataba miwili ya ununuzi wa jengo hilo na kama Rais alibariki ununuzi huo.

Alisisitiza kuwa mchakato mzima ulizingatia sera za Serikali na masilahi ya Taifa, ukiwemo uthamini wa jengo uliofanywa na Wizara ya Ujenzi na Wizara ya Ardhi na Maendeleo Mijini.

Mkapa pia alithibitisha kuwa Profesa Mahalu ni mtu wa tabia njema, mwaminifu na mchapaji kazi, na alitambuliwa na Rais wa Italia kwa tuzo ya heshima kwa mchango wake katika diplomasia. Wakili wa Profesa Mahalu alikuwa Mabere Marando.

Profesa Mahalu alizaliwa Julai 9, 1948, katika Kijiji cha Katunguru, Sengerema, mkoani Mwanza.