Watanzania 236 waliokwama Dubai warejea nchini, wasimulia waliyopitia

Dar es Salaam. “Nilikuwa naomba Mungu kila siku nimwone tena mwanangu akiwa hai. Leo nimemkumbatia tena hapa uwanja wa ndege, siwezi kueleza furaha niliyonayo.”

Hayo ni maneno ya mama aliyejitambulisha kwa jina moja la Sharifa, ambaye ameshindwa kuyazuia machozi ya furaha yaliyomtoka alipompokea mwanaye katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) jijini Dar es Salaam.

Sharifa ni miongoni mwa ndugu na jamaa waliokusanyika uwanjani hapo kusubiri ndege maalumu iliyowarejesha Watanzania 236 waliokuwa wamekwama katika miji ya Dubai na Abu Dhabi huko Falme za Kiarabu (UAE), kufuatia hali tete ya kiusalama inayoripotiwa katika baadhi ya maeneo ya Mashariki ya Kati.

Ndege hiyo iliyotumwa na Serikali ya Tanzania, imewasili mchana wa leo Machi 9, 2026 ikiwa na raia hao waliokuwa wakifanya kazi, biashara au safari binafsi, wanafunzi na wanamichezo katika mataifa ya Ghuba kabla ya hali ya usalama kuzorota.

Mwananchi imeshuhudia ndugu, jamaa na marafiki waliokuwa wakisubiri wapendwa wao wakionyesha hisia kali za furaha, shukrani na nafuu baada ya siku kadhaa za wasiwasi kufuatia mashambulizi huko mashariki ya kati.

“Nilikuwa napigiwa simu kila siku na ndugu yangu akisema kuna hofu, watu wanaishi kwa tahadhari kubwa. Tulikuwa tunaomba tu warudi salama,” amesema ndugu mmoja aliyefika kumpokea kaka yake aliyekuwa huko kibiashara na baadaye kushindwa kusafiri kurudi Tanzania.

Mmoja wa wasafiri hao waliowasili nchini, John Bina ameliambia Mwananchi kuwa hali katika Taifa hilo ni ya hatari akibainisha kuwa mashambulizi yalikuwa yakiendelea maeneo mbalimbali huku watu wakilazimika kujifungia ndani.

Ameeleza jinsi mawasiliano ya mtandao yalivyokuwa msaada kwao wakati wote akisema ndiyo yaliwezesha kupata taarifa kwa Watanzania kuhusu utaratibu wa kufanikisha kurejeshwa kwao nyumbani.

“Katika Taifa hilo, jambo pekee nililoona ni namna wanavyosimamia huduma ya mawasiliano. Pamoja na vita vyote, mtandao upo vizuri wakati wote na ndio uliokuwa unatusaidia kupata taarifa. Kwa kweli namshukuru Mungu na Serikali ya Tanzania kwa msaada huu,” amesema.

Mtanzania mwingine aliyerejea, Princess Mwakatobe ameema hali hiyo iliwaathiri hasa raia wa kigeni waliokuwa hawana uhakika wa usalama wao.

“Tulikuwa tunaishi kwa tahadhari sana, namna ya kula, kutembea hata kufanya chochote ilikuwa vigumu, yaani hata usafiri ulikuwa shida ukifika uwanja wa ndege umegeuka kama uwanja wa mpira tu, hakuna kinachoendelea,” amesema.

Amesema changamoto kubwa ilikuwa ni hofu ya kutokujua kinachoendelea siku inayofuata huku kila taifa likipambana kunusuru raia wake.

“Hali ilikuwa mbaya sana Dubai na Abu Dhabi, kumefanyika mashambulizi mengi sana, hali ni mbaya hata kutembea huwezi kutamani. Wengi wetu tulisubiri msaada wa Serikali na tunashukuru sana Serikali ya Tanzania kwa msaada iliotupatia tumerudi salama,” amesema.

Watanzania hao wamesema walipopokea taarifa ya mpango wa kurejeshwa nyumbani kwa msaada wa Serikali ya Tanzania walifurahi kwani wengi walikuwa wameanza kuwa na hofu ya kuendelea kukaa huko bila uhakika wa maisha yao.

Akizungumzia hatua zilizofanywa na Serikali kuwarejesha, Meneja wa Operesheni wa Shirika la Ndege la Air Tanzania (ATCL), Kapteni Arif Jinnah amesema operesheni ya kuwarejesha raia hao ilifanyika kwa ushirikiano kati ya serikali, balozi na mamlaka za anga za Tanzania na Dubai.

Amesema baada ya kupata taarifa kuhusu uwepo wa Watanzania waliokuwa katika mazingira ya hatari au wasiwasi wa kiusalama, Serikali ilichukua hatua za haraka kupanga usafiri maalumu wa kuwarudisha nyumbani.

“Naishukuru sana Serikali, kwa kweli imeonyesha dhamira yake ya kulinda raia wake popote walipo. Tuliratibu safari maalumu ya ndege kuwachukua Watanzania hawa na kuhakikisha wanarejea nyumbani salama,” amesema.

Amesema waliorejeshwa ni Watanzania waliokuwa huko wakifanya shughuli zao au waliokwenda mara moja na kukumbana na hali iliyotishia usalama wao.

“Haikuwa ndege ya kibiashara, ilitolewa kwa maagizo maalumu ya Rais Samia na ilikuwa na gharama nafuu kuhakikisha tunawaokoa Watanzania wote,” amesema.

Ameongeza kuwa ndege hiyo iliondoka na akiba ya kutosha ya mafuta ili kukabiliana na dharura yoyote ambayo ingeweza kutokea kutokana na vita vinavyoendelea huko.

“Tumetumia siku nyingi katika operesheni hii kutokana na tahadhari ya vyombo vyetu na abiria wetu,” ameongeza.