Majonzi mwili wa Naomi ukipatikana katika mazingira tata

Iringa. Majonzi mazito yametanda katika familia moja mjini Iringa baada ya kupatikana kwa mwili wa Naomi Kivamba (13) aliyekuwa akisoma darasa la saba Shule ya Msingi Njiapanda aliripotiwa kupotea ghafla nyumbani kwao kabla ya kupatikana akiwa amefariki dunia.

Ndani ya nyumba ya familia hiyo kulikuwa na hali ya huzuni iliyochanganyika na mshangao, huku watu wakikusanyika kwa makundi wakijaribu kufarijiana na wakati huohuo wakisimulia kumbukumbu zao kuhusu mtoto huyo.

Kilio cha mama Naomi kilisikika zaidi ya sauti nyingine zote, kikitawala mazingira ya maombolezo na kugusa hisia za waliokuwepo.

Akiwa ameketi chini huku akiwa na maumivu makali ya kumpoteza mtoto wake, alisikika akimuita kwa sauti ya uchungu kana kwamba bado anaweza kumjibu.

“Mwanangu, kweli .. kweli mwanangu… nimefika bibi yako nimefika… njoo mwanangu njoo tupike, njoo tupike koleza moto mwanangu, koleza moto mwanangu njoo mwanangu tupike,” alilia kwa uchungu huku akionekana kushindwa kuamini kwamba sauti yake haitajibiwa tena na mjukuu wake.

Kwa mujibu wa maelezo ya familia, Mjomba wa Naomi, Benjamin Kikula anasema kuwa tukio hilo lilitokea Machi 7, 2026 mchana baada ya mtoto huyo kutumwa dukani kununua kiberiti na kutokurudi tena mpaka kufikwa na tukio hilo.

“Naomi alitumwa kununua kiberiti na kaka yake na baada ya hapo hakuonekana tena,” anasema Kikula.

Kikula anaeleza kuwa Machi 7, 2026 majira ya saa tisa walipogundua kuwa Naomi haonekani nyumbani hawakupata hofu lakini kadri muda ulivyozidi kupita bila yeye kurejea ndipo hali ya wasiwasi ilianza kuongezeka.

Akizungumza leo Machi 8, 2026 mmoja wa majirani, Jacob Mwalongo amesimulia kuwa walipogundua mtoto huyo haonekani walianza kumtafuta katika maeneo ya karibu na ilipofika jioni na giza kuanza kuingia huku Naomi akiwa bado hajapatikana, familia iliamua kwenda kutoa taarifa katika kituo cha polisi ili kupata msaada zaidi wa kumtafuta.

“Tulipofika kituoni tulipokewa na askari ambao walitusikiliza na kutupatia ushirikiano katika juhudi za kumtafuta mtoto wetu, “ anasema Mwalongo.

Mwalongo anaendelea kusimulia kuwa baada ya kutoa taarifa hiyo, wanafamilia hawakuacha juhudi za kumtafuta na baadhi yao waliendelea kuzunguka katika maeneo ya jirani hadi usiku huku wakitumaini wangempata mtoto huyo akiwa hai na salama.

Imeelezwa kuwa, usiku huo ulipita katika hali ya wasiwasi  huku wengi wakikesha wakijadili wapi wangeweza kuendelea kumtafuta asubuhi inayofuata.

Mwalongo anasema asubuhi ilipofika, jitihada za kumtafuta Naomi ziliendelea tena kwa nguvu zaidi huku majirani na watu wengine wakijiunga na familia katika kupekua maeneo ya karibu na kuuliza kwa wakazi wa mitaa jirani kama kuna mtu aliyemuona mtoto huyo tangu aliporipotiwa kupotea.

Mwalongo anasema katika harakati hizo ndipo jirani yao anayejulikana kama Kalinga alipotoa taarifa ambayo iliwafanya waliokuwa wakimtafuta kushtuka na kuelekea haraka katika eneo alilolitaja ili kujua kilichokuwa kimetokea.

“Alituambia mtoto amepatikana na yupo hapa amedondoka,” amesimulia Mwalongo.

Wakiwa na matumaini kwamba mtoto huyo angekuwa ameanguka au kujeruhiwa na bado angeweza kusaidiwa, wanafamilia pamoja na majirani walikimbilia haraka katika eneo alilotaja jirani huyo na walipofika, baadhi yao walianza kuangalia kwa karibu ili kuona hali ya mtoto huyo lakini waligundua mara moja kuwa hali haikuwa kama walivyotarajia.

“Baada ya kufika tuligundua mtoto siyo kwamba amedondoka tu bali tayari ni maiti na hapo ndipo tulipoona tufunike mwili wake kwanza kisha tukaripoti tena polisi kwa mara ya pili ili wachukue hatua zaidi,” amesema Mwalongo.

Baada ya taarifa hiyo kutolewa kwa mara ya pili, imeelezwa kuwa askari wa polisi walifika katika eneo la tukio na kuanza kufanya uchunguzi wa awali.

Kwa mujibu wa maelezo ya wanafamilia, polisi walipoangalia mwili wa mtoto huyo waliona dalili za majeraha  na baadaye mwili wa mtoto huyo ulipelekwa hospitali na kufanyiwa uchunguzi wa kitabibu ili kubaini chanzo cha kifo chake.

Baada ya uchunguzi huo kufanyika, familia inaeleza kuwa madaktari walibaini kuwa mtoto huyo alikuwa amefanyiwa ukatili mkubwa kabla ya kifo chake, jambo lililowaacha ndugu na jamaa wakiwa katika majonzi makubwa na mshangao.

Jirani na ndugu wa familia hiyo, Adela Isack anasema alipokea taarifa ya kupotea kwa Naomi wakati akiwa hajisikii vizuri kiafya, hali iliyomfanya awaombe ndugu wengine kusaidia katika juhudi za kumtafuta mtoto huyo kwa sababu yeye mwenyewe hakuwa katika hali nzuri ya kuweza kushiriki kikamilifu katika harakati hizo.

“Asubuhi nilipigiwa simu nikaambiwa mtoto amepatikana yupo nyumba ya pili jirani na nilipotoka nikafika pale nikakuta tayari mtoto ameshafunikwa shuka,” anasema Adela

Adela anasema walishirikiana na askari polisi waliofika katika eneo hilo walionesha ushirikiano katika hatua za awali za uchunguzi kwa kuwasikiliza wanafamilia na kuanza kukusanya taarifa muhimu kuhusu tukio hilo.

Adela anasema walipoangalia mwili wa mtoto huyo waliona baadhi ya majeraha makubwa ikiwamo mkono uliokuwa kama umevunjika pamoja na shingo iliyokuwa imelegea, hali iliyowaacha wakiwa katika huzuni kubwa na kuamini kuwa mtoto huyo alipata mateso makubwa kabla ya kupoteza maisha.

Adela anaongeza kuwa waliona pia alama za vidonda katika sehemu ya paja pamoja na upande mmoja wa nguo zake kuwa umechanika chanika, jambo lililowaacha wakiwa na maswali mengi kuhusu mazingira halisi yaliyosababisha tukio hilo.

Mwenyekiti wa Mtaa wa Njiapanda Kata ya Isakalilo, Maisha Modester anasema alipokea taarifa za tukio hilo akiwa safarini lakini aliwaruhusu wajumbe wa mtaa kuendelea kushirikiana na wananchi pamoja na polisi jamii katika kusaidia hatua za awali za uchunguzi ili kuhakikisha ukweli wa tukio hilo unajulikana.

Modester anasema baadaye alipata taarifa kwamba mtoto huyo alikuwa amepatikana lakini tayari alikuwa amefanyiwa ukatili mkubwa uliosababisha kifo chake, jambo ambalo limewaacha wakazi wengi wa eneo hilo wakiwa katika huzuni na hofu.

Akithibitisha tukio hilo, Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya mkoa wa Iringa, Dk Alfred Mwakalebela ameiambia Mwananchi Digital kuwa ni kweli walipokea mwili wa Naomi na baada ya jana Machi 8, 2026 waliweza kufanya uchunguzi katika mwili wake na ndipo walipogundua kuwa alifanyiwa ukatili wa kijinsia.

“Tulifanya uchunguzi kwenye mwili wa mtoto huyo na tulikuta walimnyonga shingo na uti wa mgongo wa shingo wamemkata kabisa na alikuwa na alama ya kucha shingoni,” amesema Dk. Mwakalebela.

Jeshi la Polisi mkoani Iringa, limesema kuwa linaendelea na upelelezi wa tukio

“Upelelezi unaendelea ili kuweza kuwapata wahusika wa tukio hili ikiwa ni pamoja na kuchukuliwa hatua kali za kisheria,” inaeleza taarifa ya Kamanda wa Polisi, Mkoa wa Iringa, Allan Bukumbi.