Moshi. Serikali imezifungia zaidi ya kadi 12,000 za huduma za bima ya afya na kusitisha huduma katika vituo zaidi ya 33 vya kutolea huduma za afya, baada ya kubainika kuwapo kwa udanganyifu katika matumizi ya bima hizo.
Udanganyifu huo unahusisha wagonjwa kujiandikisha kwa kutumia kadi zao za bima, lakini huduma kama vipimo vya CT Scan kufanywa na watu wengine tofauti na walioandikishwa, hali inayosababisha upotevu wa fedha za Serikali.
Akizungumza leo Jumatatu Machi 9, 2026 katika maadhimisho ya miaka 55 ya huduma za afya katika Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Kaskazini, KCMC, Naibu Waziri wa Afya, Florence Samizi amesema hatua hiyo imechukuliwa ili kudhibiti ubadhirifu na kuhakikisha huduma za bima zinawanufaisha walengwa halali.
“Kumekuwa na udanganyifu hasa kwenye huduma za bima za afya. Mgonjwa anayejiandikisha si yule anayekwenda kufanya CT Scan, jambo linalosababisha upotevu wa fedha za Serikali,” amesema Dk Samizi.
Amesema mbali na kufungia kadi hizo, Serikali pia imechukua hatua kwa vituo vya afya vilivyobainika kushiriki au kuruhusu udanganyifu huo kwa kusitisha huduma zao katika mfumo wa bima ya afya.
“Tuna kadi zaidi ya 12,000 ambazo tumezifungia huduma kwa ajili ya udanganyifu wa aina hiyo, na pia tuna vituo zaidi ya 33 ambavyo tumesitisha huduma zake kutokana na kubainika kushiriki katika udanganyifu huo,” amesema.
Kwa mujibu wa Dk Samizi, Serikali inaendelea kuimarisha mifumo ya kidijitali katika utoaji wa huduma za afya ili kuhakikisha taarifa za mgonjwa zinafuatiliwa kwa usahihi tangu anapoingia hospitalini hadi anapopata huduma zote anazohitaji.
Amesema mifumo hiyo itasaidia kuhakikisha kuwa mgonjwa anayesajiliwa mapokezi ndiye anayepokea huduma katika vitengo vingine kama maabara na radiolojia.
“Mifumo lazima isomane. Lazima tujue aliyeandikishwa mapokezi ndiye aliyefika maabara. Huwezi kufanikisha hilo bila kuimarisha mifumo,” amesema.
Ameongeza kuwa hatua hiyo si tu itazuia upotevu wa fedha za Serikali, bali pia itasaidia kuboresha ubora wa huduma za afya kwa kuhakikisha taarifa sahihi za mgonjwa zinapatikana na kutumika ipasavyo katika matibabu.
Katika hatua nyingine, Dk Samizi ameipongeza Hospitali ya KCMC kwa kuanzisha kitengo kipya cha huduma za magonjwa ya moyo, akisema Serikali itaendelea kushirikiana na taasisi hiyo katika kuboresha huduma za kibingwa na bobezi nchini.
Amesema Serikali itaendelea kutoa fedha kwa ajili ya ununuzi wa vifaa tiba vya kisasa na kusaidia utekelezaji wa miradi ya kimkakati katika sekta ya afya.
“Serikali itaendelea kusaidia kwa karibu hospitali ya KCMC katika kuhakikisha miradi ya kimkakati ya sekta ya afya inatekelezwa na kukamilika kwa wakati,” amesema.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa KCMC, Gileard Masenga amesema ujenzi wa jengo jipya la huduma za magonjwa ya moyo unatarajiwa kugharimu zaidi ya Sh25 bilioni.
Amesema kitengo hicho kitakuwa na uwezo wa kulaza wagonjwa 102 kwa wakati mmoja, wakiwemo watoto 50 na watu wazima 52, na kitasaidia kupanua upatikanaji wa huduma za kibingwa kwa wagonjwa wanaohitaji matibabu ya moyo.
“Kitengo hiki kitasaidia kupunguza rufaa za wagonjwa kwenda hospitali nyingine na kuwapa wananchi huduma za kibingwa karibu zaidi,” amesema Profesa Masenga.
Naye Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Alex Malasusa ameishauri Serikali kuendelea kutenga fedha kwa ajili ya kukamilisha miradi ya afya, ikiwemo ununuzi wa vifaa tiba vya kisasa kwa ajili ya kitengo hicho cha magonjwa ya moyo.
Amesema uwekezaji katika miundombinu na vifaatiba utasaidia kupanua upatikanaji wa huduma bora za afya na kuwasaidia wagonjwa wengi zaidi kupata matibabu nchini.