Dar es Salaam. Mjadala umeibuka miongoni mwa wadau wa sekta ya uchukuzi na wafanyabiashara kufuatia kutangazwa kwa ada mpya za mizigo ya ndani katika bandari nchini, huku baadhi wakidai zinaongeza gharama za biashara. Hata hivyo, Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) imesema hatua hiyo inalenga kuboresha miundombinu na kuongeza ufanisi wa huduma za bandari.
Pia kupunguza gharama nyingine za uendeshaji kwa watumiaji wa bandari kwa muda mrefu. Kwa mujibu wa taarifa ya TPA kitabu kipya cha ada za bandari (ambacho kimebeba mabadiliko ya gharama) kimeanza kutumia Machi 08, 2025 baada ya kilichokuwepo kudumu kwa miaka 13 (Tangu Machi, 2013.
Baada ya taarifa hiyo kuliibuka mjadala miongoni mwa wafanyabiashara na wasafirishaji wakidai kuwa ada hizo ni kubwa, utekelezaji wake umeharakishwa huku wengine wakisema kuwa ushirikishaji haukuwa mkubwa lakini TPA imeweka wazi utaratibu uliotumika, madhumuni na ushirikishwaji ulivyokuwa.
Kwa mujibu wa (TPA) ongezeko la gharama hizo linalenga kufadhili uboreshaji wa miundombinu ya bandari kwa kiwango cha juu zaidi lakini pia kutunisha mfuko wa ulinzi wa mazingira ya bandari. Pamoja na ongezeko hilo Mkurugenzi Mkuu wa mamlaka hiyo Plasduce Mbossa anasema ufanisi utapunguza gharama nyingine.
“Ada hizi ni shirikishi, tulikutana na wadau wote kupitia vikao mbalimbali tukawaelezea juu ya kitabu kipya cha ada wakatupa maoni yao, tukapeleka kwa mdhibiti (Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania Tasac), naye akaitisha wadau akapata maoni yao ndiyo tukaja na kitabu hiki lengo kubwa ni kuongeza ufanisi wa bandari,” anasema Mbossa akijibu wanaosema ada zimetangaza Machi 09, 2025 na kuanza siku hiyohiyo.
Mbossa anasema kupitia mabadiliko hayo ya ada TPA itaweza kujenga magati mapya 18 ndani ya kipindi cha miezi 24 akisema baada ya kukamilika kwa mradi huo na mingine ya kuboresha shughuli za bandari hiyo watumiaji watapata nafuu kubwa.
“Baada ya ujenzi wa magati haya tutakuwa na eneo la kutosha la kuhifadhi mizigo, gharama za kuchelewa kuchukua mizigo (storage) zitaondoka hivyo watumiaji wa bandari watapata nafuu kwa namna nyingine huku huduma za bandari zikiboreshwa,” anasema Mbossa na kusisitiza kuwa mara mwisho ada zimehuishwa zaidi ya muongo mmoja uliopita.
Aidha Mbossa anasema hatua hiyo haitakuwa na athari yoyote kwa biashara ya bandari hiyo akisema viwango hivyo viliwekwa kwa kuzingatia vinavyotozwa katika bandari nyingine za nchi jirani.
Kuhusu ada hizo, Mkurugenzi wa kampuni ya Dar Planet Logistics Limited, Philibert Msacky anasema zinaongeza gharama za biashara na kuumiza walaji wa mwisho kwani hivi sasa gharama za bandari zinakuwa karibu au zaidi ya gharama ya mzigo mzima.
‘Wameanzisha ada mpya ya uboreshaji wa miundombinu ambayo ni asilimia 0.09 ya CIF (Gharama za mzigo, bima na usafiri) na ada ya mradi wa utunzaji wa mazingira ambayo itatozwa kulingana na aina na ukubwa wa mzigo,” anasema Msacky.
Msacky ambaye alikuwa na mizigo anayopaswa kuiondosha bandarini jana, anasema upande wa ada ya mpango wa mazingira kontena moja la futi 20 linalipiwa Dola 50 (128,970) huku la futi 40 likilipiwa Dola 100 (Sh255,900), mizigo ya kawaida Dola 0.25 kwa tani moja na gari itatoza Dola moja kwa mita moja ya ujazo.
Mathalani Msacky amesema kuna kontena alitakiwa kulipia Sh925,848 lakini sasa anatakiwa kulipa Sh3.8 milioni na kwingineko mtandao baadhi ya watu walilalamika kuwa kuna magari walitakiwa kulipia ada ya Sh230,000 lakini sasa imepanda hadi Sh1.2 milioni, na nyingine kutoka Sh500,000 hadi Sh3.4 milioni.
Hata hivyo Mwenyekiti wa Chama cha Mawakala wa Meli Tanzania (Tasaa), Daniel Malongo, anaeleza mambo muhimu yanayopaswa kuzingatiwa kuhusu marekebisho hayo kubwa likiwa ni madhumuni yake ambayo ni kuongeza kasi ya huduma ili meli zinazoingia zisilazimike kusubiri kwa muda mrefu.
“Kitabu hiki cha ada si jambo jipya; kimekuwa kikiandaliwa kwa zaidi ya miezi sita. Mamlaka zimekuwa zikitoa taarifa na maelezo kuhusu sababu za kufanya mabadiliko haya, hasa kuboresha miundombinu ya bandari, kuongeza magati mapya, kuendeleza mfumo wa kidijitali wa uendeshaji wa bandari,” anasema Malongo.
Kadhalika anasema kitabu hicho kilikuwa hakijafanyiwa marekebisho kwa zaidi ya miaka 10, hivyo marekebisho haya yalikuwa yamechelewa kwa muda mrefu lakini pia ada hizo mpya zitafanya gharama za bandari za Tanzania kuwiana na zile za nchi jirani.