Simba, Yanga zarudishwa tena Zanzibar, kukichafua Aprili 21

ZIKIWA zimepita siku chache baada ya Yanga na Simba kutoka kucheza mechi ya Ligi Kuu Bara iliyomalizika bila kufungana kwenye Uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar, timu hizo zimetajwa kati ya nane zinazotarajiwa kushiriki michuano ya Kombe la Muungano 2026.

Kwa kutajwa huko, timu hizo zinatarajiwa kurejea tena Zanzibar kusaka heshima baada ya kushindwa kutambiana Machi Mosi 2026. Kabla ya hapo, ilishuhudiwa Yanga ikiweka heshima kwa kubeba Kombe la Mapinduzi 2026.

Simba na Yanga ni miongoni mwa timu nne za Tanzania Bara zitakazoshiriki Kombe la Muungano 2026 kuanzia Aprili 21, 2026 hadi Aprili 26, 2206. Zingine ni Singida Black Stars na Azam.

Kumbuka timu zote hizo zilishiriki Kombe la Mapinduzi 2026 na Yanga kubeba ubingwa ikiifunga Azam katika fainali iliyochezwa Januari 13, 2026 kwenye Uwanja wa Gombani, Pemba. Simba na Singida Black Stars ziliishia nusu fainali, zote zikifungwa 1-0 na wapinzani wao.

Kwa upande wa Zanzibar, katika michuano hiyo itawakilishwa na Mlandege FC, Muembe Makumbi City, Mafunzo na KVZ.

Yanga ni bingwa mtetezi wa Kombe la Muungano baada ya kulibeba mwaka jana 2025 kwa kuifunga JKU bao 1-0 katika fainali iliyochezwa Mei Mosi, 2025 kwenye Uwanja wa Gombani kisiwani Pemba.

Kwa kutwaa ubingwa huo, iliifanya Yanga kuwa kinara baada ya kulibeba mara saba ikifanya hivyo mwaka 1983, 1987, 1991, 1996, 1997, 2000 na 2025.

Licha ya tarehe na timu shiriki kufahamika mapema, lakini hadi sasa haijafahamika michuano hiyo itachezwa kisiwani gani kati ya Pemba au Unguja.

Kwa mujibu wa Katibu Mkuu wa Shirikisho la Soka Zanzibar (ZFF),  Hussein Ahmada Vuai, tarehe ya kufanyika michuano hiyo inafahamika sambamba na timu shiriki, lakini kwa upande wa sehemu ya kufanyia itatangazwa itakapokuwa tayari.

“Hadi kufikia sasa maandalizi yanakwenda vizuri na kamati ya kombe hilo itakutana na wajumbe wa pande zote mbili kwa ajili ya kufanya uamuzi wa eneo la kufanyika,” amesema.

Vuai amesema taarifa ya mapema ni kujuza umma kuwa michuano hiyo msimu huu ipo na itafanyika mwezi Aprili 2026 kama ilivyopangwa lakini muda si mrefu itatolewa taarifa kamili.

Michuano hiyo ilianzishwa mwaka 1982 ikiwa maalumu kwa ajili ya kusherekea Muungano wa Tanganyika na Zanzibar uliopatikana Aprili 26, 1964 na kuzaliwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.