TPA yasimamisha ada mpya za uendelezaji hadi Julai 1

Dar es Salaam. Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) imetangaza kusitisha matumizi ya ada ya uendelezaji wa miundombinu ya bandari (PID) iliyoanza utekelezaji Machi 8, 2026 na itaaanza tena kutumika Julai Mosi, 2026.

Kusitishwa kwa utozaji ada hiyo kumetokana na maombi kutoka kwa wadau mbalimbali wa bandari walioomba kupatiwa muda zaidi kabla ya kuanza kutumika kwa ada hiyo ambayo ipo kwenye kitabu cha Ada za Bandari Mwambao wa Bahari cha mwaka 2026. 

Ada hizo mpya zilianza kutumika Machi 8, 2026 na kuibua mijadala mbalimbali kutoka kwa wadau wa bandari. 

Katikati ya mijadala hiyo, usiku wa janaJumatatu, Machi 9, 2026, Mkurugenzi Mkuu wa TPA, Plasduce Mbossa ametoa taarifa kwa umma juu ya kusitishwa kwa ada za tozo hizo.

Mbossa amesema baada ya kupokea na kuchambua kwa kina maombi hayo, TPA imeridhia kutoa muda zaidi kabla ya kuendelea kutumika kwa Ada ya PID.
.
“Nyongeza ya muda imetolewa ili kuwawezesha wateja wote, wadau, kampuni za usafirishaji wa meli, mawakala wa forodha na usafirishaji, wasafirishaji wa mizigo, waagizaji, wauzaji nje na ndani ya nchi pamoja na umma kwa ujumla kujiandaa vema zaidi,” amesema.

Amesema kupitia muda uliotolewa utawawezesha watoa huduma kila mmoja kukamilisha masharti ya mikataba aliyonayo baina yake na wateja wake wa ndani na nje ya nchi ndani ya kipindi cha muda uliobaki hadi kufikia Juni 30, 2026.

Pia, muda huo utamuwezeaha kila mmoja  kurekebisha masharti ya mikataba yake ya kibiashara baina yake na wateja wake wa ndani au nje ya nchi ambayo yataendelea kuwa hai baada ya Julai Mosi 2026, ili kuendana na matakwa ya ada ya PID.

Hii ni mara ya pili TPA inasogeza mbele kuanza kwa ada ya PID kwani hapo awali, awali ilikuwa imepangwa kuanza Februari 8, 2026. 

“Kutokana na maombi yaliyopokelewa kipindi hicho, TPA ilisogeza muda wa kuanza kwake hadi Machi 8, 2026 kwa sababu sawa na hizo zilizoanishwa juu,” amesema.

Kufuatia hilo, TPA imewaomba wateja wote ambao wamepata ankara zao Machi 8 na 9 au wameshafanya malipo ya ada hizo kwa tarehe husika kufika katika Ofisi za TPA – Kitengo cha ankara za bandari cha bandari aliyopo kwa ajili ya kupewa utaratibu wa kurejeshewa kiasi kilicholipwa.

“Kwa mteja yoyote ambaye ana ankara ambazo bado hazijalipwa, anaombwa kufika katika Ofisi ya TPA Kitengo cha ankara za bandari cha bandari aliyopo kwa ajili ya kufanyiwa marekebisho ya ankara yake kabla ya kulipia,” amesema.