Dar es Salaam. Usemi elimu ni ufunguo wa maisha, umeibua mjadala wa makundi mawili yanayopingana. Lipo linalosema kuna matajiri wa shahada za elimu, lakini masikini wa maisha, huku lingine likisema wapo mafukara wa elimu wanaishi maisha bora.
Upinzani huo umekwenda mbali zaidi na kuibua, mjadala mwingine kati ya wanaosema elimu si nyenzo ya kuyafungua maisha, huku wengine wakisema elimu bado ni mhimili wa maendeleo ya mtu na Taifa.
Hoja ya wanaopinga umuhimu wa elimu katika kuyafikia maisha bora, wanaijenga katika msingi kuwa, ujasiri, bidii, maarifa ya vitendo na ubunifu vinaweza kumfungulia mtu maisha zaidi kuliko vyeti vya darasani.
Mjadala huo umechochewa na simulizi na video zinazowaonesha wafanyabiashara, wasanii au watu waliopata mafanikio katika maisha bila kusoma hadi ngazi za juu, hali iliyowafanya baadhi ya wananchi kuhoji thamani ya elimu rasmi katika dunia ya sasa.
Mitazamo tofauti mtandaoni
“Nawajua watu ambao hawakumaliza hata shule ya sekondari lakini wanaendesha biashara kubwa, wanaajiri watu na wanaheshimika,” amesema mmoja wa wachangiaji wa mjadala huo katika mtandao wa kijamii.
Wanaosimamia hilo wanasema elimu imekuwa kama bidhaa isiyotoa uhakika wa mafanikio, hasa katika mazingira yenye ajira chache.
Akitoa maoni yake katika hilo hivi karibuni, Augustine Willey ameandika, “kwenye nchi ambayo haithamini raia wake hususani masikini, haithamini wakiwamo walimu, madaktari, wahandisi na wengineo na zaidi haiupi thamani wala haina mpango madhubuti na wa lazima wa kukuza vipaji vya ugunduzi katika nyanja zote na hasa za kisayansi.
“Inathamini uchawa, wenye madaraka na fedha. Waliofanikiwa na wanaokula meza moja na hao wa juu wanaoishikilia nchi bila swala lolote la elimu ndio watazidi kuonekana wamefanikiwa kwenye maisha.”
Naye brandingdanny ameandika, “elimu ni muhimu ila ni elimu ipi sasa? Ya hapa bongo? Magazijuto, history ya chief mkwawa? Hebu angalia watu wanahitimu uhandisi ujenzi ila ukienda site za barabara unawakuta Wachina, kwanini tunaleta Wachina kufanya miradi ya uhandisi? Hii ina maana kwamba elimu yetu bado hamna kitu.
“Msingi wa elimu ya Kitanzania ni kuondoa ujinga tu sio kutengeneza watu wa kufanya bunifu na gunduzi.Watu wanafundishwa kukumbuka shuleni, mitihani inapima kumbukumbu tu haipimi ubunifu.” Kupitia ukurasa wake wa Instagram, Dau Kasomba ameandika, “wasio na elimu ndio huiona elimu sio muhimu kwasababu ukomo wao wa kufikiria unaishia kwenye ujinga ulio kwenye akili zao.”
Kwa upande wake Hassan Seleman amesema kinachosababisha mjadala huo ni kuwepo kwa wanaoidharaulisha elimu kwa kile alichokiita hawataki kuitumia elimu waliyoipata ikaleta tija kwenye jamii.
“Elimu iwe na athariii kwenye jamiii!! Aliwahiii kusema Chinua Achebe, haijalishi kile unachokifahamu bali yule unayeenda kumfahamu. Hata kama umesomea ualimu haitakuwa na maana kama kile ulichosoma kitakosa athari kwa unayeenda kumfundisha, yaani lazima tupambane na kuhakikisha wale unaoenda kuwafundisha wanafanikisha malengo yao.”
Joseph Kidanka ameandika, “elimu ni msingi wa ubunifu, kama wanaojiita wasomi na hakuna walichobuni, nadhani kuna haja ya kujitafakari na kubadilisha mfumo wa elimu uendane na mahitaji na changamoto za wakati.”
Diof ameandika, “Tatizo ni mfumo wa hiyo elimu, wasomi hawathaminiwi, wanafanywa machawa.”
Wengine wanasema mfumo wa elimu unafundisha nadharia nyingi zisizoendana na uhalisia wa maisha, hali inayowafanya wahitimu wengi kushindwa kujiajiri au kukabiliana na changamoto za kiuchumi.
Hata hivyo, wasomi na wadau wa elimu wamejitokeza kupinga hoja hizo wakisisitiza kuwa, elimu haiwezi kupimwa kwa kipato pekee.
Deodita Msonsa ambaye ni mwalimu wa sekondari Ilala amesema elimu hujenga uwezo wa kufikiri, kufanya uamuzi sahihi, kubuni suluhisho na kuhimili mabadiliko ya dunia.
“Ni kweli kuna watu wachache waliofanikiwa bila elimu rasmi, lakini hawawezi kuwa kigezo cha jumla,” amesema Msonsa.
Ameongeza kuwa elimu hutoa msingi mpana wa maarifa unaomwezesha mtu kubadilika kadri mazingira yanavyobadilika, tofauti na ujuzi wa bahati au fursa za muda mfupi.
Wasomi pia wanasema elimu ina mchango mkubwa katika ustawi wa jamii kwa jumla kuanzia afya bora, uongozi unaowajibika, hadi ukuaji wa uchumi.
“Mtu mwenye elimu ana uwezekano mkubwa wa kuelewa haki zake, wajibu wake na kushiriki kikamilifu katika maendeleo ya Taifa,” amesema mwalimu Msonsa.
Wachambuzi wa masuala ya kijamii, wamesema mjadala huo unaakisi changamoto pana zaidi ya mfumo wa elimu na soko la ajira.
Wanasema badala ya kuipuuza elimu, mjadala unapaswa kuelekezwa katika kuiboresha ili iendane na mahitaji ya sasa ya kiuchumi na kijamii.
“Tatizo si elimu, bali ni namna tunavyoitumia na kuiunganisha na ujuzi wa vitendo,” amesema mtaalamu wa sera za elimu, Dk Stella Mbawala.
Dk Mbawala amesema elimu ikichanganywa na ubunifu, teknolojia na ujasiriamali, bado ni nyenzo muhimu ya kumuinua mtu binafsi na Taifa.
Mhadhiri wa Elimu, Shule Kuu ya Elimu Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Profesa George Kahangwa amesema mjadala huo ni matokeo ya kuishi kwenye jamii watu wasio na uadilifu ndiyo wenye mafanikio.
“Halafu unategemea mtoto aelewe anachofundishwa darasani kuhusu maadili. Jamii ina vitu ambavyo vinakinzana na kile ambacho tulikusudia kukijenga, sasa kama tunataka elimu ijenge uzalendo, maadili na uwajibikaji tuna kila sababu ya kuviondoa vitu hivyo.
“Hilo litawezekana endapo tutaonesha kwa uwazi namna watu wenye maadili na uzalendo wanavyofanikiwa ili mtoto ajifunze; na sio kuonesha watu wanavyoweza kufanikiwa kwa ujanja ujanja. Tunaona siku hizi machawa wana maisha mazuri kuliko wasomi unategemea mtoto atajifunza nini kama sio kufanya vitendo hivyo ili na yeye afanikiwe,” amesema.
Mtafiti Dk John Mwakipesile, amesema changamoto kubwa si elimu yenyewe, bali namna inavyotolewa.
“Elimu yetu inapaswa kuendana na mahitaji ya soko la ajira na mazingira halisi ya maisha. Tunahitaji kuimarisha elimu ya ufundi, ubunifu na ujasiriamali kuanzia ngazi za chini,” amesema.
Dk Mwakipesile amesema mitalaa inapaswa kuzingatia zaidi stadi za vitendo, teknolojia na uwezo wa kujiajiri, ili wahitimu wasitegemee ajira za ofisini pekee.
Mchambuzi wa sera za elimu, Amina Mshana amependekeza kuwepo kwa ushirikiano wa karibu kati ya vyuo, Serikali na sekta binafsi.
“Waajiri washirikishwe katika kuandaa mitalaa. Hii itasaidia kuhakikisha kile kinachofundishwa darasani kinaendana na uhalisia wa soko la ajira,” amesema.
Amesisitiza kuwa, kuna umuhimu kwa vyuo kuweka utaratibu wa mafunzo kwa vitendo (internship) yaliyo na ufuatiliaji madhubuti ili wanafunzi wapate uzoefu kabla ya kuhitimu.
Kubadili mtazamo wa jamii
Mhadhiri wa saikolojia ya jamii, Dk Fatuma Nnko amesema elimu haipaswi kupimwa kwa kipato pekee.
“Elimu ni zaidi ya mshahara. Inajenga uwezo wa kufikiri kwa kina, kuchambua taarifa, kufanya uamuzi sahihi na kuwa raia anayewajibika.
“Nashauri ziwepo kampeni za kitaifa zinazolenga kuonesha mafanikio ya watu waliotumia elimu yao kubuni miradi, kuanzisha biashara au kutoa mchango mkubwa katika jamii,” amesema.
Eneo lingine lililoshauriwa ni kuimarishwa kwa taasisi za elimu ya ufundi na mafunzo ya kati, ili kuwapa vijana ujuzi unaohitajika kwa haraka katika soko la ajira.
“Elimu si lazima iwe ya chuo kikuu pekee. Elimu ya ufundi ikiwa bora na yenye hadhi sawa, inaweza kubadilisha maisha ya vijana wengi,” amesema Mshana.