Wataalamu wa fedha SADC wajadili  kuongeza bajeti

Dar es Salaam. Wataalamu wa masuala ya fedha kutoka nchi wanachama wa Jumuiya Maendeleo ya Kusini mwa nchi za Afrika  (SADC) wamekutana jijini Pretoria nchini Afrika Kusini kujadili hali ya kifedha ya jumuiya hiyo pamoja na mikakati ya kuongeza vyanzo vya mapato ili kuimarisha utekelezaji wa miradi ya maendeleo ya kikanda.

Taarifa iliyotolewa na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki imesema kikao hicho kimefanyika leo Machi 9, 2026, na kuwakutanisha   wataalamu wa fedha na bajeti kutoka nchi mbalimbali wanachama.

Ujumbe wa Tanzania katika kikao hicho umeongozwa na Kamishna wa Fedha za Nje kutoka Wizara ya Fedha,  Rishade Bade.

Katika mkutano huo, wajumbe wamejadili masuala kadhaa muhimu ikiwemo hali ya michango ya nchi wanachama wa SADC, pamoja na mapitio ya utekelezaji wa bajeti ya jumuiya hiyo kwa mwaka wa fedha 2025/2026 kwa kipindi cha miezi tisa kuanzia Aprili hadi Desemba 2025.

Aidha, wataalamu hao wamepitia mapendekezo ya bajeti ya Sadc kwa mwaka wa fedha 2026/2027 na kufanya tathmini ya makadirio ya mapato na matumizi ya jumuiya hiyo kwa kipindi cha muda wa kati kuanzia mwaka wa fedha 2027/2028 hadi 2030/2031.

Mbali na hilo, ajenda nyingine muhimu inayojadiliwa ni namna ya kuimarisha uhamasishaji wa rasilimali fedha (resource mobilization) kwa lengo la kugharamia miradi ya maendeleo ya kikanda.
 Majadiliano hayo pia yamehusisha utekelezaji wa uanzishwaji wa Mfuko wa Maendeleo wa Kanda (Regional Development Fund – RDF) unaolenga kusaidia kugharamia miradi mikubwa ya maendeleo katika nchi wanachama.

Hadi sasa, nchi 11 kati ya 16 wanachama wa SADC, ikiwemo Tanzania, zimesaini mkataba wa kuanzishwa kwa mfuko huo ambao unatarajiwa kuwa chanzo muhimu cha fedha kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya kimkakati katika ukanda wa kusini mwa Afrika.

Wajumbe wa SADC wakiwa katika kikao jijini Pretoria nchini Afrika Kusini walipokutana kujadili hali ya kifedha ya jumuiya hiyo pamoja na mikakati ya kuongeza vyanzo vya mapato ili kuimarisha utekelezaji wa miradi ya maendeleo ya kikanda.



Kikao cha Kamati ya Fedha ni sehemu ya maandalizi ya mkutano mkubwa wa Baraza la Mawaziri la SADC, ambao unatarajiwa kufanyika Machi 12 na 13, 2026, ambapo mawaziri watajadili na kutoa maamuzi ya mwisho kuhusu masuala mbalimbali ya maendeleo na ushirikiano wa kikanda.