Fainali ya mashindano ya soka nchini Brazil imeingia kwenye historia kwa sababu zisizofurahisha baada ya kuzuka kwa vurugu kubwa uwanjani zilizofanya wachezaji 23 kupewa kadi nyekundu idadi kubwa zaidi kuwahi kutokea katika historia ya soka la nchi hiyo.
Tukio hilo lilitokea katika fainali ya Mashindano ya Mineiro iliyochezwa kati ya Cruzeiro na Atlético Mineiro katika jiji la Belo Horizonte.
Vurugu zilianza muda mfupi baada ya kipa wa Atlético Mineiro, Everson, kugongana na kiungo wa Cruzeiro Christian.
Inaelezwa kuwa kipa huyo alimrukia mpinzani wake aliyekuwa chini baada ya kuumia na kuanza kumfokea karibu na sikio. Tukio hilo liliwakasirisha wachezaji wa Cruzeiro ambao walikimbia haraka kumkabili Everson, huku baadhi yao wakimsukuma hadi kwenye nguzo ya goli.

Dakika chache baadaye, uwanja mzima uligeuka uwanja wa mapigano baada ya wachezaji wengi wakiwemo waliokuwa benchi pamoja na baadhi ya maafisa wa timu kuingia uwanjani. Makonde na mateke vilianza kurushwa huku wachezaji wakipigana.
Miongoni mwa waliokuwa katikati ya vurugu hizo alikuwa nyota wa Brazil Hulk, ambaye alionekana akipigwa teke la kuruka na mmoja wa wachezaji wa Cruzeiro.
Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 39 pia alionekana akimpiga mchezaji mwingine ngumi nyuma ya kichwa wakati vurugu zikiendelea.
Baada ya hali kutulia, mwamuzi alipuliza filimbi ya mwisho ya mechi.
Cruzeiro iliibuka mshindi kwa bao 1–0, shukrani kwa bao lililofungwa dakika ya 60 na Kaio Jorge.
Baada ya mechi, maafisa wa mashindano walifanya uchunguzi na hatimaye wachezaji 23 walipewa kadi nyekundu kwa pamoja, idadi iliyovunja rekodi ya awali ya wachezaji 22 waliowahi kutolewa katika mechi kati ya Portuguesa na Botafogo mwaka 1954.

Hulk aomba radhi Baada ya tukio hilo, Hulk aliomba radhi kwa kuhusika kwake kwenye vurugu hizo.
“Inasikitisha sana. Sijawahi kuona vurugu kama hizi katika mechi yoyote ya soka,” alisema.
“Hatuwezi kuweka mfano mbaya kama huu kwa sababu una athari duniani kote. Tuna jukumu la kulinda taswira yetu na taswira ya klabu.”