Mjumbe Maalumu wa UN awasili Tanzania kujadili hali ya kisiasa, matukio ya Oktoba 29

Dar es Salaam. Mwakilishi Maalumu wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa katika Umoja wa Afrika, Parfait Onanga-Anyanga, amewasili nchini kwa ziara ya kikazi inayolenga kufanya mashauriano na Serikali pamoja na wadau mbalimbali kuhusu hali ya kisiasa nchini kufuatia matukio ya Oktoba 29, 2025.

Onanga-Anyanga, ambaye pia ni mjumbe maalumu wa Katibu Mkuu wa UN, António Guterres, tayari amekutana na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mahmoud Thabit Kombo, jijini Dar es Salaam ikiwa ni mwanzo wa mazungumzo yake na Serikali.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Onanga-Anyanga ameipongeza Serikali ya Tanzania kwa hatua ilizochukua kurejesha amani na utulivu kufuatia vurugu na matukio ya uvunjifu wa amani yaliyoripotiwa katika baadhi ya maeneo ya nchi Oktoba 29 mwaka jana.

Mwakilishi Maalumu wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa katika Umoja wa Afrika, Parfait Onanga-Anyanga akisalimiana na Waziri wa Mambo ya Nje wa Tanzania, Mahmoud Kombo.



Katika ratiba ya ziara yake, mjumbe huyo wa UN anatarajiwa kukutana na viongozi wa vyama mbalimbali vya siasa, ikiwamo Chama Cha Mapinduzi (CCM), Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), ACT Wazalendo na Chama cha Ukombozi wa Umma (Chaumma), kwa lengo la kubadilishana mawazo kuhusu utawala bora, demokrasia na kuimarisha mshikamano wa kitaifa.

Aidha, Anyanga ambaye pia ni Mkuu wa Ofisi ya Umoja wa Mataifa katika Umoja wa Afrika (UNOAU), anatarajia kufanya mazungumzo na viongozi wa mihimili mikuu ya dola, wakiwamo Spika wa Bunge, Jaji Mkuu pamoja na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, ziara ya Onanga-Anyanga inalenga kujadili namna UN inavyoweza kuendelea kuunga mkono juhudi za Serikali katika kuimarisha taasisi za kidemokrasia, kusimamia mageuzi na kukuza umoja na mshikamano wa kitaifa kupitia maridhiano jumuishi.

Katika mazungumzo hayo, mwakilishi huyo maalumu aliukaribisha mpango mpana wa kitaifa uliotangazwa na mamlaka Januari 2026 wenye kaulimbiu ya  “Repair, Rebuild,  Renew,” akisema unatoa msingi muhimu wa kuimarisha utawala wa kidemokrasia, kuendeleza mageuzi ya taasisi na kukuza maridhiano ya kitaifa.

Kwa upande wake, Waziri Kombo ameishukuru UN kwa ushirikiano wake na kusisitiza kuwa Tanzania inathamini mchango huo katika masuala ya maendeleo na amani.


Amesema Serikali itaendelea kushirikiana na UN na haitasita kuomba msaada wake pale inapohitajika, hasa katika juhudi za kuimarisha taasisi za Taifa pamoja na kulinda amani, utulivu na mshikamano wa wananchi.

Aidha, Onanga-Anyanga alimpongeza Waziri Kombo kwa juhudi zake za kuielezea jumuiya ya kimataifa hatua zinazochukuliwa na Serikali kushughulikia matukio ya Oktoba 29 na kuimarisha mshikamano wa kitaifa.