Yanga, Simba zapishana na mamilioni CAF

Hatua ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika na Kombe la Shirikisho Afrika msimu huu wa 2025/2026 inaanza wiki hii bila uwepo wa klabu za Tanzania kwa vile klabu za Yanga, Simba, Azam na Singida Black Stars zimeishia katika hatua ya makundi.

Timu hizo nne za Tanzania hasa Simba na Yanga ni kama zimepishana na ‘gari la mshahara’ kwani siku nne kabla ya kuanza, Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) limetangaza ongezeko kubwa la fedha za zawadi kwa timu zitakazotwaa mataji hayo.

Taarifa iliyotolewa na CAF jana, Jumatatu, Machi 9, 2026 imefafanua kuwa bingwa wa Ligi ya Mabingwa Afrika kuanzia msimu huu atapata kiasi cha Dola 6 milioni (Sh15.5 bilioni).

Ni ongezeko la asilimia 60 kutoka kiasi ambacho bingwa alipata katika msimu uliopita ambapo CAF ilikuwa inatoa kiasi cha Dola 4 milioni (Sh10 bilioni) kwa timu inayotwaa taji la Ligi ya Mabingwa Afrika.

Katika Kombe la Shirikisho Afrika, Azam FC na Singida Black Stars nazo zimepishana na noti za CAF.

Kwa mujibu wa CAF, kuanzia sasa bingwa wa Kombe la Shirikisho Afrika atapata kiasi cha Dola 4 milioni (Sh10 bilioni) ambacho ni ongezeko la asilimia 100 kutoka kiasi kilichokuwa kikitolewa mwanzo kwa bingwa.

Kabla ya msimu huu, timu bingwa wa Kombe la Shirikisho Afrika alikuwa akipata kiasi cha Dola 2 milioni (Sh5 bilioni).

Kiujumla, CAF imetenga kiasi cha Dola 18.8 milioni (Sh48.5 bilioni) kwa ajili ya zawadi kwa timu zinazoshiriki katika mashindano ya Klabu Afrika msimu huu.

Mabadiliko hayo yanaonekana kuwa ni utekelezaji wa ahadi ya Rais wa CAF, Patrice Motsepe ya kuziwezesha klabu za Afrika kiuchumi kupitia sapoti ya kifedha kwa zile zinazoshiriki mashindano hayo.

Ikumbukwe kwa sasa, kila timu inayoshiriki mashindano ya Klabu Afrika inakuwa na uhakika wa kupata kitita cha Dola 100,000 (Sh258 milioni).