BAADA ya kiungo mkabaji wa Simba, Yusuph Kagoma kuongeza mkataba wa miaka miwili kuendelea kuitumikia timu hiyo, ameelezea safari yake mpya namna alivyo na kazi ya kuhakikisha mchango wake unakuwa muhimu katika kutimiza malengo ya timu.
Kagoma aliyezaliwa Gungu, Kigoma Aprili 3, 1996 na sasa ana umri wa miaka 29), alijiunga na Simba Julai 8, 2024 akitokea Singida Fountain Gate (kwa sasa Fountain Gate) akisaini mkataba wa miaka miwili uliokuwa unakwenda ukingoni mwishoni mwa msimu huu.
Kabla ya mkataba wake wa awali kumalizika, Simba imeona imuongezee miaka miwili hadi 2028 kuendelea kukichafua Msimbazi.
Akizungumza na Mwanaspoti, Kagoma alisema kitendo cha kusaini mkataba mwingine kinaonyesha bado benchi la ufundi na viongozi wanakiamini kipaji chake, hivyo anaona ana kazi kubwa ya kuipambania klabu hiyo, kama alivyoaminiwa.
“Jambo kubwa na la msingi nipo kwa ajili ya kuipambania klabu katika malengo iliyojiwekea, ili iendelee kufanya makubwa ligi ya ndani na Kimataifa mwakani, kama mchezaji ni kuongeza bidii katika mazoezi ya timu na binafsi,” alisema Kagoma na kuongeza;
“Tuna kazi ya kuhakikisha tunayapambania mataji, ambayo ni hamu ya mashabiki hata sisi wachezaji, kwani ni raha sana mnapomaliza msimu kisha mnavaa medali za ubingwa, mapambano yetu yataendelea hadi pale ambapo tutafanikisha hilo.”
Kuhusu ushindani wa namba, Kagoma alisema kila anayecheza naye kuna kitu kinampa nguvu ya kupambana, kuhakikisha anakuwa katika kikosi cha kwanza, jambo linalomsaidia asijisahau na kuona amemaliza kazi.
“Nikizungumzia ushindani wa namba kila ninayecheza naye anakuwa na kitu kinachonipa morali ya kupambana, napenda ushindani ambao ndiyo sababu ya kunisaidia kuwa bora, hapo namaanisha hadi walioondoka kama Fabrice Ngoma kuna kitu nilikipata kucheza pamoja naye,” alisema.
Aliyekuwa kocha wa Simba, Fadlu Davids ndiye aliyemsajili Alassane Kante kama mbadala wa Ngoma ili kusaidiana na Kagoma, lakini kuna wakati anachezeshwa na kiraka Naby Camara kama kiungo mkabaji, jambo ambalo Kagoma alisema anafurahia kucheza na kila mtu.
Kwa aina ya uchezaji wa Kagoma, kumemuibua staa wa zamani wa Simba, Yanga na Taifa Stars, Mohamed Simba Banka aliyesema: “Kuna viungo adimu kwa sasa wanaocheza boksi kwa boksi, Kagoma anajitahidi ndiyo maana anachezeshwa kikosi cha kwanza na akikosa kuanza ni mechi chache.”
Mbali na Kagoma, beki na nahodha wa kikosi hicho, Rushine De Reuck naye ameongeza mkataba wa mwaka mmoja baada ya ule wa sasa kuelekea ukingoni ukitarajiwa kumalizika mwisho wa msimu huu.
Rushine ambaye huu ni msimu wa kwanza anaichezea Simba, tayari amejenga ngome imara ya ulinzi akiwa kikosi cha kwanza.
“Nimefurahi kuona naendelea kuwa hapa. Naweza kusema nimekuja hapa kwa ajili ya kucheza mpira, ushirikiano uliopo baina ya mashabiki, viongozi na wachezaji ni miongoni mwa sababu ya kuongeza mkataba. Kikubwa nataka kuacha kumbukumbu na kuifanya klabu kufanikiwa zaidi.
“Malengo ni kuona timu inafanya vizuri zaidi, Simba haijashinda ubingwa wa ligi kwa muda mrefu kidogo, tutafanya kila liwezekanalo wachezaji kufanikisha. Ninaamini tutafanikiwa,” alisema Rushine.