KOCHA Mkuu wa Simba, Steve Barker ameeleza kile kipigo ilichopokea Singida Black Stars cha mabao 3-0 kutoka kwa Yanga, kwao kimewaongezea ugumu wanapokwenda kukutana na Walima Alizeti hao, lakini wamejipanga kufanya kweli.
Barker ameliambia Mwanaspoti: “Pamoja na ugumu huo, nimewajenga wachezaji kimbinu na utayari wa akili.”
Hivi sasa Simba imebakiwa na mechi 19 za Ligi Kuu Bara ambazo zina jumla ya pointi 57. Itaanza safari ya kuzikusanya pointi hizo dhidi ya Singida Black Stars, mechi itakayopigwa kesho Jumatano Uwanja wa Airtel uliopo Mtipa, Singida.
Kabla ya mechi hiyo, Singida imetoka kufungwa uwanjani hapo 3-0 na Yanga, Alhamisi iliyopita, hali inayomfanya Barker kukiri watakutana na ugumu kukabiliana na wapinzani wao hao kutokana na hawatakuwa tayari kuona wanapoteza mfululizo tena mbele ya wakongwe wa ligi hiyo ambao ni washindani wakubwa katika nafasi za juu.
Hata hivyo, Barker pamoja na kuzungumzia maandalizi ya mechi hiyo, lakini nguvu yake kubwa ni kupambania ubingwa ambao Wanamsimbazi wameukosa kwa misimu minne.
“Maandalizi yapo vizuri, mechi itakuwa mgumu, ushindani na mbinu zaidi, kila kitu kipo sawa na mazoezi ya mwisho yanafanyika kesho (leo),” alisema kocha huyo na kuongeza;
“Malengo ya timu ni kupambania ubingwa wa Ligi Kuu pamoja na Kombe la Shirikisho (FA), hakuna mechi rahisi kwa sababu kila timu ina malengo yake, kikubwa nafurahishwa na mwendelezo wa kiwango wanachokionyesha wachezaji.”
Barker anayeinoa Simba kwa msimu wake wa kwanza akiwa na miezi miwili na siku 20, alikiri ugumu wa ligi hiyo, lakini nguvu ya pamoja kuanzia wachezaji, benchi la ufundi na viongozi anaamini itakwenda kuzaa matunda katika kukokotoa hesabu za pointi hizo.
Simba ikikusanya pointi 57, itamaliza msimu na pointi 81 na kwa mara ya mwisho kuchukua ubingwa wa ligi ni msimu wa 2020-2021 ilimaliza na alama 83.
Simba itashuka dimbani ikiwa na kumbukumbu ya kutoka sare katika mechi mbili zilizopita za Ligi Kuu Bara dhidi ya Dodoma Jiji na Yanga kabla ya mechi ya Kombe la FA kushinda 2-0.
Kwa upande wa Singida Black Stars, itafanya maandalizi yake ya mwisho huku ikiwa na kumbukumbu ya kuichapa Simba mabao 3-1 katika mechi ya mwisho kukutana na ilikuwa ni nusu fainali ya Kombe la FA msimu uliopita 2024-2025.
Takwimu zinaonyesha katika mechi tano zilizopita baina timu hizo, Simba imeshinda tatu zote za ligi, moja sare huku Singida Black Stars ikishinda mara moja tu na ndio ilikuwa mechi ya mwisho kukutana.
Simba imeshinda mechi hizo kwa tofauti ya bao moja, ikiwemo mbili za msimu uliopita katika ligi na ilishinda kwa bao 1-0 katika mechi ya mzunguko wa kwanza kwenye uwanja wa Liti na kurudia matokeo hayo Uwanja wa KMC.