SIMBA inapiga hesabu za kumchukua staa wa ASEC Mimosas, Souleymane Fofana ambaye ni mjuzi wa kufumania nyavu kwa mabao ya viwango. Sasa uongozi wa klabu yake umefunguka namna ya kukamilika kwa dili hilo.
Simba inapiga hesabu kali za kumsajili mshambuliaji Fofana anayeichezea ASEC Mimosa mwisho wa msimu baada ya kuwa na kiwango bora msimu huu akiwa amefunga jumla ya mabao 11 na asisti tano.
Mapema tu Rais wa ASEC, Roger Ouegnin akizungumza kwa njia ya simu na Mwanaspoti, alisema bado hawajapokea ofa rasmi ya Simba kumhitaji Fofana akiamini klabu hiyo itafuata utaratibu endapo inamtaka.
Ouegnin alisema ASEC haina kigugumizi kwenye kufanya biashara juu ya mchezaji wao yeyote na kama Simba ikiwafuata dili hilo linaweza kufikia muafaka huku akiwatahadharisha kuna ofa nyingi za Fofana.
“Naweza kukuthibitishia hadi sasa hatujapokea ofa yoyote kutoka Simba kama unavyouliza, Fofana ni mchezaji wetu anaendelea kutumikia mkataba wake, wote tunafurahia kiwango chake,” alisema Ouegnin.
“ASEC hatuna shida kwenye kufanya biashara kwa wachezaji, kama tukikubaliana kila kitu kinawezekana lakini huyu Fofana ana ofa nyingi sana hapa Afrika na hata Ulaya, kwetu sisi tutaangalia kipi kitafikia mahitaji tunayoyataka na tunaweza kumuachia mchezaji.
“Unakumbuka kuna wachezaji tuliwauza huko Tanzania akiwemo Zouzoua (Pacome) na mwingine alikwenda timu moja ya hapo, hakuna tatizo kwetu tunachotaka ni kuona klabu zinaiheshimu ASEC kwa kutufuata.
“Simba wakija tutawaambia thamani ya mchezaji ni kiasi gani lakini hatuwezi kusema sasa tutahitaji kiasi gani.”
Wakati Ouegnin akiyasema hayo, beki wa zamani wa Simba, Zana Coulibally amekoleza moto akisema kama mabosi wa klabu hiyo wakimpata Fofana watakuwa wamelamba dume kutokana na ubora wake.
Coulibally raia wa Ivory Coast ambaye amewahi kuwatumikia wekundu hao, alisema; “Nimesikia Simba wanamtaka Fofana, ni mshambuliaji mzuri ambaye chimbuko lake lilianza kama kiungo mshambuliaji, kama watafanikiwa kumpata watakuwa wamepata mchezaji mzuri kwani ni kijana anayetafuta mafanikio makubwa.”