Doumbia ni suala la muda tu Yanga

UONGOZI wa Yanga, umetaja mambo mawili ambayo yatalifanya benchi la ufundi la timu hiyo kuamua kuwarejesha kikosini au kuachana na nyota watatu wa kimataifa ambao timu hiyo imewatoa kwa mkopo kwenda timu tatu tofauti katika nchi za Afrika Kusini, Algeria na Afrika Kusini.

Wachezaji hao ni Moussa Balla Conte aliyepo Raja Casablanca ya Morocco, Mohamed Doumbia aliyepelekwa Marumo Gallants ya Afrika Kusini ni Celestin Ecua ambaye yupo JS Kabylie ya Algeria.

Ofisa Habari na Mawasiliano wa Yanga, Ally Kamwe, alisema mambo wanayoyazingatia kwa nyota hao ni viwango wanavyoonyesha uwanjani na hali yao ya ufiti.

“Tunafuatilia kwa ukaribu maendeleo ya hao wachezaji. Watathmini wetu wa video wanawafuatilia kuangalia viwango vyao na kwa mechi ambazo wanacheza tumekuwa tukitazama na iwapo na sisi tu-nakuwa na mechi, huwa mechi zao zinarekodiwa kisha benchi la ufundi linakuja kuwatazama baadaye. Tumekuwa tukiwasiliana hizo timu kupata viwango vya utimamu ili kupata maendeleo yao.

“Baada ya msimu kumalizika, benchi la ufundi ndio litatoa tathmini ya jumla juu ya nafasi ya kila mmoja kama anarudishwa au la,” alisema Kamwe.

Kati ya hao watatu, Doumbia ndio anaonekana kuwa na nyakati bora zaidi kulinganisha na nyota wen-gine wa kimataifa ambao Yanga iliwatoa kwa mkopo dirisha dogo la usajili.

Tangu alipojiunga na Marumo Gallants, Doumbia amecheza mechi zote nne za timu hiyo kwa dakika 90 katika kila mechi, mara zote ikiwa ni katika Ligi Kuu Afrika Kusini.

Akicheza kama kiungo wa kati, Doumbia katika mechi hizo nne amefunga bao moja ingawa timu yake imepoteza michezo mitatu na kupata ushindi mara moja.

Aliye katika wakati mgumu anaonekana kuwa ni Moussa Balla Conte ambaye kwa sasa anacheza kwa mkopo hadi mwishoni mwa msimu.

Tangu Ecua alipojiunga na JS Kabylie katika dirisha dogo, winga huyo ametumika katika mechi tatu tu kati ya sita ambazo timu hiyo ya Algeria imecheza katika mashindano tofauti.

Mechi hizo zote tatu ambazo Ecua ameitumikia JS Kabylie ni za Ligi Kuu ya Algeria na moja timu yake imepata ushindi dhidi ya Paradou na michezo miwili dhidi ya MC Algiers na ES Mostaganem ilitoka sare.

Katika mechi hizo tatu, Ecua ametumika kwa dakika 105 sawa na wastani wa dakika 35 tu kwa mchezo na mara moja alianza kikosini na katika mechi mbili alitokea benchi.

Mchango mkubwa ambao Ecua ameutoa katika michezo hiyo mitatu ni kupiga pasi moja ya bao am-bapo alifanya hivyo dhidi ya Paradou na JS Kabylie iliibuka na ushindi wa mabao 3-2.

Mchezaji huyo raia wa Guinea, tangu ajiunge na Raja Casablanca ya Morocco, timu hiyo imecheza idadi ya mechi saba na kati ya hizo, Conte ametumika katika mchezo mmoja tu.

Mchezo huo mmoja ambao Conte alicheza ni dhidi ya RS Berkane uliomalizika kwa sare ya bao 1-1, kiungo huyo aliingia akitokea benchi katika dakika ya 63.