Dar es Salaam. Katika kipindi ambacho lugha ya Kiswahili inaendelea kupanua mipaka yake kimataifa, jina la Consolata Mushi limeendelea kujitokeza kama nguzo muhimu katika safari hiyo.
Akiwa Katibu Mtendaji wa Baraza la Kiswahili la Taifa (Bakita), Mushi ni miongoni mwa viongozi wanaoamini kwa dhati kuwa Kiswahili si tu chombo cha mawasiliano, bali ni rasilimali na fursa ya maendeleo kwa mtu binafsi na taifa kwa ujumla. Kupitia uongozi wake, Kiswahili kimepiga hatua kubwa katika taasisi za kikanda na kimataifa.
Katika mahojiano haya maalumu, Mushi anaangazia changamoto za uongozi, misingi inayomuongoza, hadi ndoto yake ya kuona Kiswahili kikitambulika zaidi duniani na namna kinavyoweza kuwa fursa ya kiuchumi.
Swali: Umefikaje hapo ulipo leo?
Jibu: Nilizaliwa mwaka 1969 Kibosho, Kilimanjaro. Elimu yangu ya msingi ilianza shule ya Masoka na Singachini, na baadaye kidato cha kwanza hadi cha sita Shule ya Wasichana Kibosho.
Baada ya mafunzo ya Jeshi la Kujenga Taifa, nilijiunga na chuo cha ualimu Marangu, nikaanza kufundisha shule kadhaa kabla ya kujiunga na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kwa masomo ya Shahada ya kwanza katika masomo ya Sayansi ya Siasa na Kiswahili mwaka 1997. Kisha nilifanya Shahada ya umahiri ambapo nilihitimu mwaka 2004 na baada ya hapo nilianza kazi Baraza la Kiswahili la Taifa mwaka 2004 nikiwa kama msanifu lugha. Nilidumu katika nafasi hiyo kwa miaka zaidi ya 10 hadi kufikia ngazi ya msanifu lugha mwandamizi.
Safari yangu ya uongozi imeanzia mbali, kutoka shule ya msingi, sekondari, jeshini hadi nilipoanza kazi ya ualimu.
Nikiwa Bakita nimekuwa mkuu wa idara ya istilahi na kamusi na kaimu mkuu wa sehemu ya uhusiano na umma. Pia, nimekuwa makamu wa katibu mtendaji kwa miaka minne na kaimu katibu mtendaji kwa miaka miwili na kisha Katibu Mtendaji kutoka mwaka 2021. Vilevile, nimefanya kazi kama mhadhiri wa muda Chuo Kikuu Huria cha Tanzania na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.
Fauka ya hayo, nimekuwa mchambuzi wa masuala ya lugha katika redio za ndani na nje ya nchi. Pia, nimekuwa mfasiri wa nyaraka mbalimbali kutoka Kiingereza kuja Kiswahili na mhariri wa vitabu kadhaa vilivyoandikwa kwa Kiswahili.
Swali: Ni changamoto zipi umekutana nazo kwenye maisha yako ya kitaaluma na uongozi na je changamoto hizo zimekuimarisha vipi kwenye uongozi?
Jibu: Kama ilivyo ada hakuna mwanadamu asiyekabiliwa na changamoto zozote, Nami nimekumbana na changamoto kadhaa hususan katika uongozi. Kila mtu ana matamanio yake na hasa angetamani kuyakamilisha kabla ya kumaliza muda wake wa utumishi wa umma.
Hata hivyo, si kila mmoja anaelewa ni nini angetamani kikamilike mapema kabla ya kustaafu utumishi wa umma na hivyo baadhi watashindwa kukusaidia ili kukamilisha lengo. Hata hivyo, changamoto hiyo imeniimarisha katika uongozi kwamba ni lazima ujitahidi kwa kadri ya upeo wa uelewa wako kukamilisha malengo yako. “ Kwenye msafara wa mamba na kenge wamo”
Aidha, binadamu kwa silika na maumbile yake, baadhi hawapendi kuona mafanikio ya wengine. Hivyo ukiwa kiongozi ni lazima ukubali kuwa wapo watakaokuelewa na wapo watakaokupinga kwa sababu tu ile nafsi ya umoja imeukamata moyo wake. Penye nia pana njia, Ukiwa kiongozi ni kuhakikisha unafanikisha malengo na hakuna cha kukuzuia.
Swali: Ni nini kilikuvutia kuchagua taaluma ya ualimu na lugha ya Kiswahili, na ulijuaje mapema kuwa huu ndiyo wito wa maisha yako?
Jibu:Binafsi nimekuwa na mapenzi makubwa kwenye lugha ya Kiswahili kutoka nikiwa shule ya sekondari hadi elimu ya juu. Mwanzo kabisa nilitamani kuwa mwandishi wa habari na daima niliona fahari kumsikia mwanamke akisoma habari kwa kujiamini na kwa lugha fasaha.
Baada ya kuchaguliwa kozi ya ualimu nilianza kupenda ualimu na niliamua kufanya kazi hiyo kwa jitihada na kwa nguvu zangu zote.
Kwa hakika ninapenda kazi ya ualimu kwa sababu inakupa marafiki wa ujanani na uzeeni na ni kazi ambayo hata ukiiacha heshima ya ualimu inabaki. Nikiwa katika shughuli zangu hivi leo ninasalimiwa: “Shikamoo mwalimu” ninashangaa ni nani wewe ndugu yangu, ananikumbusha kwa furaha, Mwalimu ulinifundisha, kwangu hiyo ni zawadi.
Ualimu wa lugha kwangu ni kivutio zaidi na hii ni kwa namna nilivyowaona walimu wangu walivyokuwa wakiona fahari kufundisha Kiswahili. Mbegu yao ikamea kwangu na hata leo imezaa mti utakaoacha matunda.
Swali: Kama mwanamke anayeongoza taasisi muhimu ya lugha ya taifa, ni mitazamo ipi ya kijamii au kitaasisi ulihitaji kuibadilisha?
Jibu: Kutoamini katika kile ulichonacho. Baadhi ya watu wanadhani kuwa Kiswahili ni lugha hafifu na haina nguvu kimataifa hilo kwangu ni kinyume kabisa. Dhima ya lugha yoyote ni mawasiliano na hakuna lugha iliyo bora kuliko nyingine. Kiswahili kinaweza na hatuna budi kuachana na dhana potofu kuwa Kiswahili si lugha kubwa na ya kimataifa.
Swali: Ni kwa namna gani kazi yako Bakita imechangia si tu maendeleo ya Kiswahili, bali pia kujenga nafasi za wanawake katika masuala ya sera na lugha?
Jibu: Nikiwa kiongozi ambaye katika utumishi wangu yametokea mambo makubwa kuhusu Kiswahili, inanifanya kuamini kuwa chini ya uongozi wa mwanamke mambo makubwa yanaweza kutokea. Kufanikiwa huku kunawafanya wanawake si tu kuaminika bali pia kuwa na uwezo wa kushiriki kikamilifu katika masuala ya sera za kuleta mageuzi.
Kiswahili kimepiga hatua kubwa sana na sasa kimekubaliwa kuwa lugha rasmi katika mikutano mikuu ya Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (Unesco). Ni lugha rasmi katika Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC), lugha rasmi ya Umoja wa Afrika (AU) na Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC). Aidha, kwa sasa tayari tumeanza harakati za kukiingiza Umoja wa Mataifa jambo ambalo ninaamini litatokea muda si mrefu.
Swali: Uongozi wako katika nyadhifa mbalimbali za Bakita umekufundisha nini kuhusu subira, uthabiti na uamuzi mgumu kama kiongozi mwanamke?
Jibu: Hizi ni nguzo muhimu kwa kiongozi yeyote yule, kwani pasipo subira utaharibu baadhi ya mambo. “Subira yavuta heri” Wahenga hawakokosea waliposema hayo wakiwa wametathmini mambo mengi. Katika uongozi kuna vitu unatamani lakini baadhi vinahitaji subira ili vitokee. Hivyo kila kiongozi anayejielewa ni muhimu kuwa na subira. Labda nitoe mfano: “usimuhukumu mtu yeyote pasipo kutulia na kufanya tathmini ya kina”. Jihoji kabla ya kuamua.
Je, hayo unayoyaona makosa ni endelevu? Umewahi kumnasihi huyo unayemtuhumu? Mkanye na umpe nafasi ya kujirekebisha. Miongoni mwa wenye sifa hizo hubadilika na kuwa wazuri na pengine wakawa washauri wako na kupitia wao ukafanikiwa. Hayo ni matokeo ya subira.
Vilevile, uwe thabiti katika utendaji na uamuzi wako, Ukikosa haya huwezi kufanikiwa kwani kipimo cha kiongozi ni uthabiti katika kuamua na namna ya kukabili mambo magumu. Kuwa na uwezo wa kutoa uamuzi sahihi katika nyakati zote. Lakini ikitokea umefanya uamuzi na baadaye ukabaini umekosea uweze kurudi nyuma na kusahihisha, kwani “binadamu ni kilihafi na hakosi uchafu” kubali kuwa unaweza kukosea.
Swali: Unaonaje nafasi ya Kiswahili katika kuwawezesha wanawake kiuchumi, kielimu na kisiasa ndani na nje ya Tanzania?
Jibu: Kiswahili kina nafasi kubwa ya kuwaendeleza wanataaluma wake na wanajamii kwa ujumla. Kupitia nafasi ya Kiswahili kwa sasa duniani, ni dhahiri kuwa kipo kwenye nafasi ya kuwanufaisha wanataaluma wake. Hivyo, wanawake wanaweza kunufaika kupitia Kiswahili kwa kuwa walimu weledi, wafasiri, wakalimani, waandishi wa vitabu lakini pia kupitia kazi mbalimbali za sanaa.
Kwa upande wa siasa, kwanza weledi kisiasa unahitaji uwezo mzuri wa kutumia lugha na si lugha tu bali Kiswahili kwa Watanzania. Wanawake wanayo nafasi kubwa ya kuitumia fursa hii kupata nyadhifa za kisiasa. Kinamama ni hodari wa kunadi jambo lakini pia kulisimamia. Hivyo, kwa kukijua vyema Kiswahili kutawawezesha kupata majukwaa fulanifulani ya kisiasa. Sisemi kwamba wasiwe na taaluma, ninachokusudia ni kuongeza thamani kwa kuweza kujieleza vizuri na kwa lugha ya utulivu na yenye mvuto.
Kielimu bado kinamama wana nafasi kubwa ya kujiendeleza katika Kiswahili. Leo, unaweza kusoma hadi shahada ya uzamivu kwa Kiswahili jambo ambalo wakati wetu halikuwezekana.
Swali: Ni ushauri gani ungependa kuwapa wasichana na wanawake wanaopenda lugha lakini wanaona taaluma hiyo haina fursa kubwa?
Jibu: Ninachoweza kuwashauri ni kuwa lugha ni msingi wa kila kitu katika maisha. Hakuna chochote kinachowezekana bila lugha. Huu ni mhimili mkubwa. Tusome lugha na itukutanishe na fursa nyingi duniani. Mama ni mwalimu wa lugha kwa viumbe wote.
Mtoto hufundishwa lugha ya kwanza kupitia mama. Hivyo, tujiamini kwamba kibali cha kujua lugha na kuitumia vizuri tulijaliwa na Muumba, na kwa sababu hiyo kupitia kipaji hicho tunaweza kuwa walimu wazuri wa Kiswahili ndani na nje ya nchi.
Swali:Ungependa kukumbukwa vipi kama mwanamke na kiongozi katika historia ya maendeleo ya Kiswahili?
Jibu: Ninatamani nikumbukwe kwa matumizi ya Kiswahili kutandawaa duniani lakini kama mwanamke ninayeamini kuwa Kiswahili ni pesa na fursa hii ninatamani itumiwe vizuri kiasi kwamba Kiswahili baadaye kiwe na mchango mkubwa kwenye pato la mtu binafsi na taifa kwa ujumla.