Viongozi 70 CCM Moshi wasaini kumkataa kigogo mwenzao

Dar es Salaam. Msuguano ndani ya Chama cha Mapinduzi (CCM), Wilaya ya Moshi Mjini, mkoani Kilimanjaro unaonekana kuingia katika hatua ngumu zaidi baada ya viongozi 70 kusaini barua ya kutokuwa na imani na kigogo wa chama hicho ngazi ya wilaya.

Taarifa za uhakika zilizolifikia Mwananchi, zinaeleza miongoni mwa waliosaini barua hiyo iliyotumwa kwa Katibu wa CCM Mkoa wa Kilimanjaro ni madiwani na wajumbe wa Halmashauri Kuu ya chama hicho wilaya ya kichama ya Moshi Mjini.

Wajumbe hao wanamtuhumu kiongozi huyo kwa kutengeneza majungu na kufitinisha viongozi wenzake jambo linalosababisha mpasuko na kugawa wanachama na viongozi.

Ujumbe wa kiongozi huyo (jina linahifadhiwa kwa sasa) aliouweka kimakosa katika ukurasa wake wa WhatsApp Jumapili ya Februari 22,2026 akitamba kumshughulikia Meya Zuberi Kidumo na Mkurugenzi wa Manispaa, Mwajuma Nasombe umekoleza moto huo.

Katika ujumbe huo ambao aliufuta baadaye ulikuwa unasomeka: “Hii ndio habari ya mjini kaeni mkao wa kula. Tumeshawasha taa nyekundu, hatutabakisha mtu, tunawatoa wote,” unasomeka ujumbe huo uliosambaa mitandao ya kijamii.

Wanadai kwa kuwa jambo hilo ni zito na linaleta mpasuko na mgawanyiko kwa wanaCCM na linavunja mahusiano mema kati ya CCM na Serikali, wameamua kukijulisha chama kuwa kiongozi huyo anakivuruga chama hicho na kukishushia hadhi.

Mwenyekiti wa CCM Moshi mjini, Faraji Swai (kushoto) akiteta jambo na Katibu wake, Amosi Shimba, katika kikao cha Halmashauri Kuu ya CCM Moshi mjini kilichofanyika Jumamosi Machi 7,2026.



Kwa mujibu wa andiko hilo, wanadai kiongozi huyo ameonyesha wazi hamuungi mkono meya na mkurugenzi wa manispaa na kushindwa kuwaunganisha wanachama na viongozi kwa madai ya kuendekeza majungu na mpasuko.

Jana Machi 9, 2026, wajumbe wote waliosaini andiko hilo walitakiwa kufika mbele ya sekratarieti ya CCM mkoa ili kuhojiwa juu ya malalamiko yao, lakini waliofika walikuwa watatu pekee.

Waliosaini andiko hilo la Februari 23, 2026 ambalo ndio kiini cha purukushani zilizoibuka katika kikao cha Halmashauri Kuu ya CCM Mkoa Kilimanjaro iliyoketi Machi 7, 2026, walitaka suala hilo lijadiliwe kwanza kabla ya kuanza kikao.

Leo Jumanne, Machi 10, 2026 Kamati ya Siasa ya Mkoa wa Kilimanjaro inakutana chini ya Mwenyekiti wake, Patrick Boisafi na inaelezwa miongoni mwa mambo yatakayotawala mijadala ya kikao hicho ni mtafaruku unaoendelea.

Alipotafutwa na Mwananchi asubuhi ya leo kuzungumzia hilo, Boisafi amesema yupo kikaoni na kwamba atafutwe baadaye.

“Sasa hivi nipo kwenye kikao cha kamati ya siasa kama hutojali nipigie kwenye saa tisa, 10 hivi,” amesema Boisafi.

Kwa upande wa Katibu wa CCM mkoa huo, Mercy Mollel alipokea simu na kujibu kwa kunong’ona kuwa, “Nipo kikao… kikao.”

Msuguano kikao cha Halmashauri kuu

Kutokana na msuguano huo, kikao cha Halmashauri Kuu ya chama hicho ambacho kiliketi Machi 7, 2026 katika ukumbi wa CCM mkoa almanusura kisifanyike, kama sio busara za Boisafi.

Kikao hicho kilichokuwa na ajenda ya kupokea taarifa ya utekelezaji ilani ya CCM, kilihudhuriwa pia na Mkuu wa Wilaya ya Moshi, Godfrey Mzava na Mbunge wa Moshi mjini, Ibrahim Shayo, ambaye hata hivyo aliondoka baadaye.

Tukio hilo linakuja takribani wiki moja tangu mlezi wa mkoa huo kichama ambaye pia ni Mjumbe wa Kamati Kuu (CC) na Katibu wa Siasa na Uhusiano wa Kimataifa, Rabia Hamid, kuitisha kikao cha maridhiano kilichofanyika Machi 1, 2026.

Kikao hicho kilihudhuriwa na Sheikh wa Mkoa wa Kilimanjaro, Shaaban Mlewa, Mkuu wa Mkoa Kilimanjaro, Nurdin Babu, Mkuu wa Wilaya ya Moshi, Mbunge wa Moshi Mjini na Meya wa Manispaa ya Moshi, Zuberi Kidumo.

Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Kilimanjaro, Patrick Boisafi.



Wengine waliohudhuria ni mjumbe wa Halmashauri Kuu (NEC), Seleman Mfinanga, Katibu mwenezi wa CCM Manispaa ya Moshi, Athman Ally na Diwani wa Kata ya Bomambuzi, Juma Raibu na Mwenyekiti CCM Wilaya, Faraji Swai.

Baada ya Mwenyekiti wa CCM Moshi Mjini, Faraji Swai kufungua kikao hicho, walijitokeza baadhi ya wajumbe wakimtaka apokee taarifa au malalamiko hayo kabla ya taarifa ya utekelezaji wa ilani kuwasilishwa kikaoni hapo.

Wakati kundi hilo likipaza sauti likimtaka mwenyekiti apokee taarifa kabla ya kuendelea na kikao, liliibuka kundi lingine likipaza sauti kuwa hao wanaoleta tafrani waondolewe ukumbini, tafrani zilizodumu kwa takribani dakika 10.

Mwenyekiti huyo wa wilaya akalazimika kusimama na kueleza kuwa “Napenda niwafahamishe kwamba sina ajenda ya taarifa. Sina ajenda ya taarifa na sina taarifa ya kupokea kutoka kwenu. Huo sio utaratibu wa chama chetu”

“Mimi nimetangaza rasmi kwamba nimefungua kikao kiendelee chama chetu kina utaratibu wake na hawa vijana wamejipanga kuleta vurugu. Nakuomba (kiongozi wa usalama) uchukue nafasi yako,” alisisitiza.

Hata baada ya kauli hiyo, bado kundi lililokuwa likimtaka apokee taarifa kwanza walisikika wakipaza sauti kuwa “hakuna kikao hapa hadi upokee taarifa”, huku kundi lingine likitaka kundi hilo linaloleta tafrani liondolewe ukumbini.

Kutokana na tafrani hiyo, wakuu wa idara na wataalamu wa Halmashauri ya Manispaa ya Moshi waliokuwa wawasilishe taarifa ya utekelezaji walitoka nje na baadaye kurudi ukumbini baada ya hali kutulizwa na Boisafi.

Akizungumza katika kikao hicho, Boisafi alisema kilikuwa ni mahsusi kuangalia utekelezaji wa ilani ya uchaguzi kwa miezi sita kuanzia Juni hadi Desemba 2025 na akawaomba radhi wataalamu wa halmashauri kwa kile kilichotokea ukumbini.

“Wataalamu hapa mmeona vitu ambavyo hamkuzoea kuviona lakini hizi ndio siasa. Hakuna jambo la ajabu limetokea ni jambo la kutafakarisha na nasikitika. Kikao hiki kina ajenda, na ajenda ziko nne,” alisema mwenyekiti huyo.

“Kuna ajenda zinahusu utekelezaji wa ilani ya CCM ambayo kwayo nyinyi wataalamu mngekuwa mnawasilisha kwa kupitia kamisaa wetu, tukimaliza tungewaomba mtoke nje na waandishi wa habari pia wangetupisha,” alisema.

“Lakini yametokea yaliyotokea. Haya yatajadiliwa baada ya kupokea taarifa ya utekelezaji wa ilani ya chama chetu na agenda itakayofuata na mwenyekiti wa wilaya atasimamia,”alisisitiza Boisafi wakati akijaribu kuweka mambo sawa.

“Chama chetu kina taratibu zake. Unaandika kwa mamlaka, watasoma watakuiteni  na kuwasikiliza na baadaye kujadiliana. Kukosoa na kukosolewa  ni sehemu ya miongozo kwenye chama chetu,”alisisitiza Boisafi na kuongeza kusema kuwa,

“Tusipoenda hivyo, mnajua hii wilaya ilikuwa wapi. Miaka 25 tumekataa maendeleo yetu wenyewe. Miaka mitano ya nyuma tukakubali tunataka maendeleo, miaka mitano hii (2025-2030) tukasema tunataka maendeleo.”

“Lakini sasa kama tunataka kuturejesha kule tulipotoka. Niwaombe wajumbe wa Halmashauri Kuu wa wilaya ya Moshi mjitafakari. Tunataka kurudi kule tulipotoka au tunataka kwenda mbele na kwenda mbele tunatakiwa tufanye nini”

“Tunasema mamlaka yanatoka kwa Mungu, basi tuheshimu mamlaka. Tusikilize . Kama kuna ushauri tuutoe. Tusiposikilizwa  ndio hatua zinazostahiki zilichukuliwe”.

“Lazima tujue hilo, na kuonyesha ukomavu, kukua kisiasa , kwenye maisha , kwenye uchumi na nini  lazima muonyeshe. Mlichokionyesha hapa mbele ya hawa watendaji, kesho kutwa mtaenda kukagua miradi pia”alisema na kuongeza;,

“Wameona pia mlivyojipambanua hapa. Sasa mkijipambanua tofauti mnawashauri nini. Kwa hiyo nyinyi watendaji mjisikie hamjaona jambo la ajabu tuliopewa dhamana na wanachama wetu mjisike hamjafanya jambo zuri.”

Habari kutoka ndani ya CCM, zinadai mgawanyiko na mpasuko ulianzia katika mchakato wa kura za maoni ya ubunge 2020 na 2025 ila hakuna jitihada za kuvunja makundi zinaonekana kufanywa na viongozi.