Azam yairudisha Yanga Benjamin Mkapa, yataja sababu

Azam imethibitisha kwamba mchezo wake dhidi ya Yanga, Jumapili, Machi 15, 2026 utachezwa katika Uwanja wa Benjamin Mkapa badala ya Azam Complex, Dar es Salaam.

Ofisa Habari na Mawasiliano wa Azam FC, Thabit Zakaria ‘Zaka Zakazi’ amesema kuwa wameamua kucheza mechi hiyo katika Uwanja wa Benjamin Mkapa kwa vile wamiliki wamewapa ruhusa ya kuutumia kwa sababu ukarabati wake bado haujaanza.

“Kabla ya msimu kuanza, Azam FC tulichagua kutumia Uwanja wa Benjamin Mkapa kwa mechi zetu mbili za nyumbani dhidi ya Yanga na Simba badala ya Azam Complex. Sasa tulivyoona taarifa kuwa Uwanja utafungwa kwa ukarabati, tukawa tunaangalia uwezekano wa mchezo huo kuchezwa katika Uwanja wa Azam Complex lakini wamiliki wa Uwanja wa Benjamin Mkapa wakatuelekeza kuwa hautotumika pale maboresho yake yatakapoanza na sio kwa sasa hivyo tunaweza kuutumia.

“Uwanja wa Benjamin Mkapa tunaamini tutakuwa na faida zaidi kucheza dhidi ya Yanga kwa sababu tumeshakutana nao pale mara nyingi na tumewafunga sana katika ule Uwanja.

“Hivyo tuwaondoea wasiwasi mashabiki wa Azam na wapenda soka kiujumla kwamba hatuna hofu ya kukutana na Yanga katika Uwanja wa Benjamin Mkapa na tunaamini tutapata matokeo mazuri,” amesema Zaka.

Ikumbukwe mchezo wa mwisho wa Ligi Kuu ambao Azam ilicheza katika Uwanja wa Benjamin Mkapa ulikuwa ni wa mzunguko wa kwanza msimu huu dhidi ya Simba ambao iliibuka na ushindi wa mabao 2-0.

Katika mchezo huo ambao ulichezwa Desemba 7, 2025, mabao ya Azam yaliwekwa kimiani na Japhte Kitambala na Idd Seleman ‘Nado’.

Mara ya mwisho kwa Yanga na Azam kucheza katika Uwanja wa Benjamin Mkapa ilikuwa ni Machi 17, 2024 katika mechi ya mzunguko wa pili wa Ligi Kuu Tanzania Bara.

Katika mchezo huo, Azam FC iliibuka na ushindi wa mabao 2-1 yaliyowekwa kimiani na Gibril Sillah na Feisal Salum huku bao la Yanga likifungwa na Clement Mzize.

Yanga kwa sasa inaongoza msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara ikiwa imekusanya idadi ya pointi 32 katika mechi 12.

Kwa upande wa Azam FC, iko nafasi ya tatu katika msimamo wa ligi ikiwa imevuna idadi ya pointi 24 katika michezo 12.