Dar es Salaam. Katika Kijiji cha Kasanga, wilayani Nkasi, Mkoa wa Rukwa, simulizi ya Gabriel Mkwiti (60) imeacha maswali mengi kuhusu kilichotokea siku mke wake alipokwenda kujifungua katika hospitali ya wilaya, tukio analodai liliwaacha na mtoto mmoja badala ya pacha kama ambavyo kadi ya kliniki inavyoonesha.
Mkwiti ametoa simulizi ya tukio hilo leo Jumanne, Machi 10, 2026 katika mkutano wa Waziri Mkuu, Dk Mwigulu Nchemba anayeendelea na ziara mkoani Rukwa.
Amesema Oktoba mwaka jana mke wake alikwenda katika Hospitali ya Wilaya ya Kalambo kwa ajili ya kujifungua.
Mkwiti amesema baada ya upasuaji mke wake alimweleza kuwa alijifungua watoto pacha na hata kwenye kadi ya kliniki kulikuwa na taarifa zilizoonesha hivyo.
Hata hivyo, wakati wa kuruhusiwa kutoka hospitali, alikabidhiwa mtoto mmoja pekee.
“Mke wangu aliporudi nyumbani aliniambia wazi kwamba amejifungua watoto pacha. Alinionesha kadi ya kliniki yenye vielelezo hivyo, lakini alipewa mtoto mmoja tu,” amesema Mkwiti.
Amesema mke wake alipojaribu kuuliza kuhusu mtoto wa pili akiwa hospitalini, alifokewa na wahudumu na kuambiwa asijadili zaidi suala hilo.
Kutokana na hali yake ya ulemavu inayomfanya ashindwe kusafiri kwa urahisi, Mkwiti amesema hakuwahi kwenda hospitalini kufuatilia jambo hilo, badala yake, aliamua kumtafuta daktari wa zahanati katika eneo lao na kumueleza kilichotokea.
“Oktoba 28, 2025 nilienda kwa daktari nikamueleza tatizo hili ili anishauri nifanye nini. Aliniambia atalifuatilia lakini akanisisitiza nisizungumze na mtu yeyote hadi watakapopata ufumbuzi,” amesema.
Tangu Oktoba mwaka jana hakukuwa na majibu yoyote hadi Februari 6, 2026 baada ya viongozi kutoka hospitali ya wilaya kufika nyumbani kwake kumuhoji kuhusu tukio hilo.
Mkwiti amesema aliambiwa hadi kufikia Jumatatu wangekuwa tayari wamempatia majibu.
Hata hivyo, siku iliyofuata alipokea simu kutoka kwa Mganga Mkuu wa Wilaya ya Kalambo akimtaka afike wilayani kwa ajili ya mazungumzo kuhusu suala hilo.
“Nikamwambia kutokana na hali yangu ya ulemavu na mazingira ya nyumbani sina fedha za kwenda wilayani mara moja, nikamuomba anipe muda kidogo na akakubali,” amesema.
Amesema awali alitakiwa kufika Jumatatu, lakini siku iliyofuata aliambiwa asiende siku hiyo kwa sababu ya ziara ya Waziri Mkuu wilayani humo.
“Aliniambia niende Jumanne baada ya Waziri Mkuu kuondoka. Nikamuuliza kwa nini nisubiri hadi aondoke, akasema suala hili linaweza kumfukuzisha mtu kazi, hivyo wanahitaji kwanza kulijadili,” amesema.
Mkwiti amesema baadaye baadhi ya viongozi walifika nyumbani kwake na kumtaka aende katika ofisi ya mwenyekiti wa kijiji ili wazungumze na kumaliza suala hilo.
Hata hivyo, alikataa kwenda yeye na mke wake peke yao, akisisitiza ndugu na jamaa wanapaswa kuwepo ili kusikiliza maelezo yote.
“Niliwaambia siwezi kwenda peke yangu na mke wangu wakati nimewasilisha taarifa tangu mwezi wa kumi lakini hakuna aliyelipeleka suala hili polisi au kwa viongozi wa Serikali,” amesema.
Waziri Mkuu, Dk Mwigulu amemtaka, Mganga Mkuu wa Wilaya ya Kalambo (hakutaja jina lake) kuzungumzia suala hilo ambaye amekiri kupata malalamiko hayo Machi 5, 2026 na alianza kuchukua hatua za ufuatiliaji kubaini ukweli.
“Nilipopata taarifa hizi, nilikwenda kuzungumza na familia ile, bado nikarudi kuangalia nyaraka za hospitali, kumbukumbu za upasuaji zinaonesha mama huyo alijifungua mtoto mmoja mwenye uzito wa kilo tatu.
“Bado hiyo haikuniridhisha ikabidi tuitishe kikao cha watumishi wote waliomhudumia yule mama kuanzia siku aliyoingia hadi ameruhusiwa. Tuliangalia pia kitabu cha wodini kinachorekodi taarifa za wazazi, nacho kinaonesha alijifungua mtoto mmoja,” amesema.
Amesema uchunguzi wao ulibaini siku ambayo mama huyo aliruhusiwa kutoka hospitalini, kulikuwa na mama mwingine kutoka Kijiji cha Msanzi aliyekuwa amejifungua watoto pacha.
“Katika kuandika taarifa, nesi aliingiza taarifa za mama huyo wa Msanzi kwenye kadi ya mama huyu, hivyo kusababisha mkanganyiko,” amesema.
Dk Mwigulu atoa maelekezo
Baada ya kusikiliza pande zote mbili Waziri Mkuu alivielekeza vyombo vya uchunguzi ikiwamo Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), ofisa wa usalama wa mkoa na chombo kinachohusika na maadili ya wanataaluma wa afya kufanya uchunguzi wa kina wa tukio hilo.
Amesisitiza uchunguzi huo uangalie kwa undani ikiwa ni pamoja na uwezekano wa kufanya vipimo vya vinasaba (DNA) ili kubaini ukweli.
“Anzeni na nesi aliyejaza taarifa. Inawezekanaje kufanya kosa kwenye jambo nyeti kama hili? Pia, tujue kama kweli mama mwingine aliyesemekana ana pacha hajapewa mtoto asiye wake,” amesema.
Amesema uchunguzi huo ni muhimu ili haki ya wazazi hao iweze kujulikana, huku akiwataka mkuu wa mkoa na mkuu wa wilaya kufuatilia kwa karibu suala hilo.