Arusha. Mahakama ya Rufaa imebariki hukumu ya kunyongwa hadi kufa waliyokuwa wamehukumiwa watu watatu baada ya kupatikana na hatia ya kumuua Peter Mwita kwa kumshambulia kumpiga na matofali, vijiti, mbao na chuma.
Ilidaiwa siku ya tukio, pacha wa Peter, Zumba Mwita (shahidi wa tatu wa Jamhuri) alipopita eneo lililokuwa likiendelea kujengwa na warufani hao wakifanya kazi walidai Zumba ameiba baadhi ya vifaa vya ujenzi na kuanza kumshambulia na kusababisha kifo chake.
Uamuzi huo ulitolewa Machi 6,2026 na jopo la majaji watatu wa Mahakama ya Rufaa walioketi Dar es Salaam, ambao ni Barke Sehel,Leila Mgonya na Khamis Ramadhan Shaaban.
Warufani katika kesi hiyo ni Yohana Mgoli, Edwin Siwale na Iddi Mdaturu, ambao walikata rufaa kupinga hukumu ya Mahakama Kuu iliyotolewa Aprili 24, 2024.
Katika hukumu hiyo Mahakama ya Rufaa ilisema baada ya kupitia ushahidi wote uliowasilishwa katika kesi hiyo, imejiridhisha kwamba upande wa mashtaka uliweza kuthibitisha shtaka la mauaji dhidi ya warufani hao bila kuacha shaka yoyote.
Mahakama ya Rufaa ilikubaliana na warufani kwamba gwaride la utambuzi lilikuwa na kasoro za kitaratibu na kutokana na dosari hizo, mahakama iliamua kuondoa ushahidi wa gwaride la utambuzi kutoka kwenye rekodi ya kesi.
Hata hivyo, majaji walisema kuwa bado kulikuwa na ushahidi mwingine wa kutosha uliowaunganisha warufani na tukio la mauaji.
Jaji Sehel amesema kuwa mashahidi wawili muhimu waliwatambua warufani hao kwa sababu walikuwa wanawafahamu kabla ya tukio hilo na kueleza kuwa tukio lilitokea mchana kweupe na mashahidi walikuwa karibu sana na washambuliaji, hivyo hali ya utambuzi ilikuwa nzuri.
Mahakama pia ilisema kuwa maelezo ya mashahidi kuhusu jinsi marehemu alivyoshambuliwa yalikuwa wazi na ya kuaminika ambapo pia ilikataa hoja ya warufani kwamba ripoti ya uchunguzi wa maiti haikuwa halali kisheria.
Jaji amesema ingawa fomu iliyotumika ilikuwa imepewa jina tofauti, maudhui yake yalikuwa sawa na fomu inayotakiwa kisheria na kueleza kwa sababu hiyo, kasoro hiyo haikuathiri uhalali wa ushahidi wa kitabibu uliowasilishwa.
Baada ya kupitia mwenendo, ushahidi na sababu za rufaa, Mahakama ilifikia hitimisho kwamba upande wa mashtaka uliweza kuthibitisha vipengele vyote muhimu vya kosa la mauaji na warufani walihusika moja kwa moja katika shambulio hilo.
Aidha, mahakama ilibainisha kuwa namna walivyomshambulia marehemu kwa kutumia vyuma, vijiti na matofali ilionesha wazi nia mbaya ya kusababisha madhara makubwa au kifo, kutokana na sababu hizo, Mahakama ya Rufaa iliamua kwamba rufaa ya warufani haina msingi
Ilidaiwa Machi 27, 2022, shahidi wa pili, Mwita Messo akiwa na wanawe pacha, Zumba Mwita (shahidi wa tatu) na Peter (marehemu kwa sasa),wakiwa shambani aliwatuma nyumbani mmoja kwenda kuchota maji na mwingine kununua chakula.
Shahidi wa tatu alipopita karibu na eneo la ujenzi, warufani waliokuwa wakifanya kazi katika eneo hilo walimshtaki kwa kuiba baadhi ya vifaa vya ujenzi ambapo walimkamata na kuanza shambulio la kikatili, wakimpiga kwa matofali, vijiti, mbao na chuma.
Baadaye, mmoja wa washambuliaji alikwenda kumtafuta pacha wake ( Peter) na kumleta eneo la tukio, ambapo wote wawili walishambuliwa.
Shahidi wa pili alidai alipokuwa njiani kurudi nyumbani, aligundua umati wa watu uliokusanyika karibu na duka la Manyitu na alipokaribia mahali hapo, alishtuka kuona wanawe pacha wakishambuliwa bila huruma.
Alisogea eneo hilo akiwasihi washambuliaji waache kuwapiga na akajitolea kufidia vifaa vilivyodaiwa kuibiwa ambapo warufani walidai Sh40,000 ambayo baba huyo aliahidi kuwalipa, na kukimbilia barabara kuu kwa ajili ya msaada unaowezekana wa kukusanya pesa hiyo.
Alidai aliporudi, ni mrufani wa pili pekee aliyebaki wengine walikuwa wamekimbia na kuwa alijaribu kumzuia mrufani huyo kutoendelea kumpiga mwanaye ambapo alitoroka.
Baada ya kugundua hali ya Peter ni mbaya, shahidi wa pili aliomba msaada katika kituo cha polisi kilicho karibu.
Inspekta Adam Mabula alienda naye eneo la tukio na kuwakuta pacha hao wamelala chini. Walipokuwa wakipelekwa Hospitali ya Wilaya ya Mkuranga, Peter alifariki dunia njiani.
Shahidi wa nne, Dk Irene Lyatuu, aliyefanya uchunguzi wa mwili wa marehemu, aligundua jeraha kubwa kichwani, mkono wa kushoto kuvunjika karibu na kiganja, damu kutoka puani na mdomoni, pamoja na nguo zilizotapakaa damu.
Baadaye jioni, shahidi wa sita alirudi kwenye eneo la ujenzi na kufanikiwa kuwakamata warufani wa pili na tatu huku mrufani wa kwanza akikamatwa Machi 28, 2022 akiwa kazini katika eneo hilo.
Kupitia mawakili wao, warufani walitoa hoja kadhaa kupinga hukumu hiyo, moja ya hoja kuu ilikuwa kwamba utambuzi wao ulifanyika kwa njia yenye dosari, hasa katika gwaride la utambuzi lililoandaliwa na polisi.
Walidai kuwa washiriki waliowekwa katika gwaride hilo hawakuwa na umri, urefu na mwonekano unaofanana na watuhumiwa, jambo lililokiuka taratibu za polisi.
Pia, walidai kuwa mashahidi waliwaona watuhumiwa kabla ya kufanyika kwa gwaride la utambuzi, jambo ambalo lingeweza kuathiri uhalali wa utambuzi huo.
Aidha, walipinga ushahidi wa kitabibu uliowasilishwa mahakamani wakidai kuwa fomu ya ripoti ya uchunguzi wa maiti haikutayarishwa kwa kufuata taratibu za kisheria.
Kwa upande mwingine, walidai kuwa mahakama ya awali ilishindwa kutathmini ipasavyo ushahidi uliotolewa na mashahidi mbalimbali.