Tanzania inavyopambana kuwarejesha walionasa Mashariki ya Kati

Dar es Salaam. Serikali ya Tanzania imesema inaendelea kutafuta njia salama za kuwasaidia Watanzania wengine waliopo ukanda wa Mashariki ya Kati kurejea nyumbani, kufuatia hali ya usalama inayoendelea kuwa tete katika baadhi ya mataifa ya eneo hilo.

Kuzorota kwa hali ya usalama katika eneo hilo kunatokana na mapigano baina ya Iran dhidi ya Israel na Marekani yanayoingia siku ya 12 ambayo yamesababisha vifo, majeruhi, uharibifu wa mali kuhatarisha ongezeko la gharama za maisha duniani kwa bei ya mafuta kupanda.

Miongoni mwa waliofariki dunia kwenye mapigano hayo ni ya Kiongozi Mkuu Iran, Ayatollah Ali Khamenei. Irani yenyewe imekuwa ikijibu mapigo kwa kuishambulia Israel na baadhi ya washirika wa karibu wa Marekani kama UEA, Qatar, Bahrain, Kuwait, Jordan, Saudi Arabia, Oman, Iraq na Syria.

Baadhi ya mataifa hayo yamesitisha safari za ndege.

Kauli ya Tanzania imekuja siku moja baada ya Watanzania 236 waliokuwa wamekwama katika miji ya Dubai na Abu Dhabi huko Falme za Kiarabu (UAE) kurejeshwa nchini Tanzania jana kwa ndege maalumu iliyotumwa na Serikali.

Leo Jumanne Machi 10, 2026, Mwananchi limemtafuta Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa kujua hatua inazochukua kwa raia wake hao waliopo huko kurejea nyumbani ambapo amesema, Serikali inaendelea na tathmini ili kuona uwezekano wa kuwasaidia wengine waliobaki katika ukanda huo.

Amesema changamoto kubwa inayokwamisha juhudi hizo ni kufungwa kwa baadhi ya viwanja vya ndege katika mataifa yanayokumbwa na taharuki ya kiusalama.

“Tathmini inaendelea, pale tutakapoweza tutatuma. Changamoto iliyopo ni kwamba baadhi ya viwanja vya ndege vimefungwa na lazima upate kibali maalumu.

Hii tuliyofanya ni kwa kibali maalumu lakini kuna nchi nyingine zimefunga kabisa viwanja vyao, hawaruhusu ndege kutua wala kupaa,” amesema.

Jana Jumatatu, ndege maalumu iliyotumwa na Serikali iliwasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) jijini Dar es Salaam ikiwa na Watanzania 236 waliokuwa wamekwama katika mataifa ya Ghuba kutokana na hali ya taharuki ya kiusalama inayoripotiwa katika ukanda wa Mashariki ya Kati.

Waliofika uwanjani hapo walikuwa ni watu waliokuwa wakifanya kazi, biashara, masomo pamoja na shughuli nyingine binafsi katika mataifa hayo kabla ya hali ya usalama kuzorota na kuwalazimu kutafuta namna ya kurejea nyumbani.

Hatua ya kurejeshwa kwao iliibua hisia kali za furaha kwa ndugu na jamaa waliokuwa wakisubiri kujua hatma ya ndugu hao, wengi wakisema walikuwa wakiishi katika hofu kubwa kwa siku kadhaa wakifuatilia taarifa za mashambulizi yanayoripotiwa na vyombo vya habari katika ukanda huo.

Baadhi ya Watanzania waliorejea walisimulia hali ya taharuki waliyoishuhudia, wakieleza katika baadhi ya maeneo kulikuwa na hofu kubwa huku wakazi na wageni wakilazimika kujifungia ndani wakifuatilia taarifa za usalama.

Mmoja wa waliorejea jana, John Bina alisema katika kipindi chote alichokuwa Dubai  kulikuwa na hali ya wasiwasi huku watu wengi wakijifungia majumbani huku viwanja vya ndege vikifungwa.

“Kwa kweli kulikuwa na hofu. Watu walikuwa wanafuatilia habari kila saa kujua kinachoendelea na nini kinaweza kutokea baadaye,” amesema.

Mtanzania mwingine aliyerejea, Princes Mwakatobe amesema hali hiyo imekuwa ikiwaathiri zaidi raia wa kigeni, wanakosa uhakika wa usalama wao huku wengi wakisubiri msaada kutoka katika serikali za nchi zao.

Amesema walipopata taarifa kuwa Serikali ya Tanzania imeandaa mpango wa kuwasaidia kurejea nyumbani walipata faraja kubwa baada ya siku kadhaa za taharuki.

Kwa mujibu wa Serikali, operesheni ya kuwarejesha Watanzania hao ilifanyika kwa ushirikiano wa karibu kati ya mamlaka za Tanzania, balozi na mamlaka za anga za mataifa husika ili kuhakikisha raia hao wanarejea nyumbani salama.