Jamhuri yaomba kufanya mabadiliko kesi ya silaha inayomkabili Mkaguzi wa Polisi

Dar es Salaam. Jamhuri katika kesi kukutwa na silaha inayomkabili, umeiomba Mahakama kufanya mabadiliko ya hati ya mashtaka, kabla ya kuendelea na hatua nyingine.

Maombi hayo yamewasilishwa leo Jumanne, Machi 10, 2026 na wakili wa Serikali Mwandamizi, Theresia Mtao wakati kesi hiyo ilipoitwa kwa ajili ya kutajwa.

Malekela kutoka Kambi ya Polisi Kilwa Road, anakabiliwa na mashtaka manane yakiwemo ya kukutwa akimiliki bastola tatu na risasi 26, bila kuwa na leseni katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.

Wakili wa Serikali Mwandamizi, Theresia Mtao ameieleza Mahakama hiyo kuwa upelelezi wa kesi umekamilika, lakini wanaomba tarehe nyingine kwa ajili kufanya mabadiliko ya hati ya mashtaka.

“Mheshimiwa kwa sababu hiyo, tunaomba mahakama itupangie tarehe nyingine ili Jamhuri ifanye mabadiliko kwenye hati ya mashtaka,” amesema.

Mtao ameiomba Mahakama hiyo, mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi, Geofrey Mhini, anayesikiliza kesi hiyo.

Hakimu Mhini alikubali ombi la Jamhuri na kuahirisha hadi Machi 13, 2026 na mshtakiwa yupo nje kwa dhamana.

Kati ya mashtaka hayo manane yanayomkabili Malekela, matatu ni ya kughushi; matatu ni ya kuwasilisha nyaraka za uongo; moja la kukutwa akimiliki silaha tatu na lingine ni la kumiliki risasi bila kuwa na leseni.

Katika shtaka la kughushi, mshtakiwa anadaiwa Juni 20, 2025 eneo lisilojulikana ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa nia ya kudanganya walitengeneza nyaraka ya uongo ambayo ni kibali cha kumiliki silaha chenye jina la Marwan Harbetsh akionyesha kuwa ni kibali halali, wakati akijua kuwa ni uongo.

Shtaka la pili na la tatu, mshtakiwa anadaiwa Oktoba 30, 2024 ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa nia ya kudanganya alitengeneza kibali cha kumiliki silaha chenye jina la Ahmed Sandruddin na Muntaser Harbetsh, akionyesha kuwa ni kibali halali, wakati akijua kuwa ni uongo.

Shtaka la nne, tano na sita ni kuwasilisha nyaraka za uongo, ambapo mshtakiwa anadaiwa Julai 11, 2025 sehemu isiyofahamika ndani ya Jiji la Dar es Salaam, mshtakiwa aliwasilisha nyaraka ya uongo zenye majina ya Marwan Harbeth, Muntaser Harbetsh na Ahmed Sandruddin, kwa kuonyesha kuwa ni kibali halali, wakati akijua kuwa ni uongo.

Iliendelea kudaiwa kuwa katika shtaka la saba, inadaiwa Juni 4, 2025 katika Kambi ya Polisi Kurasini iliyopo wilaya ya Ilala, mshtakiwa alikutwa akiwa na silaha tatu aina ya bastola, bila kuwa na leseni

Silaha hizo ni bastola aina ya CZP yenye namba yenye D108054, bastola aina ya Glock 26 yenye namba XSL 7694 na bastola aina ya Glock 17 yenye namba LXE088, bila kuwa na leseni.

Shtaka la nane, mshtakiwa anadaiwa Juni 4, 2025 eneo hilo la Kambi ya Polisi Kurasini, alikutwa akimiliki risasi 26 za bastola bila kuwa na leseni.