Daraja la Sh9.4 bilioni kuondoa adha kwa wananchi  Magu

Magu. Wananchi wa Wilaya ya Magu mkoani Mwanza, wameeleza adha wanazokumbana nazo wakati wa kuvuka Daraja Sukuma, ikiwamo ya kusombwa na maji nyakati za mvua.

Wamesema daraja hilo ndiyo njia pekee inayowaunganisha wananchi wa Kata ya Vaya na Magu Wilayani, ambalo nyakati za mvua hukata mawasiliano.

Wameyaeleza hayo leo Jumanne, Machi 10, 2026 wakati Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Kenani Kihongosi alipofanya ziara wilayani humo, pamoja na mambo mengine, anakagua miradi ya maendeleo ambayo Serikali imepeleka fedha.

“Kipindi cha nyuma watu walikuwa wakisombwa na maji nyakati za mvua, wengine shindwa kuvuka na kukata mawasiliano ya Vaya na watu wanaokwenda wilayani,” amesema Kalango Nsabi.

Muonekano wa daraja Sukuma wilayani Magu mkoani Mwanza



Mwananchi mwingine, Emmanuel Sabuni, amesema nyakati za mvua ilikuwa changamoto kwao, baadhi walilazimika kuvuka kwa mashaka na hofu, huku baadhi yao wakikumbana na adha ya kusombwa na maji.

“Kuna nyakati mifugo ipo kule (upande wa pili) mvua imenyesha kubwa huwezi kurudi, unabaki huko huko ulipo, wale waliolazimisha wengi wao walisombwa na maji,” amesema.

Mbali na watu, Sabuni amesema hata mifugo na mazao nayo imekuwa ikisombwa na maji nyakati za mvua.

Akikagua maendeleo ya ujenzi wa daraja hilo, Kihongosi ametaka lifunguliwe Aprili ili wananchi wa Magu waanze kulitumia.

Amesema, daraja hilo lililogharimu Sh9.4 bilioni litakuwa suluhu ya kudumu kwa wananchi hao.

Katibu wa NEC, Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Kenani Kihongosi akizungumza baada ya kukagua daraja Sukuma, Magu.



Akisoma taarifa ya utekelezaji wa ujenzi huo, Meneja wa Wakala wa Barabara Tanzania, (Tanroads) Mkoa wa Mwanza, Ambrose Pascal, amesema daraja hilo la urefu wa mita 70 na ujenzi umefikia asilimia 80.

Amesema miongoni mwa kazi zilizofanyika ni ujenzi wa nguzo za katikati (Piers), kuta za mwanzo (Abutments), nguzo mlalo, Deck Slab na tabaka la changarawe.

Kihongosi ameanza ziara mkoani Mwanza na leo Machi 10, 2026 alipokewa na mamia ya wananchi katika Kijiji cha Masanza Nsola, wilayani Magu na kuwapa salamu za Rais Samia Suluhu Hassan.

Pia, amewashukuru wananchi hao kwa kuchagua wabunge na madiwani wa CCM ambao wote kwa pamoja wanashirikiana na Rais kutekeleza ilani ya chama.

Wilayani Magu, Kihongosi pia alitembelea Shina la chama namba mbili kwenye tawi la Itumbili kabla ya kufanya mkutano wa hadhara katika eneo la Nyangunge.