Mambo 7 yamkalia pabaya Pedro Yanga

YANGA inaendelea kugawa dozi kwenye mechi zake ikitoka kupata mshtuko wa kudondosha pointi mbili baada ya kulazimishwa sare dhidi ya Simba, mchezo ambao uliibua hoja mbalimbali juu ya kiwango cha kikosi hicho.

Huo ulikuwa mchezo wa kwanza wa dabi timu hiyo ikiwa chini ya Kocha Pedro Goncalves tangu aanze kazi ya kukifundisha kikosi hicho kutoka kwa Romain Folz ambaye naye licha ya kuifundisha Yanga kwa muda mfupi lakini alionja utamu wa kushinda mchezo huo mkubwa.

Kufanya kazi kwenye klabu kubwa za Simba na Yanga presha ni kitu cha kawaida na hulka ya mashabiki na hata viongozi wake wanatamani kila wakati kuona timu zao zinafanya vizuri, zikicheza mpira mzuri na kushinda kwa matokeo mazuri.

Baada ya Yanga kutolewa Ligi ya Mabingwa Afrika ikiishia hatua ya makundi, pia kuja kupata sare dhidi ya Simba iliyokuwa inajipigia kwa michezo sita mfululizo iliyopita kuna maneno ya chinichini yameanza kuzunguka juu ya mustakabali wa Pedro, baadhi ya mashabiki na hata viongozi kuanza kuweka mashaka ya uwezo wa kocha huyo raia wa Ureno.

Hata hivyo, Pedro bado hana mashaka sana kwa kuwa timu inaendelea kushinda lakini hebu tuangalie mambo ambayo yanaweza kumtibulia wakati wowote kocha huyo na yakitokea makosa ya kupata sare tena au kupoteza nafasi yake inaweza kuwa kwenye wakati mgumu.

Pedro alisajili wachezaji wawili wa kigeni wa kwanza ni mshambuliaji Laurindo Aurelio ‘Depu’ ambaye hakuna shaka uwezo wake umewakosha wengi akiwa ameshapachika mabao tisa kwenye mashindano yote na asisti moja lakini shida ipo hapa kwa winga Buba Jamell.

Buba ambaye ameshafunga mabao mawili bado uwezo wake haujawateka wengi ndani ya klabu hiyo wakiona kama anaonyesha kitu cha kawaida sana tofauti na walivyotarajia kabla ya ujio wake katika kikosi hicho.

Bahati mbaya sana Buba hakucheza kwa takribani miezi miwili kabla ya kuja Yanga na anahitaji muda kujiimarisha lakini kama atashindwa kuonyesha kiwango, presha kubwa itakuwa kwa aliyemleta Pedro.


Yanga kama unavyoona ikiwa chini ya Pedro imeshacheza jumla ya mechi 17 za mashindano yote, ikishinda 12 ikitoa sare tatu na kupoteza mbili zote kwenye Ligi ya mabingwa Afrika ikiwa inaongoza msimamo wa ligi ambako haijapoteza mchezo wowote.

Takwimu hizo ni bora kabisa kwa Pedro lakini kuna baadhi ya mashabiki matarajio yao yamekuwa tofauti, bado hawakubali sana kiwango cha timu yao wakiona kama sawa wanapata matokeo mazuri lakini namna kikosi chao kinavyocheza hakiwapi raha sana.

Mashabiki hao wanataka kuona Yanga inatawala vizuri zaidi mechi zake ikiupiga mwingi na kushinda hilo kwao halijatimia sana kwa timu yao ikiwa chini ya Pedro wakianzisha kelele taratibu kama zile ambazo zilianza kwa kocha aliyepita Folz na baadaye kutimuliwa.

Yanga mpaka sasa ina wachezaji watatu muhimu, akianza mshambuliaji Clement Mzize ambaye ameumia tena licha ya hivi karibuni kuonyesha anaweza kurejea na sasa sio rahisi tena kuonekana uwanjani msimu huu.

Beki na nahodha msaidizi Dickson Job naye ameingia wodi hii ya wagonjwa wa muda mrefu akiwa ameumia goti na hivi unavyosoma yupo nchini Afrika Kusini kwa matibabu ya upasuaji naye anaweza asirejee tena msimu huu.

Kiungo Pacome Zouzoua naye yupo hapa ambaye aliumia bega lake kwenye mchezo wa mwisho wa makundi ligi ya mabingwa ingawa inaelezwa anaweza kurejea haraka, kumbuka hawa wote ni wachezaji muhimu sana kukosekana kwao ni pigo kwa Pedro.


Bahati mbaya kidogo Pedro anafika Yanga wakati mtani wao Simba akiwa ameimarika baada ya kujisuka upya kwa haraka, hili nalo sio zuri kwa kocha huyo kwani namna timu hizo mbili zilivyokutana wiki iliyopita huku wekundu hao wakionekana walicheza vizuri kuliko kikosi chake inaweza kuwa habari mbaya kwake itakayomwongezea presha.

Simba kupata sare mbele ya Yanga itaongeza morali kwa wekundu hao kuona inawezekana wakawashika wababe wao hao na hata mchezo ujao baina ya timu hizo kama Pedro akiwa bado yupo timu hiyo kisha wapinzani wake wakapata matokeo mazuri inaweza kuwa shida kubwa kwake.

Kuna wakati makocha wanaweza kupoteza nafasi zao kutokana na presha ya wachezaji wao ambao wanaweza kuwa hawakubaliani na baadhi ya mambo na kocha wao, Pedro anatakiwa kuhakikisha eneo hili anaendelea kuwa salama ili wachezaji wake wasichochee moto mkali kwake.

Pedro aliishia hatua ya makundi wakati mashabiki na viongozi wake walikuwa wanatamani sana kuona timu yao inatinga robo fainali, Yanga wanaweza kulinyamazia hilo la kutolewa kwa shingo upande lakini lisizuke lolote baya litaamsha kivuli hicho cha matokeo ya kukwama kimataifa.


Kelele nyingine zinazopigwa chichini ni namna Yanga inavyopata wakati mgumu kupata matokeo mazuri kwenye mechi kubwa ikianzia zile mbili dhidi ya Al Ahly na ilishindwa kuulinda ushindi baada ya kuwa inaongoza kwa bao 1-0 likarudi.

Kule Morocco ilikuwa ni kama ilishapata sare lakini dakika za mwisho ikaaruhusu bao lilokuja kuamua mchezo na hata ilivyocheza ugenini dhidi ya JS Kabylie ikapata sare wakati wengine wakiona kama wangeweza kushinda.

Wadau wa klabu hiyo wanaona kama kocha huyo anahusudu sana mbinu za kujilinda kwa timu yake kukaa nyuma kiasi ingawa mwenyewe amekuwa akipingana na hoja hii akidai Yanga huwa inashambulia na siyo kujilinda, kama ikitokea mechi kubwa zinazokuja kikosi hicho kikashindwa kupata ushindi itaongeza presha kwa Pedro.


Pedro anatakiwa kuwa makini na haya kabla ya muda kuamua hatma yake anaweza wakati wowote haya yakamletea presha ngumu ndani ya Yanga, tumtakie kila la kheri akikwepe kikombe hicho kibaya.