Mechi za mtego Ligi Kuu, Barker abadili mbinu

LEO Jumatano, macho na masikio ya mashabiki wa soka hapa nchini yataelekezwa Mtipa mkoani Singida ambako kutakuwa na moja ya mechi ya kusisimua ya Ligi Kuu Bara kati ya wenyeji, Singida Black Stars dhidi ya Simba.

Hii itakuwa mechi ya pili ya ligi kuchezwa leo ikitarajiwa kupigwa saa 10:00 jioni baada ya kutanguliwa na mechi ya mapema saa 8:00 mchana kati ya TRA United dhidi ya Namungo ikayochezwa Arusha, huku mechi ya mwisho ikiwa saa 1:15 usiku kati ya Dodoma Jiji dhidi ya Azam FC.

Ukiziangalia kwa umakini mkubwa, mechi zote hizo zimekaa kimtego kwani zinakutana timu zinazopishana kidogo kwa pointi, lakini pia zimekuwa na matokeo mazuri siku za karibuni. Hali hiyo inafanya kila mechi kuwa na ushindani wake.

Simba inaingia katika mechi hii ikiwa na historia nzuri dhidi ya Singida Black Stars katika ligi tangu timu hiyo ikiitwa Ihefu, takwimu zinaonyesha Simba haijawahi kupoteza mbele ya walima alizeti hao.

Katika mechi nane za ligi kati ya timu hizi mbili, Simba imeshinda mara saba huku mechi moja tu ikiisha kwa sare. Singida Black Stars bado haijapata ushindi katika mfululizo huu wa ligi.

Licha ya kuwa rekodi hiyo nzuri katika ligi, Simba ina kumbukumbu ya kuchapwa 3-1 na Singida Black Stars, ikatupwa nje ya Kombe la Shirikisho la CRDB msimu uliopita 2024-2025 hatua ya nusu fainali, wakati huo timu ikiwa chini ya kocha Fadlu Davids ambaye kwa sasa anainoa Raja Casablanca ya Morocco.

Kwa upande wa mabao, Simba imefunga 14 katika mechi hizo nane za ligi huku Singida Black Stars ikifunga matatu pekee. Hii inaonyesha uimara wa safu ya ushambuliaji ya Simba pamoja na ulinzi.

Pamoja na kwamba Simba ilishinda mechi zote mbili msimu uliopita kwa bao 1-0, nyumbani na ugenini, imekuwa na wastani wa kufunga mabao 2.1 huku mechi baina yao zikiwa na mabao chini ya manne.

Timu hizi zinakutana wakati wote katika mechi zao za mwisho za ligi zikitoka kucheza dhidi ya Yanga kwa vipindi tofauti, ilianza Simba Machi Mosi 2026 huko Zanzibar kwa kutoka suluhu huku Singida BS siku nne baadaye, Machi 5 ikichapwa nyumbani kwa mabao 3-0.

NO MWALIMU, NO SOWAH, KUNA HUYU

Baada ya sekeseka la Jonathan Sowah ambalo lilitokea kabla ya Dabi ya Kariakoo, Kocha wa Simba, Steve Barker alikuwa na mpango maalum mwenyewe ameupa jina X kuhakikisha anaongeza kitu kwenye safu yake ya ushambuliaji.

Ikumbukwe kuwa, Simba iliachana na washambuliaji wake wawili, Kibu Denis na Steven Mukwala kwa kuwauza Al Nasr Benghazi ya Libya, hivyo ilimbidi kumjenga Inno Jospin Loemba ambaye ni kiungo na kumtumia katika eneo hilo na makali yake yalionekana katika dabi.

Hivyo kufungiwa mechi tatu kwa Seleman Mwalimu kwa kosa la kumpiga kiwiko kwa makusudi mchezaji Andy Lobulka Bikoko wa Dodoma Jiji, kutamfanya kocha huyo kuendelea kuhitaji zaidi huduma ya Mkongomani huyo.

“Kuna wakati inabidi mchezaji awe tayari kubeba majukumu ya timu hata ikibidi kutumika katika nafasi nyingine kwa sababu ndani ya msimu huwa kuna mambo mengi ikiwemo suala la majeruhi, nafurahi kuwa na wachezaji wa aina hiyo,” alisema Barker.

Mbali na Loemba, Simba inajivunia kuwa na mawinga wenye kasi na nguvu, Libasse Guaye na Anicet Alain Oura ambao wanaweza kuwaweka katika wakati mgumu mabeki wa Singida BS huku katika eneo la ubunifu nyuma ya mshambuliaji wa mwisho wakiwa na Clatous Chama.

Nyota wawili wa Singida BS, Khalid Aucho na kipa, Amas Obasogie ambao awali walisimamishwa, wamerejea kundini na wanatarajiwa kuwa sehemu ya mechi ya leo baada ya kukosekana katika mechi iliyopita ya ligi dhidi ya Yanga.

Aucho alisimamishwa kwa utovu wa nidhamu huku Amas ikiwa kwa shutuma za upangaji wa matokeo ambazo hata hivyo zilitupiliwa mbali kufuatia kukosekana kwa ushahidi baada ya uchunguzi kufanyika.

Akizungumzia urejeo wa wachezaji hao na ugumu wa mechi ya leo, meneja mkuu wa Singida BS, Othmen Najjar alisema: “Ni wachezaji muhimu kwenye kikosi chetu, lakini tutaona katika mazoezi ya mwisho leo (jana) kabla ya kufanya uamuzi wa mwisho nani anatakiwa kuwa sehemu ya mchezo huo. Hii ni mechi nyingine ngumu na kubwa, kuna mambo ambayo tumeyafanyia kazi ili kuwa bora tofauti na ilivyokuwa dhidi ya Yanga.”

Licha ya kuwa miongoni mwa timu sita za juu katika msimamo wa ligi, Namungo haijashinda katika mechi tano zilizopita, imeambulia sare mbili tu dhidi ya Singida BS na Mtibwa Sugar, imepoteza tatu dhidi ya Yanga kwa bao 1-0, Tanzania Prisons kwa mabao 3-2 na Pamba Jiji kwa bao 1-0.

Vijana hao wa Juma Mgunda, watakuwa na kibarua kingine leo cha kukabiliana na TRA United ambayo imetoka kuifunga Fountain Gate bao 1-0. Hii ni mechi ngumu kwa timu zote mbili kulingana na viwango vyao.

TRA ambayo ipo nafasi ya 11 ikiwa na pointi 16, itahitaji ushindi ili kuwa mbali na kundi ambalo lipo kwenye hatari ya kushuka daraja, kwa Namungo ambayo ipo nafasi ya sita ikiwa na pointi 21, itahitaji kuisogelea nne bora ambayo ipo umbali wa pointi tatu kuifikia kutoka sasa.

Mechi kati ya Dodoma Jiji dhidi ya Azam inatarajiwa kuwa na ushindani mkubwa kutokana na mwenendo mzuri wa timu zote mbili katika mechi tano zilizopita. Timu hizi zinaingia katika mechi hii zikiwa na matokeo chanya katika mechi hizo, jambo linaloongeza uzito wa pambano hilo.

Dodoma Jiji imeonyesha uimara mkubwa katika mechi hizo, timu hiyo imeshinda mara tatu na kutoka sare mara mbili bila kupoteza hata moja. Ushindi dhidi ya TRA United, KMC na JKT Tanzania pamoja na sare dhidi ya Simba na Mbeya City.

Kwa upande wa Azam FC, imekuwa katika kiwango kizuri pia. Katika mechi tano zilizopita imeshinda tatu na kutoka sare mara mbili. Ushindi ni dhidi ya Mtibwa Sugar, KMC na TRA United.

Tofauti ndogo kati ya timu hizi inaonekana katika idadi ya mabao yaliyofungwa, ambapo Azam imeonyesha makali zaidi katika ushambuliaji kwa kufunga jumla ya mabao tisa katika mechi hizo ikiruhusu mawili.

Hata hivyo, Dodoma Jiji yenye mabao saba imekuwa na nidhamu nzuri ya mchezo na uwezo wa kudhibiti wapinzani wao nao wakiruhusu mabao mawili, jambo linaloweza kufanya mechi hii kuwa ngumu kutabirika.