Morogoro. Wakati dunia ikiendelea kuadhimisha Siku ya Wanawake Duniani, inayoadhimishwa kila mwaka ifikapo Machi 8, simulizi ya Abra Kingologo inaibua tafakuri mpya kuhusu maana halisi ya ujasiri, ndoto na thamani ya kazi.
Akiwa na umri wa miaka 23 na mhitimu wa Chuo Kikuu cha Mzumbe, Abra amechagua njia ambayo wengi hawakuitarajia ya kuweka pembeni vyeti vyake na kushika usukani wa mashine nzito za kilimo, akiamini kazi ni kazi ilimradi inamwezesha mtu kujipatia riziki halali.
Mwananchi imefanya naye mahojiano na kueleza kwamba, baada ya kuhitimu Shahada ya Menejimenti ya Uhandisi wa Viwanda mwaka 2025, alijiunga na maelfu ya vijana walioko katika harakati za kutafuta ajira.
Anasema kwa miezi kadhaa alizunguka huku na kule akiwasilisha maombi ya kazi, akitumaini siku moja ndoto yake ingetimia, lakini juhudi hizo hazikuzaa matunda.
Anasema ndipo Januari mwaka huu, alipochukua uamuzi uliobadili kabisa mwelekeo wa maisha yake.
Alijiunga na Chuo cha Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (Veta) Kihonda na kuanza kusoma kozi fupi ya ufundi na uendeshaji wa mashine na mitambo ya kilimo.
Miongoni mwa mitambo aliyojifunza kuiendesha ni mashine ya kuvunia mpunga maarufu ‘Combine harvester’ pamoja na mashine nyingine za kisasa zinazotumika katika shughuli za kilimo.
Abra anasema safari yake ya elimu ilianza katika Shule ya Msingi Katulukila, alikomaliza masomo ya msingi na baadaye kuchaguliwa kujiunga na Shule ya Sekondari Mwanihana iliyopo Wilaya ya Kilombero.
Akiwa mwanafunzi mwenye bidii, anasema alifaulu vizuri na kupata nafasi ya kuendelea na elimu ya juu katika Chuo Kikuu cha Mzumbe.
Wakati huo ndoto yake kubwa ilikuwa kuwa mhandisi na mshauri mashuhuri katika masuala ya viwanda.
“Mimi ndiye mtoto wa kwanza kuzaliwa katika familia yetu. Nina wadogo zangu wanasoma shule ya msingi na wengine sekondari. Nimezaliwa na kukulia Wilaya ya Kilombero, wazazi wangu ni wakulima wadogo wa mpunga na mazao mengine ya chakula. Ukweli ni kwamba elimu yangu na maisha yangu inategemea kilimo, hivyo ninakipa thamani kubwa sana,” anasema Abra.
Anasema uzoefu aliouona nyumbani kwao ulimfanya aone umuhimu wa kujifunza matumizi ya mitambo ya kisasa ya kilimo.
Anasema kwa miaka mingi wazazi wake wamekuwa wakilima kwa kutumia jembe la mkono, kuanzia hatua ya kuandaa shamba hadi kuvuna.
Abra anasema njia hiyo imekuwa ikisababisha uchovu mkubwa na wakati mwingine upotevu wa mazao hasa wakati wa mavuno.
“Pamoja na kwamba ndoto yangu ni kuwa mhandisi mkubwa kwenye masuala ya viwanda, bado ninatamani kuwa mkulima mkubwa wa mpunga. Kujifunza kuendesha mtambo wa kuvunia mpunga kumetokana na ugumu wa kazi ya kilimo tuliyozoea nyumbani. Wazazi wangu wamekuwa wakivuna kwa mkono na wakati mwingine mpunga mwingi hupotea shambani,” anasema Abra.
Anasema maarifa aliyoyapata Veta yanaweza kuwa chachu ya mabadiliko katika familia yake na hata jamii inayomzunguka.
Abra anasema anaamini matumizi ya mashine na mitambo ya kisasa yataongeza uzalishaji wa mpunga na kupunguza kazi ngumu inayowakabili wakulima wengi vijijini.
Binti huyo anasema kwa sasa familia yao huzalisha wastani wa magunia manane ya mpunga kwa hekari moja. Hata hivyo, anaamini kuwa kwa kutumia mitambo ya kisasa, kiwango hicho kinaweza kuongezeka zaidi.
Anasema zaidi ya hapo, ujuzi huo unaweza pia kumfungulia milango ya ajira kwenye mashamba makubwa ya wawekezaji, kwa kuwa mashine ya kuvunia mpunga pia inaweza kutumika kuvuna mazao mengine kama ngano, mtama, uwele na ulezi.
Tangu akiwa mdogo, Abra anasema amekuwa na hulka ya kupenda kufanya mambo ambayo mara nyingi huonekana ya kiume katika jamii nyingi.
Anasema anapenda kuendesha vyombo mbalimbali vya moto kama pikipiki na magari na sasa ameongeza ujuzi mpya wa kuendesha mashine ya kuvunia mpunga pamoja na trekta.
Hata hivyo, safari hiyo haijakosa changamoto, anasema katika kijiji anachotoka, baadhi ya watu wamekuwa wakimchukulia kama msichana wa ajabu baada ya kuona ameacha vyeti vya chuo kikuu na kuamua kujifunza uendeshaji wa mitambo ya kilimo.
Anasema wapo pia wanaomwona kama msichana mbabe au mwenye tabia zinazodhaniwa kuwa za kiume.
“Pamoja na maneno hayo, sikuvunjika moyo. Niliendelea kujifunza kozi hii ya mwezi mmoja na bado natamani kujifunza zaidi kuhusu mitambo mingine. Napenda kufanya kazi ngumu na zinazohitaji akili na ujuzi mkubwa, hata kama wengine wanaona hazifai kwa wanawake,” anasema.
Licha ya mitazamo tofauti ya baadhi ya watu, Abra anasema amepata msaada mkubwa kutoka kwa familia yake. Wazazi wake pamoja na bibi yake walimuunga mkono tangu mwanzo na walikubali kumsaidia kugharamia mahitaji yaliyohitajika wakati wa mafunzo yake.
Anatumia nafasi hiyo pia kuishukuru Serikali pamoja na wadau mbalimbali waliowezesha vijana kupata mafunzo ya ufundi kupitia vyuo vya Veta.
Anasema fursa hiyo ilitolewa kupitia Shirika la Agra, lililosaidia vijana wengi kupata ujuzi wa vitendo unaohitajika katika sekta ya kilimo.
“Fursa hii ilinipata wakati nilikuwa na uhitaji mkubwa wa kujifunza ujuzi mpya. Niliichangamkia na sasa nimehitimu nikiwa na uwezo wa kuendesha mitambo na mashine mbalimbali za kilimo,” anasema.
Baada ya kuhitimu mafunzo hayo, mpango wake ni kurejea kijijini kwao na kuanza kufanya kilimo cha kisasa kwa kutumia mashine na mitambo ya kilimo.
Anasema anaamini wakulima wengi vijijini hawatumii mashine si kwa sababu tu ya ukosefu wa uwezo, bali pia kwa sababu hawajui faida zake.
“Wakulima wengi hawajui faida ya kutumia mashine. Mimi nitaanza kutumia mashine na mitambo hata kama ni kwa kukodi. Kwa kuwa najua kuziendesha, nitaendesha mwenyewe na hivyo kupunguza gharama za uzalishaji,” anasema.
Katika hatua nyingine, Abra anaiomba Serikali na wadau mbalimbali kumsaidia kupata mashine na mitambo ya kilimo ili aweze kujiajiri au kupata nafasi ya kufanya kazi kwenye mashamba makubwa ya ngano au mpunga.
Anasema ujuzi wake hauishii kwenye uendeshaji wa mashine pekee, bali pia anajua kufanya matengenezo pale zinapoharibika.
Kupitia Mradi wa Ujasiriamali wa Vijana kwa Mustakabali wa Chakula na Kilimo (YEFFA), Abra ni miongoni mwa vijana 5,631 waliolengwa kupata ujuzi wa kutumia teknolojia na zana za kisasa za kilimo.
Mradi huo ulizinduliwa Machi 5, 2026 mkoani Morogoro na Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Wanu Hafidh Ameir na unatekelezwa na Veta kwa ufadhili wa Shirika la Agra.