Rais wa Shirikisho la Soka Kongo Afungwa Jela Maisha kwa Kashfa ya Fedha

shemeliezer shem
March 11, 2026
0 Comments

Jean-Guy Blaise Mayolas, Aliyekua Rais wa Shirikisho la soka Kongo Brazzaville (Kushoto), Gianni Infantino rais wa Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA)

Mahakama nchini Kongo Brazzaville imemkuta na hatia Rais wa Shirikisho la Soka la nchi hiyo, Jean-Guy Blaise Mayolas, kwa makosa makubwa ya kifedha yaliyohusisha utakatishaji fedha, ubadhirifu wa mali za taasisi na kughushi pamoja na kutumia nyaraka bandia.

Kwa mujibu wa uamuzi wa mahakama, Mayolas alihusika katika mtandao wa matumizi mabaya ya fedha za shirikisho unaokadiriwa kufikia takribani dola za Marekani milioni 1.7, sawa na zaidi ya shilingi za Tanzania bilioni 4.4. Baada ya kusikiliza ushahidi na vielelezo vilivyowasilishwa, mahakama iliamua kumtia hatiani na kumpa adhabu ya kifungo cha maisha jela.

Timu ya Taifa ya Soka la Kongo Brazzaville

Katika kesi hiyo hiyo, viongozi wengine wawili wa juu wa shirikisho la soka la nchi hiyo pia walikutwa na hatia. Katibu Mkuu Badji Mombo Wantete pamoja na Mweka Hazina Raoul Kanda walihukumiwa kifungo cha miaka mitano jela kila mmoja kwa kuhusika katika ubadhirifu na usimamizi mbaya wa fedha za shirikisho.

Uamuzi huo umeibua mjadala mkubwa katika sekta ya michezo nchini humo, huku wadau wa soka wakisisitiza umuhimu wa uwazi na uwajibikaji katika usimamizi wa fedha za mashirikisho ya michezo barani Afrika.