Mbinu mpya uingizaji wa mihadarati zinatia hofu

Biashara haramu ya dawa za kulevya inaendelea kubadilika kadiri mamlaka zinavyoimarisha udhibiti wake. Hivi sasa, wafanyabiashara wa dawa hizo wamebuni mbinu mpya ya kuziingiza Zanzibar, hali inayoongeza wasiwasi kuhusu usalama wa jamii, hususan watoto na vijana. Mbinu hii mpya imeibuka baada ya njia nyingi zilizokuwa zikitumiwa kwa muda mrefu, zikiwemo kuzimeza na kuzibeba tumboni, kugundulika na kudhibitiwa na vyombo vya dola.

Katika msako maalum uliofanyika mwishoni mwa mwezi uliopita mjini Unguja pamoja na katika vijiji vinavyotembelewa sana na watalii vya Paje na Jambiani, kusini mwa Unguja, kilo 7.5 za dawa za kulevya zilinaswa katika maduka na maghala mbalimbali. Uchunguzi wa awali ulionyesha kuwa dawa hizo, zikiwemo kokeini na bangi, zilifichwa ndani ya vyakula kama biskuti, chokoleti na korosho. Ugunduzi huo umeibua taharuki kubwa kwa sababu vyakula hivyo ni miongoni mwa vinavyopendwa na watoto, na hivyo vinaweza kuliwa bila mtu kufahamu kuwa vina dawa za kulevya hatari.

Hatari ya mbinu hii ni kubwa zaidi kuliko njia zilizotumika hapo awali. Kuweka dawa za kulevya ndani ya vyakula kunafungua uwezekano wa watu wengi, wakiwemo watoto, kutumia dawa hizo bila kujua, jambo ambalo linaweza kuathiri vibaya afya zao na hata kusababisha vifo. Hali hii inaonesha namna wafanyabiashara hao wanavyoweza kubuni njia mpya kila mara ili kukwepa udhibiti wa vyombo vya dola.

Kwa mujibu wa Kamishna wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya Zanzibar (DCEA), Kanali Burhani Zuberi Nassor, uchunguzi bado unaendelea ili kubaini njia halisi iliyotumika kuingiza dawa hizo. Hata hivyo, taarifa za awali zinaonesha kuwa huenda zilisafirishwa kupitia baadhi ya nchi jirani, zikiwemo Malawi na mataifa mengine ya Afrika Mashariki.

Kufuatia tukio hilo, watu watatu wamefunguliwa mashitaka wakituhumiwa kuhusika na uhalifu huo. Miongoni mwao ni raia mmoja wa Romania na Watanzania wawili.

Serikali pia imechukua hatua ya kukamata magari matatu na pikipiki sita zinazodhaniwa kutumika kusafirisha vyakula hivyo vilivyotiwa dawa za kulevya.

Licha ya hatua hizo, bado yapo maswali mengi yanayohitaji majibu ya kina. Wananchi wanahitaji kufahamu ni nani hasa waliagiza bidhaa hizo kutoka nje ya nchi na zilipitia wapi kabla ya kuingia Zanzibar. Ikiwa kweli zilitoka Malawi, ina maana zilipitia vituo mbalimbali vya ukaguzi wa forodha na usalama kabla ya kufika katika maghala na maduka yaliyopatikana nazo.

Hali hii inazua shaka kuhusu uimara wa mifumo ya ukaguzi wa bidhaa zinazoingia nchini. Ikiwa dawa hizo ziliingia kupitia njia halali za biashara, ni muhimu kufahamu kama zilifanyiwa ukaguzi wa ubora na usalama. Zaidi ya hapo, ni nani aliyeruhusu ziingizwe na kuuzwa kama bidhaa salama kwa matumizi ya binadamu.

Uzoefu unaonesha kuwa biashara ya dawa za kulevya mara nyingi huendeshwa na mitandao mikubwa ya kihalifu. Watu wanaokamatwa mara nyingi huwa ni sehemu ndogo tu ya mtandao huo, huku wahusika wakuu wakibaki nyuma ya pazia. Ndiyo maana kuna hofu kuwa watuhumiwa waliokamatwa huenda wakawa ni “vidagaa”, wakati “mapapa” halisi wanaendelea kufaidika na biashara hiyo hatari.

Pia kuna haja ya kuwepo uwazi zaidi kuhusu mwenendo wa kesi zinazohusiana na dawa za kulevya. Kumekuwa na matukio kadhaa yaliyowahi kuripotiwa huko nyuma, lakini wananchi wengi hawajui yaliishia wapi. Kutokuwepo kwa taarifa wazi kuhusu matokeo ya kesi hizo kunachangia kuibua minong’ono na mashaka katika jamii.

Wakati mwingine hali hiyo husababisha baadhi ya watu kuamini kuwa operesheni za kukamata watuhumiwa zinaishia kuwa za muda mfupi tu bila matokeo ya kudumu. Ili kuondoa dhana hiyo, ni muhimu mamlaka husika kutoa taarifa za wazi kuhusu hatua zinazochukuliwa dhidi ya wahusika na hukumu zinazotolewa mahakamani.

Ni ukweli usiopingika kwamba matumizi ya dawa za kulevya yameathiri kwa kiasi kikubwa jamii ya Zanzibar. Familia nyingi zimepoteza vijana wao kutokana na uraibu, huku athari zake zikigusa pia uchumi na ustawi wa jamii kwa ujumla.

Hata hivyo, katika miezi ya hivi karibuni kulikuwa na dalili za matumaini kwamba tatizo hilo linaanza kupungua kutokana na juhudi za vyombo vya dola pamoja na kuimarishwa kwa elimu ya jamii kuhusu madhara ya dawa hizo.

Ugunduzi wa mbinu hii mpya ya kuficha dawa za kulevya ndani ya vyakula unaonesha kuwa vita dhidi ya biashara hiyo bado ni ndefu na inahitaji umakini zaidi. Mbinu hiyo ni tishio kubwa kwa sababu inalenga hata bidhaa zinazotumiwa na watoto.

Kwa sababu hiyo, hakuna sababu ya kulichukulia suala hili kwa mzaha. Watu wanaojihusisha na kuingiza, kusambaza na kuuza dawa za kulevya wanahatarisha maisha ya wananchi kwa makusudi, na hivyo hawapaswi kuonewa huruma.

Wakati huohuo, kuna umuhimu wa kuangalia upya sheria zinazodhibiti dawa za kulevya ili kuhakikisha zinakuwa kali na zenye uwezo wa kuzuia uhalifu huo. Adhabu kali na utekelezaji madhubuti wa sheria vinaweza kuwa sehemu muhimu ya kuzuia watu kujiingiza katika biashara hiyo hatari.

Hata hivyo, jukumu la kupambana na dawa za kulevya haliishii kwa vyombo vya dola pekee. Wananchi pia wanapaswa kushiriki kikamilifu kwa kutoa taarifa na kushirikiana na mamlaka pale wanapobaini dalili zozote za biashara hiyo.

Kwa kufanya hivyo, jamii inaweza kusaidia kufunga mianya inayotumiwa na wafanyabiashara wa dawa za kulevya na kulinda mustakabali wa kizazi kijacho. Vita dhidi ya dawa za kulevya ni jukumu la pamoja, na mafanikio yake yanategemea ushirikiano wa kila mmoja katika jamii.