Leo zimetimia siku 12 tangu kuanza kwa mashambulizi ya anga Mashariki ya Kati, baada ya Marekani na Israel kuishambulia Iran, taifa la Kiislamu lenye utajiri wa mafuta katika ukanda huo.
Mashambulizi hayo yalianza Februari 28, 2026, pale Kiongozi Mkuu wa Iran, Ayatollah Ali Khamenei alipoteza maisha siku hiyo sambamba na viongozi wengine waandamizi Zaidi ya 40 wakiwemo maofisa wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC).
Katika kipindi hicho, mambo mengi yametokea si tu katika ukanda wa mashariki ya kati, bali kwa ulimwengu mzima kwa sababu athari za vita hiyo ipo dhahiri kila sehemu kutokana na kutegemeana katika mnyororo wa usambazaji.
Mbali na vifo vya watu katika nchi za Iran, Israel, Lebanon na Marekani ambazo zinashiriki mapigano moja kwa moja, nchi nyingine za jirani kama Saudi Arabia, Falme za Kiarabu (UAE), Bahrain, Kuwait, Uturuki, Syria na Oman, pia, zimeathirika kutokana na mashambulizi ya Iran.
Kama inavyofahamika, mashariki ya kati ni eneo lenye utajiri mkubwa wa mafuta, likichangia asilimia 20 ya mafuta kwenye soko la dunia. Vilevile, Mlango wa Bahari wa Hormuz ni eneo muhimu katika usambazaji wa mafuta.
Hata hivyo, usafirishaji wa mafuta yanayopita katika mlango huo umesitishwa kutokana na sababu za kiusalama kwa kuwa Iran imekuwa ikizilenga meli za mafuta za Marekani na washirika wake, jambo lililosababisha bei ya mafuta kupanda.
Ndani ya siku hizo 12, Mwananchi linaangazia masuala makubwa yaliyojitokeza huku mashambulizi hayo yakichukua sura mpya kila siku na muda maalumu wa kusitishwa kwa mapigano hayo bado haujulikani.
Huenda vita kati ya Marekani-Israel dhidi ya Iran ikachukua muda mrefu zaidi kutokana na mataifa hayo kueleza kutokuwa tayari kukaa mezani kujadili namna au kusitisha mapigano hayo ili maisha ya kawaida yaendelee.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Abbas Araghchi ameiambia PBS News kwamba kuzungumza au kufanya mazungumzo na Marekani hakuko tena kwenye ajenda zao, baada ya kile alichokiita “uzoefu mchungu sana” wakati wa duru zilizopita za mazungumzo kuhusu nyuklia.
“Walituahidi kwamba hawakuwa na nia yoyote ya kutushambulia, na walitaka kutatua suala la nyuklia la Iran kwa njia ya amani na kupata suluhisho kupitia mazungumzo,” alisema Araghchi.
“Lakini bado waliamua kutushambulia. Sidhani kama suala la kuzungumza na Wamarekani…kwa mara nyingine tena litakuwa kwenye meza ya mazungumzo.”
Hata hivyo, Rais wa Marekani, Donald Trump, naye aliweka msimamo kwamba vita hiyo haitafikia ukomo hadi pale Iran itakapojisalimisha na kukubaliana na matakwa ya Marekani, jambo ambalo Iran imelipuuza.
Juzi, Trump na Rais wa Russia, Vladimir Putin walifanya mazungumzo kwa simu, wakijadili masuala kadhaa ya usalama wa kimataifa ikiwamo juhudi za kumaliza vita vinavyoendelea Mashariki ya Kati, ikizihusisha nchi za Israel na Iran pamoja na vita kati ya Russia na Ukraine.
Kwa mujibu wa Trump, katika mazungumzo hayo, Putin alionyesha nia ya kusaidia mchakato wa kumaliza mapigano kati ya Marekani, Israel na Iran. Hata hivyo, kiongozi huyo wa Marekani alisema: “nimemwambia anaweza kusaidia zaidi kwa kumaliza vita kati ya Russia na Ukraine.”
Mojtaba abeba mustakabali
Iran imemtangaza Mojtaba Khamenei kuwa mrithi wa baba yake aliyeuawa, kuwa kiongozi mkuu, hatua inayoashiria kuwa viongozi wenye msimamo mkali bado wanadhibiti mamlaka kwa nguvu na inaonekana kufunga njia yoyote ya kumaliza haraka vita vya mashariki ya kati.
Matarajio kwamba usumbufu wa usambazaji wa nishati duniani, ambao tayari ni miongoni mwa mikubwa zaidi katika historia unaweza kudumu kwa muda mrefu zaidi kuliko ilivyotarajiwa, yamesababisha bei ya mafuta kupanda kwa kasi kubwa na masoko ya hisa duniani kuporomoka.
Mojtaba, mwenye umri wa miaka 56, ni mwanazuoni wa madhehebu ya Shia mwenye msingi wa nguvu ndani ya vyombo vya usalama na himaya yao kubwa ya biashara.
Hata hivyo, ametangazwa licha ya kuwa hakubaliki kwa Rais wa Marekani, Trump, ambaye ameitaka Iran kujisalimisha bila masharti.
Licha ya onyo la Trump, Iran imeendelea kuonyesha msimamo wa kutokubali kushinikizwa. Uturuki ilisema mifumo ya ulinzi wa anga ya Nato ilidungua kombora la balistiki lililorushwa kutoka Iran na kuingia katika anga ya nchi hiyo, tukio la pili la aina hiyo tangu vita vianze.
Vyombo vya habari vya serikali ya Iran vilionyesha makundi ya watu katika mitaa ya miji kadhaa wakionyesha kumuunga mkono kiongozi mpya, wakiwa wamebeba bendera za Iran na picha za baba yake, Ali Khamenei, aliyeuawa na mashambulizi ya anga siku ya kwanza ya vita.
Katika mji wa Isfahan, televisheni ya serikali iliripoti kusikika kwa milipuko karibu na eneo hilo kutokana na mashambulizi ya anga yanayodhaniwa kufanyika, wakati wafuasi walipokusanyika katika uwanja wa Imam Square, wakipiga kelele “Mungu ni Mkuu” chini ya jukwaa lililokuwa na picha za Ali na Mojtaba Khamenei.
Katika mji wa Tehran, mtu aliyekuwa akisoma mashairi ya maombolezo alisikika akiimba: “Ama kifo au Khamenei, damu yetu inaongoza kuelekea peponi.”
Wanasiasa na taasisi mbalimbali pia walitoa ahadi za utii kwa kiongozi mpya mkuu. “Tutamtii kamanda mkuu hadi tone la mwisho la damu yetu,” ilisema taarifa ya baraza la ulinzi.
Wairani waliozungumza kwa simu walionyesha mitazamo iliyogawanyika: wafuasi wa serikali walipongeza uteuzi huo kama ishara ya ujasiri dhidi ya maadui huku wapinzani wakihofia kwamba utaondoa matumaini yao ya mabadiliko.
“Nina furaha sana kwamba yeye ndiye kiongozi wetu mpya. Ni kama kofi kwa maadui wetu waliodhani mfumo utaanguka baada ya kuuawa kwa baba yake. Njia ya kiongozi wetu marehemu itaendelea,” alisema mwanafunzi wa chuo kikuu, Zahra Mirbagheri, mwenye umri wa miaka 21 kutoka Tehran.
Wairani wengi walikuwa wamesherehekea kifo cha Khamenei, wiki chache baada ya vikosi vyake vya usalama kuua maelfu ya waandamanaji wanaopinga serikali katika machafuko makubwa zaidi ya ndani tangu enzi ya Mapinduzi ya Irani.
Hata hivyo, tangu wakati huo kumekuwa na dalili chache za shughuli za kupinga serikali, huku wanaharakati wakiogopa kuingia mitaani wakati Iran iko chini ya mashambulizi.
“IRGC na mfumo wa serikali bado wana nguvu kubwa. Wana makumi ya maelfu ya wanajeshi walio tayari kupigana ili kuilinda serikali hii. Sisi wananchi hatuna kitu,” alisema Babak, mfanyabiashara mwenye umri wa miaka 34 katika mji wa Arak, ambaye aliomba jina lake la familia lisitajwe.
Bei ya mafuta imepanda na kuvuka Dola za Marekani 100 kwa pipa kufuatia athari za vita kati ya Marekani na Israel dhidi ya Iran.
Mafuta ghafi ambayo ni kipimo cha kimataifa cha bei ya mafuta ghafi, ilipanda kwa zaidi ya asilimia 30 Jumapili iliyopita na kufikia zaidi ya dola 119 kwa pipa, huku hofu ikiongezeka kuhusu uwezekano wa usumbufu wa muda mrefu katika usambazaji wa nishati duniani.
Kupanda huku kulikuwa mara ya kwanza kwa mafuta kuvuka dola 100 kwa pipa tangu Russia ilipoivamia Ukraine mwaka 2022.
Bei ya mafuta ilishuka tena hadi karibu dola 110 kwa pipa baada ya gazeti la Financial Times kuripoti kuwa mawaziri wa fedha wa nchi za G7 watajadili kuachia akiba za mafuta kwa uratibu na International Energy Agency.
Rais wa Marekani, Trump, ambaye alifanya kampeni kubwa kuhusu gharama ya maisha kabla ya uchaguzi wa mwaka 2024, alipuuza ongezeko hilo la bei.
“Bei za mafuta kwa muda mfupi, ambazo zitashuka haraka baada ya tishio la nyuklia la Iran kuharibiwa, ni gharama ndogo sana kulipia usalama na amani ya Marekani na dunia,” Trump aliandika katika mtandao wa Truth Social: “ni wajinga tu wangefikiri tofauti!”
Waziri wa Nishati wa Marekani, Chris Wright, pia, alipunguza wasiwasi kuhusu kupanda kwa bei za nishati mapema Jumapili, alikiambia kipindi cha Face the Nation kwenye televisheni CBS News kwamba ongezeko lolote la bei kwenye vituo vya mafuta litakuwa “la muda tu”.
Bei ya mafuta ghafi imepanda kwa takribani asilimia 50 tangu Marekani na Israel zilipoanzisha mashambulizi ya pamoja dhidi ya Iran Februari 28.
Iran imezuia kwa kiasi kikubwa usafirishaji wa meli katika Mlango Bahari wa Hormuz kama hatua ya kulipiza kisasi, hali inayotishia karibu sehemu ya tano ya usambazaji wa mafuta duniani.
Iraq, UAE na Kuwait, wazalishaji wakubwa wa mafuta ndani ya (OPEC), wamepunguza uzalishaji huku kukiwa na mkusanyiko wa mapipa ya mafuta yasiyoweza kusafirishwa kutokana na kufungwa kwa njia hiyo ya baharini.
Mashambulizi dhidi ya miundombinu ya uzalishaji wa nishati katika eneo hilo pia yameongeza hatari kwa usambazaji. Iran imelaumiwa kwa mashambulizi kadhaa dhidi ya vituo vya nishati katika eneo la Ghuba, ikiwemo katika Qatar, Saudi Arabia na Kuwait.
Jumamosi, Israel ilifanya mashambulizi ya anga yaliyolenga miundombinu ya mafuta ya Iran kwa mara ya kwanza tangu vita vianze.
Kwa mujibu wa vyombo vya habari vya serikali ya Iran, mashambulizi hayo yalilenga vituo vinne vya kuhifadhi mafuta na kituo cha kusafirisha bidhaa za mafuta katika Tehran na jimbo Alborz.
IRGC, Jumapili ilitishia kushambulia miundombinu ya nishati katika eneo lote kama hatua ya kulipiza kisasi, ikionya kuwa bei ya mafuta inaweza kufikia dola 200 kwa pipa ikiwa Marekani na Israel “wataendelea na mchezo huu”.
Mhadhiri wa Chuo cha Diplomasia cha dk Salim Ahmed Salim, Innocent Shoo amesema migogoro ya kimataifa mara nyingi husababisha wawekezaji kuwa waoga. Mitaji huhama kutoka masoko yanayoibukia kwenda kwenye mali zinazochukuliwa kuwa salama.
Amesema Afrika, ikiwa ni pamoja na Tanzania, inaweza kushuhudia kupungua kwa mtiririko wa uwekezaji wa moja kwa moja wa kigeni (FDI) au kucheleweshwa kwa miradi mikubwa ya maendeleo.
Aidha, amesema usumbufu katika usafirishaji wa kimataifa unaweza kuongeza gharama za mizigo, kuathiri biashara ya kimataifa, na kuathiri mapato ya bandari na sekta ya usafirishaji.
“Katika mazingira kama haya, bara la Afrika linaweza kuchukua nafasi ya kuwa sauti ya busara. Kupitia Umoja wa Afrika (AU), nchi za Afrika zinaweza kuhimiza mazungumzo na kupinga kuenea kwa vita.
“Tanzania, yenye historia ya diplomasia ya amani tangu enzi za Mwalimu Julius Nyerere, inaweza kuendelea kusisitiza umuhimu wa suluhisho la mazungumzo badala ya silaha,” amesema Shoo.