Japo sijui umri wala sura zenu, kwa walengwao mjijuao, nitakuiteni waheshimiwa msiojulikana mnaofanya mambo yanayojulikana tena ya kuudhi. Nawapa shikamoo kama ishara ya heshima ila siyo kuwazeesha bali kuwasifia na kuwafurahisheni msiniteke, kunipoteza, hata kunidedisha kama wale wenzangu. Juzi, nilisikitika sana na kushangaa.
Nilihuzunika na kuchukia namna wengine wanavyokasirika na kufyatuka kiasi cha kupayuka na kufyatua waliokuwa wakifyatua kwa vile walidai nanyi mliwafyatua. Cha mno, nilisikitika na kuogopa sana. Ni pale nilipoona mliowazunguka na kuwatumikia wakizuga na kuzugana badala ya kuwashauri wakaamua kujishauri.
Wapendwa na waogopwa tena mlioko juu, kwanza, nikiri. Najua kayani tuna watoi watundu waliokosa adabu, wavuta bangi wanaodaiwa kupenda njuluku kiasi cha kuhongwa na kutaka kubomoa hata kuchoma moto kaya yetu pekee waliyotuachia baba na babu.
Nimehuzunishwa na kushangazwa na wazushao kuwa hawa watoto watundu walihongwa tena na mbuzi dume wachome kaya moto. Wapi ushahidi? Ilinishangaza sana kuona mafyatu wazima wakifanya mambo ya kikumbaff kiaisi.
Yawezekana wamefanya hivyo kutokana kuwa mafyatu wanaoweza kufyatuka na kufyatua lolote ima kugoma au kugopa kuwafyatua tukafyatuana kikaeleweka. Sijui ni kwa sababu ya uzushi au kutaka kukwepa lawama.
Kuna niliowasikia runingani na kuwaona redioni baada ya watoi watundu kufyatuka, kufyatua na kukukera, hawataki fyatu yoyote alalamike wala kuulizia hatma yao.
Wapo waliolalama na kulaani sana wapanzi walioshindwa kuwafunza watoi wao adabu hadi wakaikosa na kutishia kutuumiza wote kayani. Katu, sikubaliani na hii dhana, dhuluma, na rongorongo uchwara. Nadhani kama wangesoma na kucheza na watoi wa maza wa kuwazaa mwenyewe tena munene wenye tabia nzuri na mafanikio, hakika, nao wangekuwa nayo.
Kama wangeshirikishwa na maza wa kambo kwenye kamati ya uendeshaji wa kaya yao kama wake hadi hata warume wao, yote yasingetokea. Hayo leo tuyaache.
Kingine nijuacho, hawa watoi watundu wengi wanatoka shule za Kayumba. Kama wangesoma intaneshno na Kimombo media, wasingekuwa watundu hivi bali kama kuku wa kitasha. Wangekuwa wamezaliwa kwenye hos za bei mbaya, wasingekuwa na utundu wala utukutu bali utanuaji tena wa dezo. Hivyo, nadhani sababu ya watoi kuwa watundu hadi wakataka kuchoma kaya ni ukapuku wa madingi zao. Mtoi anayelala kwenye ngwarangwara akielekea shulee hawezi kuwa na adabu wala tabia. Hawezi kuwa sawa na wale wanaoendeshwa kwenye midude ya bei mbaya ambayo ni full viyoyozi kama wa wanene. Hawezi huyu maskini. Ni kama tunawaonea au hatuwaelewi. Kama tunawaelewa, basi hatuelewi, hawatuelewi na hatuelewani.
Wapendwa, nilishangaa kusikia eti watoi watundu walitaka kuharibu kaya yetu ilhali ilishaharibiwa baada ya kupigwa mnada na ndugu zetu wenye uchu wa njuluku tena wahongwao peremende, udohoudoho, na upuuzi mwingine. Nani zwazwa awahonge njuluku watoi wachome kaya ambayo si yao tena? Au ni wale wenye tabia za mbuzi dume? Nadhani hata mbuzi wanajua kuwa kaya yetu ya urithi ilishapigwa mnada. Hata hivyo, tukiwa wakweli, nani ahongwi nyumbani kwetu? Muonyesheni ili watoi waende kwake wajifunze. Mnakumbuka yule baba aliyetuacha alivyowahi kusema. Kuna kuwa lile shamba la Bwagamoyo lisiuzwe vinginevyo watakavyofanya hivyo wawe machizi na mataahira wasiojua ukubwa na manufaa yake. Je, halikuuzwa?
Yule baba japo alikuwa na yake kama ukali kupita kiasi hata ukatili kiasi cha kuwachapa wenzetu hadi wakatekwa, wakapotea, na kufa, pia, alikuwa na uzuri wake. Nakumbuka. Hakuwahi kupendelea watoi wake na kuwaumiza watoi wa kufikia kama ilivyo. Sikumbuki kuona mtoi wake hata mkwewe au mkamwana kwenye kamati yake ya kuongoza kaya. Kwa hili, sitaacha kumkumbuka mbali na kupambana na wale vidokozi waliokuwa wakiiba na kuramba sukari na kufanya wengine tunywe uji wenye chumvi.
Juzi, kuna watoi wakorofi walivunja vikombe na kupiga mateke sufuria na mambo mengine. Bahati mbaya, wale walinzi wetu si waliwaunguza mikono eti wakiwaadhibu! Mpaka nifyatukapo, wapo waliokimbia kiasi cha kutojulikana walipo. Wapo wanaodai kuwa waliuawa na miili yao kutupwa mbali pasipojulikana kama wale wasiojulikana japo wanatenda jinai na ukatili vinavyojulikana. Wazushi walizua na kuzusha kuwa wale walinzi waliwaua na kuwatupa baharini ilhali maza yao akiangalia na kuwalaumu.
Juzi, nilipita kijiweni. Niliyosikia yanatisha. Kumbe watoi watundu wenzao wanasema lazima walinzi washikwe na kushikishwa adabu hadi wawaonyeshe wenzao au miili yao badala ya kujitoa ufahamu na kukaa kimya kana kwamba waliopotea ni wadudu. Wanataka kujua nani alimuamuru kuua watoi wachanga tena kwa kuonyesha utoto wao. Mashambenga na wabaya wanazoza wazi kuwa kuwa kuna ubaguzi hasa kuwaacha walinzi wawaue kwa vile ni wana wa kufikia.
Nani kawalipa nani na wangapi, nini, kiasi, na lini ili apate nini na kwanini? Je, ‘vyombo’ vilikuwa wapi? Tumuamini na kutomwamini nani?
Kumbe naota! Mgoshi Machungi keshantumia kombora!