Ibenge ataka wawili Azam | Mwanaspoti

AZAM leo itakuwa ugenini kupambana na Dodoma Jiji kwenye mechi ya Ligi Kuu Bara, lakini mezani kwa viongozi wa klabu hiyo kuna mahitaji mawili ya mastaa wapya yaliyoletwa na kocha wa timu hiyo, Florent Ibenge.

Iko hivi; Ibenge bado hafurahii sana ufanisi wa eneo la kushambulia na amewaambia mabosi wake waanze mchakato taratibu kwa kumtafutia mshambuliaji mwingine mwenye makali kwa matumizi ya msimu ujao kwenye kikosi hicho.

Safu ya ushambuliaji ya timu hiyo inaongozwa na Wakongomani wawili, Jephte Kitambala ambaye alianza msimu huu, lakini mpaka sasa amefanikiwa kufunga mabao mawili kwenye ligi akiwa ameshakaribia kumaliza nusu ya msimu na matajiri hao wa Chamazi.

Ibenge dirisha dogo akamuongeza Jean Ngita ambapo tayari amefunga mabao manne Ligi Kuu Bara, huku viungo wawili washambuliaji Feisal Salum ‘Fei Toto’ na Idd Seleman wakiwa ndio vinara wa ufungaji katika timu hiyo kila mmoja akifunga mabao matano.

Msimu ujao, Ibenge anataka mshambuliaji mwingine na inaelezwa mabosi wa kikosi hicho wameshaingia msituni kumtafutia hitaji lake.

Taarifa za ndani zililiambia Mwanaspoti: “Tunatafuta wachezaji wawili, wa kwanza ni mshambuliaji wa kati, kulikuwa na matarajio makubwa kwa Kitambala lakini mambo kama hayaendi kama ambavyo tulitarajia.

“Kocha anataka mtu mwingine mpya, amekuja Ngita unaona kuna kitu ameongeza, lakini bado na huyu ni mdogo, tunataka awe na mtu bora zaidi kabla yake.”

Mbali na mshambuliaji wa kati, Ibenge anataka pia atafutiwe kiungo mshambuliaji namba 10 mwingine bora zaidi au kama Fei Toto na Azam FC bado haina uhakika sana wa kubaki na mchezaji huyo kutokana na ofa zinazokuja.

Taarifa hizo zilisema kuwa: “Kocha pia anataka namba kumi, ukweli ni leo akikosekana Fei unaona tunapata shida sana pale mbele, hizi mechi mbili za mwisho umeona namna tunatengeneza ugumu sana nafasi za mabao baada ya Fei kuwa nje kwa adhabu.

“Kocha anataka mtu kama Fei au zaidi yake na unajua kuna ofa nyingi sana zinakuja, sasa hakuna uhakika kama ataendelea kubaki au anaweza kuondoka.

“Tunatamani kubaki naye lakini wakati mwingine soka ni biashara, zinaweza kuja fedha nyingi mkashawishika kumuuza, sasa ni bora tuwe tumejiandaa sawasawa.”

Azam imemkosa Fei Toto baada ya adhabu aliyoipata kwenye mechi dhidi ya Pamba Jiji na kupelekea kukosa mechi mbili dhidi ya Tanzania Prisons iliyomalizika kwa timu hizo kushindwa kufungana Ligi Kuu Bara na ile ya Kombe la Shirikisho la CRDB dhidi ya Mbeya Kwanza ambayo Azam ilishinda 1-0. Leo dhidi ya Dodoma Jiji anatarajiwa kurejea baada ya adhabu kumalizika.

Baada ya kumalizana na Dodoma Jiji, matajiri hao wa Chamazi watakuwa wenyeji wa Yanga katika Dabi ya Dar es Salaam Machi 15 mwaka huu kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, saa 1:30 usiku.