Hizi ndio sababu Kisena wa ‘Udart’ na wenzake kuachiwa huru

Dar es Salaam. Mahakama ya Rufani Tanzania, imebatilisha hukumu na kufuta adhabu waliyopewa, aliyekuwa mkurugenzi wa Kampuni ya Mabasi Yaendayo Haraka (Udart), Robert Kisena na wenzake wawili na kisha kuwaachia huru.

Kisena na wenzake, Charles Newe aliyekuwa pia mkurugenzi wa Udart na Tumaini Kulwa aliyekuwa Mtunza Fedha (Cashier), Udart, walipatikana na hatia ya makosa ya Uhujumu Uchumi na kufungwa miaka mitatu na kuamriwa kulipa faini.

Kwa mujibu wa hukumu hiyo, Kisena alihukumiwa kifungo cha miaka mitatu na kulipa faini ya Sh200 milioni, Newe naye akahukumiwa kifungo cha miaka mitatu na kulipa faini ya Sh200 milioni, wakati Kulwa yeye alihukumiwa miaka 3 na faini ya Sh100 milioni.

Hukumu hiyo ilitolewa Desemba 22, 2023 na Jaji Elinaza Luvanda wa Mahakama Kuu Divisheni ya Rushwa na Makosa ya Uhujumu Uchumi, lakini jana Jumanne Machi 10, 2026, jopo la majaji watatu wa Mahakama ya Rufani walitengua hukumu hiyo.

Kulingana na hukumu ya jopo hilo, Augustine Mwarija, Pantrine Kente na Zainab Muruke, awali warufani hao walikuwa wamepatikana na hatia katika makosa ya uhujumu uchumi yanayohusisha pia makosa ya utakatishaji fedha haramu.

Kulingana na hati ya mashitaka ya makosa 15 waliyokuwa wakishitakiwa nayo ambayo hata hivyo waliyakanusha, walitenda makosa hayo kati ya Mei 25 na Julai 10, 2016 wakiwa wanatekeleza majukumu yao ya kila siku.

Majaji hao walisema hakukuwa na ubishi wakati mgogoro huo unaoibuka, Kisena alikuwa mkurugenzi wa Udart, Ofisa Mtendaji wa Kampuni ya Simon Group na wakati huo huo Mkurugenzi wa Shirika la Usafiri Dar es Salaam (Uda).

Kwa upande wa mrufani wa pili, Newe, hapakuwa na ubishani kuwa alikuwa ni mkurugenzi Udart, Mtendaji wa Simon Group na mkurugenzi Uda wakati mrufani wa tatu yeye alikuwa akishikilia wadhifa wa mtunza fedha kampuni ya Udart.

Wakirejea hukumu iliyowatia hatiani, majaji hao walisema mrufani wa kwanza na wa pili walipatikana na hatia katika kosa la 1,2,6,11,12, 13 na 14 yaliyohusu utakatishaji fedha na mrufani wa tatu akapatikana na hatia katika kosa la 3 na 14.

Katika kosa la kwanza na la pili, warufani walihukumiwa kifungo cha miaka mitatu jela na kuhusiana na kosa la 6,11 na 12, warufani wa kwanza na wa pili wote walihukumiwa kulipa faini ya Sh100 milioni au kutumikia kifungo cha miaka 5.

Kuhusiana na kosa la 13 na 14, warufani wote walihukumiwa kulipa faini ya Sh100 milioni kila mmoja au kutumikia kifungo cha miaka 5 na katika kosa la kuisababishia hasara Serikali, wote walihukumiwa kifungo cha miaka 3 jela.

Mahakama Kuu chini ya Jaji Luvanda iliamuru vifungo vitumikiwe kwa pamoja (concurrent) lakini katika suala la faini, zilitakiwa zilipwe moja baada ya nyingine, hukumu ambayo hawakuridhika nayo na kuamua kukata rufaa mahakama ya juu.

Katika ushahidi huo, mashahidi wa Jamhuri walijaribu kujenga picha pamoja na mambo mengine, kulikuwa hakuna mgogoro juu ya umiliki wa hisa za Uda na Udart ambazo zilidaiwa na mashahidi kuwa Serikali ilimiliki asilimia 100.

Kwa upande wao, warufani katika ushahidi wao walibaki imara katika msimamo wao kwamba Uda inamilikiwa na ushirikiano (partnership) kati ya Simon Group ikiwa hisa asilimia 51 na Serikali kupitia Msajili wa Hazina ikiwa na hisa asilimia 49.

Hata hivyo, majaji hao walisema haikubishaniwa kwamba Uda ndio alikuwa mmiliki mwenye hisa nyingi za Udart, Shirika lililokuwa likiendesha mfumo wa mabasi yaendayo kwa kasi katika maeneo mbalimbali ya Jiji la Dar es Salaam.

Kutokana na kutoelewana kati ya upande wa mashitaka na warufani kuhusu umiliki wa Uda na Udart, katika hukumu yake jaji alitumia muda kupima kama warufani wana mkono katika fedha zilizodaiwa kuibwa au kutakatishwa.

Mwisho wa siku Jaji Luvanda alikubali msimamo wa mwendesha mashtaka kwamba kimsingi, hakukuwa na mgogoro wa umiliki wa hisa za Uda na Udart na warufani hawakuwa na hisa katika fedha zilizoibwa au kutakatishwa.

Kwa kuzingatia ushahidi mwingine uliotolewa kuunga mkono kesi ya mashtaka, Jaji wa Mahakama Kuu aliona kwamba kosa la 1,2,6,11,12,13 na 14 yalithibitishwa bila kuacha shaka kisha akaendelea kuwatia hatiani warufani hao.

Hoja za Rufaa zilizowatoa

Katika sababu 12 za rufaa, Mahakama iliona sababu ya kwanza na ya pili, wana zilikuwa na dalili za kumaliza rufaa hiyo licha ya mlalamikiwa (Jamhuri) kukata rufaa kuhusiana na adhabu zilizotolewa na Mahakama Kuu chini ya Jaji Luvanda.

Kulingana na sababu hizo, warufani walidai jaji alikosea kwa kukataa kusimamisha na usikilizwaji wa kesi kulipoibuka mzozo kuhusu umiliki wa hisa kati ya Simon Group Limited na Msajili wa Hazina kuhusu umiliki wa Uda na Udart.

Msingi mkuu wa hoja ni kwamba, kwa kuwa Mahakama ilikuwa ni  ya jinai, basi haikuwa na uwezo na wala mamlaka ya kuamua mzozo wa umiliki wa hisa ambao uko chini ya mamlaka ya Mahakama ya madai na sio Mahakama ya Jinai.

Mawakili wa warufani, Deusdedit Luteja na Nduruma Majembe, walijenga hoja kuwa kwa kuwa mgogoro wa umiliki wa hisa kati ya Simon Group kwenye Uda na Udart, basi jaji hakuwa na mamlaka ya kusikiliza hoja zinazohusu kesi ya madai.

Kwa upande wake, wakili wa Serikali Patrick Mwita aliyeongoza jopo la mawakili watano wa Serikali walioiwakilisha Jamhuri, alikiri kulikuwepo na mgogoro wa umiliki wa Uda lakini haraka akasema hapakukuwa na mgogoro kwenye Udart.

Wakili huyo alieleza kuwa, kulikuwa hakuna ubishi Udart inamilikiwa na Uda kwa asilimia 99 na Simon Group inamiliki asilimia 1 tu na kusisitiza kuwa, umiliki wa hisa haikuwa ni hoja (issue) bali Udart ndio ilikuwa imesababishiwa hasara.

Kuhusu hoja ya warufani kuwa makosa hayo yalitokana na mahusiano ya kimkataba kati ya Udart na Longway Engineering Limited inayomilikiwa na warufani, wakili wa Serikali, alisema hapakuwepo mkataba baina ya wawili hao.

Katika hukumu yao iliyowekwa katika tovuti ya Mahakama Machi 11,2026, majaji wa Mahakama ya rufani walisema baada ya kusikiliza hoja za pande mbili, hoja ya kuamuliwa ni kama ushahidi uliotolewa ulihusu pia mgogoro wa umiliki wa hisa.

“Hoja ya kuamuliwa hapa ni kama kulikuwa na mgogoro ama la wa umilikiwa hisa za Uda na Udart na kukiukwa kwa mkataba kati ya Udart na Longway Engineering Limited na kama ndio tutajadili kama jaji alikuwa sahihi,”walisema jaji.

Majaji hao walisema ushahidi wa mashahidi wa nne wa Jamhuri na mrufani wa kwanza (Kisena) kama inavyoonekana katika ukurasa wa 4624 wa hukumu, Mahakama hiyo haikuwa sahihi kuamua imiliki wa hisa kati ya Simo na Msajili.

Lakini jaji katika usikilizwaji huo alikataa hoja ya wakili Majembe kwamba mashitaka dhidi ya wateja wake yanahusu mgogoro wa umiliki wa hisa, na kuchukua mtizamo kuwa hilo lilihusu tu kuamua mgawanyo wa hisa hizo.

“Kulingana na jaji, mgawanyo wa hisa ulikuwa hauna uhusiano wowote na makosa ya jinai yanayowakabili warufani,”walisema majaji hao.

“Kwa kuzingatia masuala ya ushahidi ambayo jaji aliamua kwenda nayo, hatukubaliani na hoja ya wakili Mwita (kiongozi wa jopo la mawakili wa Serikali) kwamba hakukuwa na mzozo wa umiliki wa hisa katika shauri hili.

“Hakuna shaka, juu ya ushahidi wa jumla, kupitia kesi, kuwa umiliki wa hisa ulikuwa katikati ya mzozo huu. Ukweli huu unachangiwa na jaji wa Mahakama ambaye alikwenda kwa maumivu makubwa kuchambua ushahidi na hatimaye kuhitimisha kuwa hapakuwa na mzozo wa hisa katika suala hili.”

Majaji hao walisema ni wazi, katika muktadha wa kesi hii, jaji alishindwa kuzingatia ipasavyo ushahidi uliofichua kutokubaliana kwa umiliki wa hisa ambao ulipaswa kusuluhishwa kwanza kwa njia ya madai ikiwa njia zingine hazikufaulu.

Ni kutokana na sababu hizo, jopo hilo la majaji limebatilisha kutiwa hatiani kwa Kisena na wenzake na kufuta adhabu walizopewa na kuamuru waachiliwe huru kutoka gerezani, labda tu kama wanashikiliwa kwa makosa mengine ya jinai.